HabariSiasa

Raila akataa kutoa tiketi ya moja kwa moja Kibra

August 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DAVID MWERE

KINARA wa chama cha ODM, Raila Odinga amesema chama chake hakitatoa tiketi ya moja kwa moja kwa mwaniaji ubunge Kibra.

Akizungumza Jumapili alipowatambulisha wawaniaji 24 wanaotaka tiketi ya chama hicho ili kushiriki kinyang’anyiro cha Novemba 7 kwa wakazi wa Kibra, Bw Odinga alisema wote watalazimika kushiriki mchujo Jumamosi hii.

“Tutawapiga msasa wote 24 kisha wakutane uwanjani Jumamosi kujua yule atakayepewa kibali na wapiga kura aingie debeni Novemba 7. Tukimaliza mchujo huo, tutawasilisha jina kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufikia Septemba 3,” akasema Bw Odinga kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, Kibra.

Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth mwezi uliopita.

Kesho chama hicho kitaanza kuwapiga msasa wanaomezea mate tiketi hiyo, hatua ya kwanza ikiwa ni kuwaondoa wasiokuwa na uaminifu kwa ODM.

Bw Odinga alisema Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya chama chake itakagua maelezo ya wawaniaji, yakiwa pamoja na ni lini walijiunga na chama hicho.

Mkutano wa jana wa kisiasa ulitumiwa na wawaniaji hao kuuza manifesto zao kwa wapiga kura wa Kibra, huku wengi wao wakiahidi kuendeleza sera za marehemu Okoth.

Mkutano huo ulitoa mwelekeo kwa mashambuliano ya kisiasa yanayotarajiwa kutokea katika mchujo wa ODM kwani katika eneo bunge hilo kupata tiketi ya chama hicho huwa ni sawa na kuchaguliwa moja kwa moja.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba huenda Jubilee ikafuata mkondo wa wakati wa chaguzi ndogo za Embakasi Kusini, Ugenya, Kitui Magharibi na Migori ambako ilijiondoa na kuunga mkono wawaniaji wa ODM.

Lakini Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju, jana alisisitiza kuwa chama chake kitafanya mashauriano kwanza kabla ya kutangaza msimamo wake rasmi wiki hii.

Kwenye mkutano wa jana, aliyekuwa mbunge wa Embakasi Kusini, Bw Irshad Sumra alilazimishwa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho cha Kibra alipokemewa na umati.

“Sikuja hapa kuwania kiti. Nimekuja kuungana na watu wa Kibra. Mimi siwanii,” akasema Bw Sumra huku akizomwa.

Ilimlazimu mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa aingilie kati na kuutuliza umati kwa kuutangazia kuwa Bw Sumra hayumo kwenye kinyang’anyiro.

Kakake Okoth, Bw Bernard Otieno Imran pia alipata wakati mgumu umati huo ulipomzoma kuhusiana na kuchomwa kwa marehemu kakake badala ya kuzikwa kulingana na mila ya jamii ya Waluo.