Watu 3 milioni hatarini kufa njaa sababu ya ukame mkuu
CAROLYNE AGOSA na BENSON MATHEKA
WAKENYA milioni mbili unusu wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka pakubwa kufikia mwezi Oktoba.
Kulingana na ripoti ya shirika la kitaifa la kutathmini viwango vya ukame nchini (NDMA), hali inazidi kuwa mbaya.
Hii imetokana na maeneo mengi kukosa kupata mvua ya kutosha miezi ya Machi hadi Mei, hususan katika maeneo kame.
NDMA ilisema hali itazidi kudorora zaidi iwapo mvua inayotarajiwa Oktoba hadi Desemba haitanyesha.
“Kufikia sasa, idadi ya watu wanaohitaji chakula cha dharura imetimu 2.6 milioni kutoka watu 1.6 milioni mnamo Mei wakati wa tathmini ya baada ya mvua ndefu,” ilisema ripoti hiyo ya NDMA.
Aidha, ripoti hiyo iliendelea kusema, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka kutoka watu 1.1 milioni mnamo Februari, baada ya ripoti ya kutathmini matokeo ya mvua fupi iliyonyesha Oktoba-Desemba mwaka jana.
“Kuambatana na mwelekeo huu, idadi ya watu inatarajiwa kupanda hadi zaidi ya milioni tatu katika miezi mitatu ijayo hadi kufikia Oktoba 2019. Hata hivyo, mvua ikikosa kunyesha msimu ujao, hali itadorora kabisa,” ilionya ripoti.
Ripoti hiyo iliandaliwa baada ya uchunguzi uliofanywa katika kaunti 23 kame na kavu. Hizi ni pamoja na Turkana, Mandera, Wajir, Garissa, Lamu, Kwale, Kilifi, Tana River, Taita Taveta, Kitui, Makueni, Embu (Mbeere), Nyeri (Kieni), Meru Kaskazini, Pokot Magharibi, Baringo, Kajiado, Narok, Marsabit, Laikipia, Tharaka Nithi, Samburu na Isiolo.
Kwa ujumla, mvua ya masika ilikuwa ya kiwango cha chini na nyepesi katika maeneo hayo. Aidha, ilianza kuchelewa – kwa siku zaidi ya 40, ingawa ilikamilika wakati unaotarajiwa na hivyo kumaanisha kuwa msimu halisi wa mvua ulikuwa mfupi kwa siku 40.
Katika kipindi cha utathmini, kulishuhudiwa mikurupuko ya magonjwa yaliyoathiri binadamu na pia mifugo.
Takriban visa 21,128 vya maradhi ya kuhara, kipindupindu, kuhara damu na malaria viliripotiwa miongoni mwa wakazi.
Mifugo 716 waliaga dunia na wengine 1,853 wakiathiriwa na maradhi mbalimbali ikiwemo kalaazar, ugonjwa wa miguu na mdomo, na ugonjwa wa ngozi.
Aidha, kondoo na mbuzi 4,115 waliangamizwa na mafuriko ya ghafla ambayo pia yaliharibu nyumba zaidi ya 40 katika maeneo ya Letea, Lokangae na Nanaam.
Ukame ulisababisha ukosefu wa malisho na maji jambo lililoathiri thamani ya mifugo na pia kusababisha uzalishaji maziwa kupungua kwa asilimia 50.
Ukosefu wa maji pamoja na uvamizi wa viwavi vya armyworms uliangamiza mimea kwa kiwango kikubwa.
“Bei ya lishe imekua ikipanda katika kaunti za ASAL tangu Machi. Kati ya Aprili na Julai, bei iliongezeka kwa kati ya asilimia 10-40,” NDMA ilisema katika ripoti yake.
Ripoti hii imejiri wakati serikali inajiandaa kununua mahindi kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya wakazi ambao hawana chakula.
Wakulima nchini wamekuwa wakilaumu serikali kwa kuwahujumu kwa kununua mahindi yao kwa bei ya chini na kununua nje kwa bei ya juu.