Makala

Wanafunzi walezea kuhusu kifaa walichovumbua kuwafaa walemavu

August 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

RICHARD MAOSI NA KATE WANDERI

Salome Njeri na Esther Amimo mwaka huu waligonga vichwa vya habari kwa kushinda tuzo ya kimataifa walipovumbua kifaa kinachoweza kuwasaidia walemavu.

Wanafunzi hao kutoka Shule ya Upili ya Keriko, Kaunti ya Nakuru walijishindia jumla ya Sh200,000 miongoni mwa zawadi nyingine.

Ni uvumbuzi wa kipekee ambao uliashiria kuwa hakuna kisichowezekana katika dunia mradi binadamu atajikakamua na kutumia mawazo yake kujifikisha kwenye hatua nyingine ya mafanikio.

Upekee wa kifaa hiki kilichoshinda tuzo ya kimataifa ni kutokana na uwezo wake, kurahisisha mambo mbali na kutumia malighafi yanayopatikana kwenye mazingira ya kawaida kama vile mbao.

Kifaa hiki kimekopa jina kutoka kwa wanafunzi waliokibuni yaani Esther na Salome kisha wakakipatia jina la ESSA (Esther/Salome)-METER.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, Salome Njeri na Esther Amimo ni mfano wa kuigwa, kwa kuongeza mawazo yao katika ulimwengu wa uvumbuzi kuwakomboa walemavu.

Wanafunzi waliovumbua kifaa hiki walipozuru Marekani kupokea tuzo la kimataifa. Picha/ Richard Maosi

Kifaa chenyewe kilipania kutatua matatizo ya watu wasiokuwa na uwezo wa kusikia na kuona.

Wanafunzi hao wanasema licha ya kuishi mashinani, juhudi zao hazikuwazuia kuingia katika vitabu vya kumbukumbu.

Kulingana na Salome anaona kuwa mbali na kutafuta elimu ya vitabuni, inawapasa wanafunzi kutalii nyanja za utafiti wakati wao wa ziada badala ya kupoteza muda wao mwingi wakitazama filamu.

Mtambo huu una kifaa kinachoweza kuwasaidia vipofu na viziwi kutatua maswala ya Hisabati hasa kupima urefu.

Salome anasema alipata hamasa ya kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo wa kusikia na kuona kutokana na mwalimu wake wa shule ya msingi ambaye hakuwa na uwezo wa kuona wala kuskia.

Licha ya mwalimu huyo kuwa na mapungufu haya alijibidiisha kufundisha somo la Kiingereza na dini kwa ustadi jambo lililowafanya wanafunzi kumpenda.

Salome aliona kuwa ipo siku angekuja kuwa mtu wa manufaa kwa watu wengine wenye mapungufu kama hayo,ndiposa akashirikiana na mwenzake kuvumbua kifaa hiki.

Kifaa chenyewe kinafanana na saa ya ukutani lakini huzimika ghafla pale mtumiaji anapofikia lengo lake.

Lango la Shule ya Upili ya Keriko, Kaunti ya Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na Salome anatarajia kuwa kifaa hiki kitatumika kote ulimwenguni kuwasaidia watu wenye matatizo kama hayo ili waweze kuwa katika nafasi nzuri ya kuendeleza taaluma zao.

Kwa mujibu wa Salome kifaa chenyewe kiligharimu shilingi 100 tu, na kuibuka bora miongoni mwa miradi mingine waliyowakilisha katika mashindano ya kuonyesha ubunifu kwa shule za upili almaarufu kama Science Contest.

“Ingawa mradi wetu ulitumia gharama ndogo cha kushangaza ni jinsi tuliibuka kuwa bora kitaifa na kuwashangaza wengi ambao hawakuwa na mawazo kama yetu,” Salome aliongezea.

Taifa Leo Dijitali ilikutana na Bi Njeri ambaye alifafanua kuhusu namna ya kutumia kifaa hiki adimu.

Alieleza kuwa walikusanya vitu vya kawaida kama vile mbao, nyaya na kalamu kutengeneza kifaa hiki ambacho hawakujua kingewafikisha Ulaya.

Mwaka wa 2017, wanafunzi hawa hawakuwa na uwezo wa kugharamia tiketi ya ndege kuwasilisha kifaa hiki katika ulingo wa kimataifa Arizona, Marekani lakini hawakufa moyo.

Mnamo 2019 walipata habari kuwa wamefanikiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watakaopata ufadhili wa kuwasilisha ubunifu wao mbele ya kijopo cha waamuzi wa Science and Engineering Fair.

Anasema kifaa chenyewe ni rahisi kutumia kwani, hurahisisha kupima urefu, badala ya kutumia rula ambapo watu wengi wasiokuwa na uwezo wa kuona hupata matatizo kutumia rula.

Kwa wasiokuwa na uwezo wa kusikia kifaa chenyewe kina rangi tofauti ambapo kila rangi hutumika kutambulisha nambari maalum.

Salome Njeri anasema kifaa chenyewe kinafaa kuwasaidia walemavu kusoma hisabati. Picha/ Richard Maosi

Na kwa wasiokuwa na uwezo wa kuona , kifaa hiki kina sehemu mbalimbali kama vitufe ambapo mtumiaji anaweza kuvishika na kutambua nambari.

Ni kifaa rahisi ambacho kinaweza kutumia miundo mbalimbali ya rangi kurahisisha upimaji wa urefu kutokana na miundo miepesi ya aina mbalimbali ya rangi na vitufe.

Kulingana na Salome ambaye sasa ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Keriko,anasema kifaa chenyewe kinafaa kuboreshwa ili kiwafikia watumiaji wengine wengi kote ulimwenguni.

Anaona kuwa kitawafaa watumiaji endapo kitashirikisha teknolojia katika matumizi yake ili kuwapunguzia walemavu changamoto za kusoma.

Hivisasa wanalenga kushirikiana na serikali ya kitaifa, kuweka mikakati ya kufanya kifaa chao kiwe katika nafasi ya kutumia teknolojia ili kurahisisha mambo, kwani kimeunganishwa na mbao pamoja na nyaya za kawaida.

Salome anawashauri wanafunzi wenzake kujitahidi masomoni,mbali na kutumia vipaji vyao kujiendeleza kimaisha ili waje kuwa watu wa kutegemewa katika jamii siku za mbeleni.