Habari Mseto

Punjani apiga polisi chenga katika uwanja wa ndege JKIA

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN na MOHAMED AHMED

MSHUKIWA wa ulanguzi wa dawa za kulevya, Ali Punjani aliwapiga chenga tena maafisa wa polisi waliokuwa wakisubiri kumtia mbaroni katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.

Polisi walikuwa wakimsubiri bwanyenye huyo tangu asubuhi na mapema mnamo Jumatatu lakini hakuwasili kutoka India kama walivyotarajia.

Mapema Agosti 2019 polisi walivamia makao yake mtaani Nyali jijini Mombasa lakini wakapata alikuwa tayari ameondoka nchini na kwenda India.

Mshukiwa huyo alitarajiwa kurudi nchini Jumatatu wiki hii akitumia ndege ya KQ iliyopangiwa kutua saa nne na dakika ishirini asubuhi, lakini hakufika na polisi wanachunguza alikotowekea.

Ndege hiyo ambayo iliondoka jijini Mumbai nchini India, ilitua katika uwanja wa JKIA kama ilivyopangiwa lakini mshukiwa huyo hakuwa miongoni mwa abiria waliofika.

Orodha ya abiria waliofaa kutumia ndege hiyo ilionyesha Bw Punjani baadaye alipaswa kusafiri kwa ndege iliyoondoka saba na nusu mchana kutoka JKIA na kuwasili uwanja wa ndege wa Moi jijini Mombasa saa nane na nusu mchana.

Mmoja wa maafisa wanaomchunguza mshukiwa huyo alithibitisha kuwa mfanyabiashara huyo hakuingia nchini kama alivyotarajiwa.

“Huyo jamaa bado hajarudi nchini. Tunafanya uchunguzi kujua ikiwa aliondoka India kuelekea kwingine,” alisema afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Wiki tatu

Bw Punjani amekuwa nchini India kwa wiki tatu ambako habari zilidai alifanyiwa upasuaji wa moyo.

Mfanyabiashara huyo alipelekwa India baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu katika hospitali ya Heart Lung jijini Mombasa.

“Mgonjwa huyo (Bw Punjani) alilazwa (Mombasa) Julai 29 baada ya kupata ugonjwa wa moyo. Anapaswa kufanyiwa upasuaji wa moyo ili kuthibiti shida iliyopo. Ameshauriwa atibiwe wiki ijayo,” barua ya matibabu iliyotiwa saini na Dkt N. Chaudhry ilisema.

Akiwa India, polisi walifanya msako katika nyumba yake ya kifahari kwa siku mbili na kuwakamata washukiwa watatu ambao walishtakiwa.