Hofu maiti 97 zisizotambuliwa kutapakaa Mbagathi Hospital
Na COLLINS OMULO
SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi, imetoa wito kwa wakazi kujitokeza na kutambua zaidi ya mili 90 iliyohifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Mbagathi.
Msimamizi wa Sekta ya Afya katika kaunti hiyo, Mohamed Dagane, alisema mili 97 ambayo haijatambuliwa imekuwa katika mochari ya hospitali hiyo kwa miezi kadha huku baadhi ikiwa imehifadhiwa tangu mwaka jana.
Alisema mili hiyo ilianza kurundikana katika mochari hiyo mnamo 2018 wakati mili 70 ilipelekwa humo lakini haikuchukuliwa; mili mingine 27 iliwasilishwa tangu mwanzo wa mwaka, huku miili 12 ikiwasilishwa mnamo Aprili pekee.
Bw Dagane alisema kwamba, miongoni mwa miili hiyo 97, 56 ni ya wanaume huku mingine ikiwa ya wanawake.
“Tumegundua kwa wasiwasi mwingi kuwa idadi kubwa ya mili imo kwenye mochari kwa sababu hakuna yeyote ameshughulika kuja kuitambua na kuichukua.
“Tutaandaa notisi rasmi itakayochapishwa magazetini ikiwa na majina ya mili 97 ambayo haijachukuliwa wala kutambuliwa,” alisema Bw Dagane jana.
Alisema kuwa familia za marehemu zitapatiwa muda wa kutambua miili hiyo na kuichukua huku itakayosalia ikizikwa kuambatana na Sheria kuhusu Afya ya Umma.