• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Selfie kutumika kupima presha

Selfie kutumika kupima presha

Na LEONARD ONYANGO

UKIWA una simu aina ya ‘smartphone’ kuna uwezekano mkubwa kwamba karibu nusu ya picha zilizomo ni za selfie.

Kwa vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 25, inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya picha walizo nazo kwenye simu ni za selfie.

Ripoti iliyotolewa mnamo 2015 na kampuni ya kutoa huduma za Intaneti, Google, selfie zaidi ya bilioni moja hupakiwa kwenye mtandao wake kila mwaka kote duniani.

Google hutumia teknolojia kubaini ikiwa picha iliyopakiwa katika sava zake ni ya selfie au la.

Utafiti uliofanywa nchini India mwaka 2018 ulibaini kwamba watu 250 walifariki wakinasa selfie kati ya 2011 na 2017 kote duniani.

Wengi hupiga selfie na kisha wanachagua zinazopendeza na kuzipakia kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, Twitter, Snapchat na kadhalika.

Mbali na kutumia picha hizo kujifurahisha katika mitandao ya kijamii, wapenzi wa selfie sasa huenda wakazitumia kujua hali yao ya kiafya.

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Toronto, Canada na Hospitali ya Hangzhou Normal, nchini China, tayari wametengeneza programu (app) ambayo itawezesha wapenzi wa selfie kujua ikiwa wako katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu au la.

Maradhi ya shinikizo la damu huua watu ghafla bila waathiriwa kuonyesha dalili za kuugua.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watu watatu kati ya 10 wanaugua maradhi ya shinikizo la damu kote duniani.

Inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya Wakenya wanaugua maradhi haya, japo wengi wao hawajui.

Damu ya waathiriwa wa shinikizo, husafiri kwa kasi katika mishipa hata wanapokuwa wamepumzika. Damu inaposafiri kwa kasi mwilini, kuna hatari ya mwathiriwa kupatwa na maradhi ya moyo au kiharusi.

Viungo vinavyohitaji damu kila mara kama vile mapafu, mishipa, ubongo na macho pia huathirika.

Kulingana na Hali ya Uchumi iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS), yapatao watu 5,000 hufariki kila mwaka humu nchini kutokana na maradhi yanayohusiana na shinikizo la damu.

Hiyo inamaanisha kwamba takribani watu 13 hufariki kila siku nchini Kenya kutokana na ugonjwa huo.

Programu

Lakini vifo hivyo huenda vikapungua endapo programu ya kutambua shinikizo la damu kupitia picha au video za selfie itaanza kutumika.

Watafiti hao walichapisha ushahidi wao kwenye jarida la utafiti wa kisayansi linalomilikiwa na taasisi ya kutafiti maradhi ya moyo nchini Amerika, ambapo walithibitisha kwamba picha za selfie zinaweza kutumiwa kutambua shinikizo la damu.

Programu hiyo inayofahamika kama Transdermal Optical Imaging inatambua ikiwa mtu ana shinikizo la damu au la kwa kutathmini video fupi ya selfie.

Inatumia teknolojia inayochanganua mishipa iliyoko kwenye ngozi na kubaini ikiwa inasafirisha damu yenye kasi ya juu kupita kiasi au la, kulingana na Profesa Kang Lee wa Chuo Kikuu cha Toronto anayeongoza watafiti hao.

Katika kuifanyia majaribio, watafiti walihusisha watu 1,328 kutoka Canada na China.

Watafiti hao walinasa video za nyuso za washiriki hao kwa kutumia simu aina ya iPhone na kisha kuzitathmini kwa kutumia Transdermal Optical Imaging.

Baadaye waliwapima watu hao kwa kutumia mashine ya kawaida ambayo hutumiwa kupima presha ya damu hospitalini.

Watafiti walibaini kwamba matokeo ya programu hiyo na mashine ya kawaida inayotumiwa hospitalini yalikuwa sawa kwa asilimia 95.

Profesa Lee alisema kuwa wangali wanafanya majaribio zaidi kabla ya kuanza kuitumia kukabiliana na maradhi ya shinikizo la damu.

“Majaribio yalifanyiwa watu wa ngozi nyeupe ila kuna haja ya kuitumia kupima watu wa ngozi nyeusi ili kubaini ikiwa matokeo yatakuwa sawa kabla ya kuanza kutumika katika vipimo vya presha ya damu,” akasema Prof Lee.

 

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Uraibu hatari kwa afya na mazingira pia

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mabadiliko ya tabianchi tishio kuu...

adminleo