Makala

SEKTA YA ELIMU: Mwongozo huu mpya utapiga jeki masomo ya mtoto wa kike

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

VISA vya wanafunzi wa kike kukatiza masomo yao baada ya kupachikwa mimba ni baadhi ya changamoto zinazokumba azma ya serikali ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu ya kimsingi.

Japo shule nyingi zinazofadhiliwa na serikali huwapa wanafunzi kama hao nafasi ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua, baadhi ya zile zinazodhaminiwa na makanisa huwafukuza kabisa wanafunzi waliopata uja uzito kwa kuvunja kanuni ya dini inayopiga marufuku ngono kabla ya ndoa.

Imebainika kuwa wanafunzi wa kike ambao hupata mimba wakiwa shuleni aghalabu huathirika kutokana na unyanyapaa na kuhisi kutengwa, hali inayopelekea wengine wao kuvunjika moyo na kukataa masomo.

Visa hivi vimekithiri zaidi nchini hivi kwamba mwaka uliopita idara ya watoto iliripoti kuwa jumla ya wanafunzi 13,624 wa kati ya umri wa miaka 15 na 19 walipata mimba wakiwa shuleni katika kaunti ya Kilifi.

Baadhi yao, ilibainika, walijifungua katika kipindi cha mtihani ya kitaifa ya darasa na nane (KCPE) na ule wa kidato cha nne (KCSE).

Lakini kulingana na mwongozo mpya uliotayarishwa na serikali, walimu wakuu wa shule zote za msingi na upili sasa wanatakiwa kuwaruhusu wasichana waliojifungua kurejea shuleni miezi sita baada ya kujifungua.

Wasichana hao pia wanaweza kurejelea shuleni mwanzoni mwa kalenda mpya ya masomo.

Kulingana na mwongozo huo kwa jina, “National Guidelines for School Re-entry in Basic Education” watu wazima ambao watawapachika mimba wanafunzi wa kike watajipata pabaya kwa sababu walimu wakuu wanahitajika kutoa habari kwa polisi au Idara ya Watoto ili wanaume hao kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kulingana na Sheria kuhusu Uhalifu wa Kingono, mwanamume anayepatikana na hatia ya kushiriki ngono na mtoto (mwenye umri wa miaka 17 kwenda chini) atashtakiwa kwa ubakaji, kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani.

Sasa mwongozo huu, ulioandaliwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika sekta ya elimu, sasa unasubiri kutiwa saini na Waziri wa Elimu George Magoha ili mapendekezo yake yaanze kutekelezwa katika shule zote za umma na kibinafsi kote nchini.

“Usimamizi wa shule, wanafunzi na wazazi wanahitajika kutia saini stakabadhi maalum ya kuonyesha kujitolea kwao kuhakikisha kuwa mtoto anarejea shuleni”.

“Na ili kuondoa shida ya unyanyapaa na hisia ya kutengwa wizara inaruhusu mwanafunzi kusajiliwa katika shule nyingine,” hati hiyo inasema.

Mimba

Sera hiyo mpya ya kitaifa pia inawataka walimu wakuu na Tume ya Kuajri Walimu Nchini (TSC) “kutoa adhabu kali” kwa walimu ambao watapatikana na hatia ya kuwapachika wanafunzi mimba.

Hata hivyo, takwimu kutoka katika tume hiyo inaonyesha kuwa ndani ya kipindi cha miaka minane iliyopita imewapiga kalamu jumla ya walimu 1,077, wa kiume, kwa makosa ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KSSHA) Kahi Indimuli ameitaja sera hiyo kama hatua muhimu ya kuhakikisha watoto wanaendelea na masomo yao.

“Ni wajibu wa pamoja kwa wadau wote kuhakikisha kuwa watoto wanasoma katika mazingira salama shuleni. Mwongozo huu utasaidia wanafunzi lakini tutahitaji usaidizi kutoka kwa wazazi ambao wengine wao nyakati hiyo wametekelekeza wajibu wao wa malezi na kuwaachia walimu jukumu hilo,” akasema.

Na huku akipongeza mwongozo huo Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) Nicholas Maiyo aliowanya wazazi ambao huingia mkataba na wahalifu ili kuwasaidia kukwepa mkono wa sheria.

“Wizara inafaa kuwa macho kuhakikisha kuwa wazazi kama hawa pia wanaadhibiwa kwa kugeuka washirika katika unyama unaotendewa watoto wa kike,” akasema.