Itikadi ya kutohesabu watoto yatatiza sensa Narok
Na GEORGE SAYAGIE
ITIKADI ya jamii ya Wamaasai inayopiga marufuku kuhesabiwa kwa watoto na mifugo unaonekana kuwa kikwazo cha shughuli ya kuhesabu watu katika Kaunti ya Narok.
Tangu shughuli hiyo kung’oa nanga siku tano zilizopita, ni asilimia 37 pekee ya wakazi ambao wamehesabiwa.
Jamii ya Maasai inaamini kuwa kuhesabu watoto au mifugo kunaweza kuleta laana, maafa au majanga.
Wachungaji wa mifugo wamekuwa wakihama kutoka eneo moja hadi jingine kuepuka mifugo yao kuhesabiwa, hivyo kuwapa makarani wa sensa kibarua kigumu kutekeleza majukumu yao.
Kamishna wa Kaunti ya Narok, Samuel Kimiti jana alilazimika kufanya kikao na wasimamizi wa sensa kutoka wilaya zote za kaunti hiyo, ambapo walianzisha kampeni inayolenga kuwahimiza wakazi kujitokeza na kuhesabiwa kabla ya shughuli hiyo kufungwa kesho.
“Tunawaomba wakazi kujitokeza na kuhesabiwa. Ikiwa bado hujahesabiwa tafadhali nenda kwa chifu na makarani watakuja nyumbani kwako,“ Bw Kimiti akawaambia wakazi wakati wa kampeni hiyo.
Kulingana na Msimamizi wa Sensa katika Kaunti ya Narok, Bi Leah Wambugu, kaunti hiyo ina jumla ya makarani 2,700, wasimamizi 800 na wasimamizi wakuu 81.
Kupitwa na wakati
Gavana wa Narok Samuel Tunai aliwataka wakazi kutupilia mbali itikadi hiyo ya kuogopa kuhesabiwa akisema kuwa utamaduni huo umepitwa na wakati.
Gavana Tunai aliyekuwa akizungumza katika Hospitali ya Narok alipozindua shehena ya dawa za thamani ya Sh39 milioni zitakazosambazwa katika hospitali zote katika kaunti hiyo, alisema kuwa kuhesabu watoto na mifugo hakuleti laana kama inavyoaminika miongoni mwa wakazi.
“Nahimiza jamii ya Wamaasai kuruhusu serikali kuwahesabu. Utamaduni wa kutohesabu watoto na mifugo umepitwa na wakati,” akasema Gavana Tunai.
Bw Tunai alisema kuwa takwimu zitakazokusanywa na serikali ni muhimu katika ugawaji wa rasilimali kwa kaunti.