• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
SIMON MUKUHA: 1959 hadi 2019

SIMON MUKUHA: 1959 hadi 2019

Na MWANGI MUIRURI

JUMATATU, Agosti 26, 2019, ilikuwa ni tanzia kwa jumuiya ya maduka ya Naivas ambapo mwenyekiti wake, Simon Mukuiha aliaga dunia majira ya jioni katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Kulingana na habari rasmi kutoka kwa wasemaji wa familia na uwekezaji wake, marehemu alifariki baada ya kukumbwa na matatizo ya moyo.

“Tumepoteza baba wa kijamii, mfadhili wa wanyonge na aliyekuwa na maono kuhusu kuinua maisha ya Wakenya kupitia uwekezaji,” akasema aliyekuwa mkuu wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi akihojiwa na Taifa Leo.

Akaongeza: “Mukuha nilimfahamu vyema, alikuwa rafiki yangu na katika hali hii yake ya mauti, nasononeka na ninaomba tu waliobakia katika usimamizi wa maduka hayo wawajibikie kuyahifadhi na kuyakuza hadi kwa ufanisi mkuu kwa kuwa hayo ndiyo yalikuwa maono ya mwendazake.”

Akiwa na ndugu yake David Kimani, wawili hao ndio walikuwa injini ya supamaketi hizo na kwa sasa akienda zake ameacha nyuma mjane na watoto wanne.

Kwa leo hii, maduka hayo ni ushahidi tosha wa jinsi bidii na ueledi pamoja na uvumilivu huishia kuwalisha mbivu wanaofuatilia maadili hayo.

Karibu miaka 30 iliyopita, duka moja lilizinduliwa katika eneo la Rongai katika Kaunti ya Nakuru likiwa la kawaida tu na ndilo limeishia kuwa baba na mama wa supamaketi zote za Naivas ambazo hushuhudiwa katika pembe nyingi za taifa hili.

Kifo cha mzazi

Miaka tisa iliyopita, Bw Mukuha alimpoteza babake mzazi, Peter Kago na ambaye ndiye alikuwa mwanzilishi wa biashara hii ya Naivas.

Marehemu Kago ni ndugu yake Joram Kamau, ambaye ndiye naye mwanzilishi wa Tuskys.

Taswira inayojichora hapo ni familia yenye bongo la kibiashara na pengine ukiritimba katika safu ya dukakuu baada ya mengine kama Uchumi na Nakumatt kujipata katika changamoto za kifedha.

Huku kwa sasa kukiwa na kesi tele kortini katika uhusiano wa Naivas na Tuskys, bado wengi wanampa kongole mwendazake Mukuha kwa kuzingatia umakinifu wa kushughulikia kesi hizo bila kuathiri upanuzi wa Naivas ambao umezaa matunda kwa kuwa na maduka au matawi zaidi ya 50 kwa sasa.

Mwaka wa 2011 kampuni ya biashara sawa na hii ya Naivas kutoka Afrika Kusini ikifahamika kama Massmart na ambayo kwa upande mwingine iko na ushirika na ile ya Amerika ya Walmart, ilizindua mazungumzo ikitaka kununua hisa za Naivas.

Hata hivyo, mazungumzo hayo hayakwenda mbali baada ya mizozo ya kifamilia kuhusu umiliki kuchacha.

Hadi akikumbana na kifo Bw Mukuha alikuwa ametangaza mradi wa Sh176 milioni wa kuwatuza wateja wake.

Umiliki kamili wa Naivas unamwonyesha marehemu Mukuha akiwa na asilimia 25 ya hisa za Naivas, nduguye anayefahamika kama Kimani akiwa na mgao sawa, akina dada zao wakifahamika kama Linet Wairimu na Grace Wambui wakiwa na asilimia 15 kila mmoja.

Asilimia 20 inayosalia huwa ni ya baba yao na kwa kuwa ni marehemu, faida hugawanwa tena na hawa wanne kwa kiwango sawa na asilimia ya hisa zao.

You can share this post!

HASSAN OLE KAMWARO: 1944 hadi 2019

Kamishna mkuu KRA awaonywa wanaokwepa kulipa ushuru

adminleo