• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Gozi kati ya Gor na Tusker sasa kusakatiwa Kisumu

Gozi kati ya Gor na Tusker sasa kusakatiwa Kisumu

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 18 na washikilizi wa taji la Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia wameratibiwa kufungua kampeni zao za msimu huu katika kipute hicho dhidi ya Tusker FC mjini Kisumu badala ya Machakos jinsi ilivyokuwa imepangwa awali.

Haya ni kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Omondi Aduda. Mchuano huo umepangwa kuanza saa kumi na robo jioni, muda mfupi baada ya kukamilika kwa kivumbi kati ya mabingwa mara nne Ulinzi Stars na limbukeni Kisumu All Stars.

“Gor Mahia ndio wenyeji wa mchuano huo. Usimamizi umeamua kuihamisha mechi yenyewe kutoka ugani Kenyatta, Machakos hadi Moi, Kisumu,” akasema Aduda kwa kusisitiza kwamba kiini cha mabadiliko hayo ni kuwapa mashabiki wa Gor Mahia burudani tosha hasa ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha ufuasi wao jijini Kisumu.

Aidha, Aduda ameshikilia kwamba tiketi zote kwa mashabiki watakaohudhuria mechi hiyo zitatolewa kwa njia ya kielektroniki.

“Tumepania kuikumbatia njia hii ya kielektroniki kuwatoza mashabiki ada ya kiingilio ili iwe sehemu ya mikakati mipya itakayotuwezesha kupata fedha za kuendeshea masuala mbalimbali ya klabu,” akasema kinara huyo.

Gor Mahia watalenga kuanza vyema kampeni zao kwa kutia kapuni alama zote tatu dhidi ya Tusker ambao chini ya kocha Robert Matano, wamejishughulisha vilivyo sokoni kadri wanavyopania kunyanyua ubingwa wa KPL kwa mara ya 12 muhula huu.

Hamasa

Ushindi kwa Gor Mahia utawapa pia hamasa ya kujiandaa vyema kwa mechi ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya USM Alger ya Algeria ambao wamepangwa kukutana nao katika raundi ya pili ya mchujo.

Chini ya kocha Steve Pollack, Gor Mahia watachuana na USM Alger ugenini kati ya Septemba 13-15 kisha Kupiga mechi ya marudiano jijini Nairobi kati ya Septemba 27-29. Gor Mahia watapania kutinga hatua ya makundi ya CAF Champions League kwa mara ya kwanza katika historia.

Msimu jana, walishindwa kusonga mbele baada ya raundi ya pili kutokana na wingi wa mabao ya ugenini.

You can share this post!

Hamdok achukua hatua za kutaka kuiondoa Sudan kwenye orodha...

Jubilee yaruka Mariga katika Kibra

adminleo