• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Mabadiliko ya tabianchi tishio kuu kwa ajira

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mabadiliko ya tabianchi tishio kuu kwa ajira

Na LEONARD ONYANGO

JACK Omondi amegeukia kazi ya kutengeneza makaa katika Mlima Gembe, Kaunti ya Homa Bay baada ya juhudi zake za kupata kazi kuambulia patupu.

Bw Omondi, 30, anasema kuwa baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari miaka sita iliyopita, alitumai kwamba angepata kazi ya kumwezesha kujikimu kimaisha.

“Kila mwaka nimekuwa nikijaribu kujiunga na kikosi cha polisi na hata jeshi lakini sijafanikiwa. Kwa sasa nimesalia na mambo mawili; kuvua samaki katika Ziwa Victoria au kutengeneza makaa ili nilishe familia yangu,” anasema.

Anasema kuwa tofauti na miaka ya zamani alipokuwa mtoto ambapo Mlima Gembe ulifunikwa na miti, sasa ni kukavu kama jangwa la Sahara.

Bw Omondi ni mmoja tu kati ya maelfu ya vijana ambao wamegeukia biashara ya makaa kwa kukata miti kiholela.

Ukataji wa miti kiholela ni miongoni mwa mambo yanayochangia katika kuongezeka kwa joto duniani.

Ripoti iliyotolewa Julai na Shirika la Wafanyakazi Duniani (ILO) inaonyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yatasababisha ukosefu wa nafasi za ajira milioni 80 kote ulimwenguni kufikia 2030 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Mabadiliko ya tabianchi husababisha kuwepo kwa joto kupita kiasi au mafuriko makubwa yanayoleta uharibifu wa mazao.

Kwa mujibu wa ripoti, Bw Omondi na wenzake, ni adui wa watoto wao kwani hawataweza kupata nafasi za ajira katika miaka ya usoni.

Sekta ya kilimo ndiyo itaathiriwa zaidi ikifuatiwa na utalii, usafiri, michezo na viwanda.

Ripoti ya ILO pia inatabiri kwamba saa za kufanya kazi pia zitapungua kutokana na kuwepo kwa joto jingi.

Humu nchini, zaidi ya vijana milioni 5.5 hawana ajira.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia, itabidi Kenya ibuni zaidi ya nafasi 900,000 za ajira kati ya sasa na 2025 ili kuwezesha mamilioni ya Wakenya wanaosaka ajira kupata kazi.

Ripoti kuhusu Hali ya Uchumi iliyoandaliwa na KNBS ilifichua kuwa serikali ya Jubilee imefanikiwa kubuni nafasi milioni 1.8 tu tangu kutwaa hatamu za uongozi mnamo 2013.

Mbali na uhaba wa ajira, ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa mapema Agosti inaonyesha kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na tatizo la ukosefu wa chakula duniani inaongezeka kwa kasi kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Idadi ya watu wanaokumbwa na baa la njaa imefikia watu 820 milioni kote duniani.

Watafiti wanasema ulimwengu unahitaji kupanda miti trilioni moja ili kuzuia madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Wanasayansi kutoka Uswisi, kupitia utafiti wao uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Science Daily, dunia ina eneo kubwa linalotosha kupanda miti.

“Upanzi wa miti ndio njia ya pekee ya kukabiliana na joto jingi ambalo husababisha ukame katika maeneo mbalimbali,” akasema Thomas Crowther, mmoja wa watafiti katika Taasisi ya Teknolojia ya Serikali ya Uswizi.

Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko anasema kuwa serikali tayari imeanza harakati za kuhakikisha kwamba asilimia 10 ya ardhi ya Kenya inafunikwa kwa miti kufikia 2022.

Kuafikia hilo, kulingana na Bw Tobiko, Wakenya wanahitajika kupanda miche 1.8 bilioni ndani ya miaka mitatu ijayo.

“Wakenya wote, wazee kwa vijana wanafaa kujitokeza na kupanda miti mingi ili tuokoe nchi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” anasema Bw Tobiko.

You can share this post!

Selfie kutumika kupima presha

PATA USHAURI WA DKT FLO: Makamasi kooni yazima starehe

adminleo