• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
NDIVYO SIVYO: Pana ukuruba wa kiumbo katika muamana na muamala, si maana

NDIVYO SIVYO: Pana ukuruba wa kiumbo katika muamana na muamala, si maana

Na ENOCK NYARIKI

TUTAYAANGAZIA maneno mawili ambayo japo hayajazoeleka katika mazungumzo ya kila siku, wachache wanaoyatumia huyatumia visivyo au hutatizika wasifahamu ni neno lipi litumiwe katika muktadha gani.

Maneno muamana na muamala yanakaribiana sana kiumbo.

Kinachoyatofautisha maneno yenyewe kimaana ni sauti /n/ na /l/.

Katika Kiswahili, sauti hizi hujulikana kama fonimu.

Ingawa hatutaingilia sana ufafanuzi wa fonimu kwa sababu makala haya yanamhusu zaidi msomaji wa kawaida kuliko mtaalamu wa isimu, ni muhimu kutaja kwamba fonimu hujitokeza kwenye maneno yenye idadi sawa ya sauti kama maneno mawili tuliyoyataja.

Aidha, maneno hayo sharti yawe na mpangilio sawa wa sauti.

Sasa tuingie kwenye kitovu cha mjadala huu. Neno muamana inawezekana linatokana na kitenzi amini. Fasiri ya Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza ya neno muamana ni “trust”.

Kisawe kingine chalo ni “reliability”.

Tunaposema kwamba mtu hana muamana, basi tunamaanisha kuwa mtu mwenyewe hawezi kuaminika au kutegemewa kutimiza ahadi.

Kamusi Elezi ya Kiswahili inataja neno itibari kuwa kisawe cha muamana. Hakika neno itibari linasaidia katika kutupa maelezo zaidi ya neno hilo la kwanza; hali ya kuwa na imani na heshima kwa mtu.

Kuna neno ‘amana’ ambalo maana yake ya pili ina uhusiano na maneno imani na amini. Amana ni kitu alichokabidhiwa mtu akihifadhi mpaka siku mwenyewe atakapokihitaji.

Kwa maana nyingine, amana ni anachoaminiwa mtu kukiweka mpaka mwenyewe atakapokihitaji.

Neno muamala nalo lina maana mbili zinazokurubiana mno. Maana ya kwanza ni hali ya maelewano baina ya watu nayo maana ya pili ni maelewano mazuri baina ya wanaofanya biashara.

Neno jingine linaloweza kutumiwa kuleta maana ya kwanza tuliyoitaja ni mkabala. Kamusi Elezi ya Kiswahili inaeleza kuwa mkabala ni uhusiano baina ya mtu na watu wengine au kikundi cha watu na kingine. Mfano: Juma hana mkabala na wanakijiji wenzake kwa kuwa ni mtu mwenye majivuno mengi. Maana nyingine ya neno mkabala ambayo haina uhusiano na maana tuliyokwisha kuifafanua ni ‘‘mbele ya’’.

Neno hilo linaweza kutumiwa pamoja na A-unganifu “wa” au kihusishi “na”. Kwa hivyo, tunaweza kusema “mkabala wa” au “mkabala na”. Mfano katika sentensi: Hamisi amesimama mkabala na| wa makavazi ya umma.

Alhasili, neno muamana lina maana ya hali inayomfanya mtu kuheshimika na kuaminika ilhali muamala ni uhusiano baina ya mtu na mtu mwingine au baina ya mtu na kikundi cha watu.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Wadai kunipenda lakini nikieleza nina...

GWIJI WA WIKI: Timothy Sumba

adminleo