• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Washirika wa Ruto magharibi waonywa

Washirika wa Ruto magharibi waonywa

NA SHABAN MAKOKHA

WANDANI wa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Magharibi wamewaonya wenzao katika kundi la Tangatanga wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kujitayarisha kwa kinyang’anyiro kikali 2022.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Seneta Cleophas Malala waliwaeleza wabunge kutoka eneo hilo wanaompigia debe Dkt Ruto kwamba, watajutia uamuzi wao baada ya kuadhibiwa na wapigakura ambao hawavutiwi kwa vyovyote na ziara wanazofanya kila wikendi katika kaunti za eneo hilo.

“Magharibi ni nyumbani kwa muungano wa Nasa ambao bado ungali hai. Wenzetu wa Tangatanga ambao wana mazoea ya kukita kambi hapa kila wikendi wanafaa kufahamu hawatapata uungwaji mkono wowote; tutawakabili. Lazima waheshimu viongozi wa hapa wakati wa ziara zao,” akasema Bw Oparanya.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Magavana Nchini (COG) aliwaomba Wakenya kuwa na subira kuhusu kura ya maamuzi akisema Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wapo kwenye mchakato wa kuleta mageuzi makubwa katika siasa za Kenya.

“Msihadaike kuunga Punguza Mizigo kwa sababu kuna mambo mengi yanayofaa kushughulikiwa ambayo hayapo kwenye mswada huo unaodhaminiwa na kiongozi wa Third Way Alliance. Tulieni hadi ripoti ya kamati ya maridhiano ya BBI itolewe,” akaongeza Bw Oparanya.

Gavana huyo ambaye pia aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Butere alisema ni ripoti ya BBI pekee itakayotoa mwanga wa mabadiliko na kusafisha siasa za nchi.

Kwa upande wake, Bw Malala ambaye ni Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Seneti alisema, Nasa haijajiunga na Jubilee ila inashirikiana na Rais Kenyatta kufuatia muafaka kati yake na Bw Odinga, maarufu kama Handsheki, mnamo Machi 2018.

“Kundi la Tangatanga linafaa kuzinduka na kufahamu Nasa haipo ndani ya Jubilee. Wakati unakuja ambapo watafahamu msimamo wetu,” akasema Bw Malala.

Akizungumza katika eneo la Kanyumba, Kaunti ya Siaya, seneta huyo alifichua kwamba vurugu zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wenye utata wa 2017 zilitishia kusambaratisha taifa hili ndiposa vigogo wengine wa Nasa walisalimu amri na kuamua kuendesha siasa za kimyakimya ili ukuuaji wa uchumi unaoshuhudiwa usitatizwe.

Bw Malala alitabiri kwamba kivumbi cha kugombea Urais 2022 kitakuwa kikali na akawataka wanaomvumisha Dkt Ruto Magharibi kuwa tayari kutemwa na wapiga kura debeni.

Huku Bw Oparanya akishikilia kwamba atawania urais, Bw Malala hakufichua kiongozi atakayemuunga mkono wakati wa uchaguzi huo.

Naibu Rais amekuwa akishutumiwa na wandani wa Bw Odinga na kundi la Kieleweke kwa kuendesha kampeni za mapema kinyume na agizo la Rais Kenyatta.

Ingawa alinukuliwa mara kadhaa akiapa kumuunga mkono Dkt Ruto mnamo 2022 katika kipindi cha kwanza cha utawala wake, Rais Kenyatta amesalia kimya huku ushirikiano wake na Bw Odinga ukifasiriwa na baadhi ya viongozi kama njia ya kuzima nia ya naibu wake kutwaa uongozi kwenye uchaguzi huo.

Naibu Rais amepata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge Ben Washiali (Mumias Mashariki), Benard Washiali (Ikolomani), Emmanuel Wangwe (Navakholo), Dan Wanyama (Webuye Mashariki), Malulu Injendi (Malava), Charles Gimose (Hamisi) Dismus Baraza (Kimilili) na John Waluke (Sirisia).

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale na aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa pia wamekuwa wakimkaribisha Dkt Ruto katika eneo la Magharibi ambalo ni ngome ya Bw Odinga.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula pia siku za nyuma waliwaonya wabunge wanaomshabikia Dkt Ruto wakiwataka wawe tayari kushindwa 2022 wakikosa kuunga mkono mwaniaji kutoka jamii ya Waluhya.

Ingawa Mabw Mudavadi na Wetang’ula walieleza nia ya kuunganisha vyama vyao kama njia ya kuhakikisha kura za jamii ya Waluhya zinaelekezwa kwenye kikapu kimoja, juhudi hizo bado hazijafanikiwa huku kila mmoja wao akionekana kuvumisha azima yake ya kumrithi Rais Kenyatta atakapostaafu 2022.

You can share this post!

Utata wa wauaji kiwandani kuvaa sare za polisi

Serikali yakanusha madai ya kufurusha wakazi Mau

adminleo