UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uchambuzi wa hadithi ‘Tumbo Lisiloshiba’ (Said A. Mohamed)
Na CHRIS ADUNGO
MWANDISHI wa hadithi hii analenga kuonyesha umuhimu wa umoja; kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Mzee Mago anajitahidi kuwahamasisha Wanamadongoporomoka waungane ili wapiganie haki ya kuishi katika eneo lao. Anaandaa mkutano na Bi Fambo, Bi Suruta na Kabwe kwa lengo la kuhimiza umoja. Hatimaye, vibanda vinaota tena kuliko mwanzo licha ya kubomolewa awali na askari wa Baraza la Mji wakilindwa na jeshi la polisi.
Mtunzi anapania kuonyesha jinsi viongozi dhalimu wanavyowanyanyasa wanyonge katika jamii. Wakubwa wanawafurusha Wanamadongoporomoka na kutwaa ardhi yao. Wanatumia mabuldoza kuangusha vibanda alfajiri changa kabla ya jua kuchomoza. Wakubwa wanabatilisha sheria kwa kuweka vitego na vikwazo ili wadogo wasitetee mali yao (sheria imo mikononi mwa wakubwa).
Jitu linakula chakula chote katika mkahawa wa Mzee Mago bila kuwajali wateja wengine; yaani Bi Fambo, Suruta na Kabwe.
Mwandishi anadhamiria kuakisi ukweli wa methali “Lisemwalo lipo na kama halipo li njiani laja”. Japo uvumi wa kutwaliwa kwa ardhi ya Madongoporomoka ulianza kwa minong’ono uliofifia; hatimaye uligeuka kuwa ukweli baada ya muda. Mtunzi anatoa tahadhari kuwa uvumi usiwahi kupuuzwa hata kidogo. Vibanda vya Wanamadongoporomoka vilibomolewa ila vikajengwa tena kutokana na juhudi za Mzee Mago.
Hadithi inaonyesha ukubwa wa tamaa na ubinafsi miongoni mwa viongozi (wakubwa). Jitu linakula chakula chote katika Mkahawa Mshenzi bila ya kuwajali wateja wengine. Wakubwa walimiliki majengo ya kila sampuli pamoja na hoteli, majumba makubwa ya kibiashara; yaani ‘malls’, maduka, na kadhalika.
Wanatumia vyombo vya dola hasa mahakama kuwafurusha wakazi ili wawe na majengo zaidi. Hawakutosheka kabisa na vile walivyokuwa navyo. Walitwaa ardhi ya wakazi wa Madongoporomoka na kubadilisha sheria ili kuyalinda maslahi yao. Ni adimu sana kuwapata wanasheria waaminifu kwa kuwa wengi wao wanaongozwa na tamaa na ubinafsi.
Matumizi mabaya ya vyombo vya dola ni suala jingine linaloangaziwa hadithini. Viongozi au wakubwa wanawatumia askari wa Baraza la Mji na jeshi la polisi kubomoa vibanda vya Wanamadongoporomoka badala ya kulinda maslahi yao. Mtunzi anasisitiza umuhimu wa kusimama kidete; yaani kuwa na msimamo imara na thabiti katika vita vya utetezi wa haki. Vitisho vya uvumi wa kubomolewa kwa vibanda havikuwatia Wanamadongoporomoka uoga wowote. Kwa ujasiri na umoja, walitetea ardhi yao vilivyo.
Kabwe anasema wenye fedha hawawezi kabisa kutwaa eneo lao na kushikilia kwamba watatumia umoja kwa vile ndio nguvu yao. Mwandishi anaonyesha kiwango kikubwa cha uozo miongoni mwa taasisi zinazowahudumia wanajamii. Ufisadi ulikithiri sana miongoni mwa wanasheria. Mzee Mago anasema kwamba ni nadra mno kuwapata wanasheria waaminifu katika jumuiya ya Madongoporomoka.
TAMAA NA UBINAFSI
Jitu linakula chakula chote bila kuwajali wateja wengine katika mkahawa wa Mzee Mago. Linakunywa vinywaji tofauti na kula vyakula anuwai kama vile wali kwa nazi, mchuzi wa nyama, nyama ya kuchoma, minofu ya kuku, chupa tano za soda ya Coca-Cola na kufuatisha duru zaidi maadamu lina uwezo wa kulipa. Wakubwa wana tamaa ya kumiliki majengo zaidi ya yaliyokuwamo jijini ndiposa walifurusha wakazi wa Madongoporomoka. Wanasheria wengi wana tamaa ya pesa na mali ndiposa wanaendeleza ufisadi katika taaluma yao.
UMOJA NA USHIRIKIANO
Mzee Mago anawashauri wakazi wa Madongoporomoka waungane ili wapiganie ardhi yao. Kabwe, Bi Fambo na Bi Suruta wanamuunga mkono na umoja huo unahakikisha kuwa vibanda vilivyobomolewa na askari wa Baraza la Mji chini ya ulinzi wa jeshi la polisi vimeota hata zaidi kuliko awali.
Wengi wape. Umoja wa wengi una nguvu wa kuondoa udhalimu na uovu unaoendelezwa na wakubwa. Sauti ya wengi ni nguvu imara ya kuangamiza mipango yote ya wakubwa! Mzee Mago aliwaweka pamoja wenzake na kunasihiana ili wakubali maendeleo katika nchi yao. Anasema kuwa maendeleo yanadai mchango wa kila mtu. Aliwashauri wakubali upya na usasa unaochangia mafanikio.
UTETEZI WA HAKI
Mzee Mago aliwahamasisha wenzake kupinga tukio la ardhi yao kutwaliwa na wakubwa wenye tamaa. Mzee Mago, Kabwe, Bi Suruta na Bi Fambo wanakutana katika Mkahawa Mshenzi ili watafute mbinu za kutetea ardhi yao isinyakuliwe na viongozi walafi wasiotambua wala kujali haki za wanyonge.
Mzee Mago anawatafuta wanasheria waaminifu ili watatue mazonge ya sheria ngumu katika harakati za kutetea haki zao dhidi ya dhuluma za wakubwa. Hatimaye Wanamadongoporomoka wanajenga upya vibanda vyao kuliko mwanzo baada ya kubomolewa na askari wa Baraza la Mji.
UTENGANO
Kuna utengano mkubwa kati ya wakubwa na wadogo. Wadogo hawahusishwi katika shauri la kufurushwa kutoka Madongoporomoka. Iwapo wangeshauriwa, wangeeleza vizuri zaidi kuhusu namna ya kuchangia maendeleo katika nchi yao.
Kuna utengano wa kiuchumi au wa mali kati ya walionavyo na wasionavyo. Wakubwa wanamiliki majengo mengi katika jiji kama vile ‘Departmental Stores’, hospitali na majumba makubwa ya kibiashara huku wadogo wakimiliki vibanda tu.
Kuna utengano kati ya wakazi wa Madongoporomoka na askari. Askari wa Baraza la Jiji wanafurusha na kubomoa vibanda vyao badala ya kulinda maslahi yao.
Kuna utengano wa kimazingira. Wakubwa wanaendelea kupanua jiji mahali palipo na majumba ya kifahari huku maskini (wadogo) wakifurushwa na vibanda vyao kubomolewa.
Upo pia utengano wa kitabaka. Matajiri wanamiliki magari ya kifahari na pia wana madereva. Jitu linalipia vyakula vya kila sampuli mkahawani. Walalahoi wanaishi katika vibanda huku wakishindwa hata kumudu gharama ya maisha. Mzee Mago ametengana na wenzake kifikira. Alipiga hatua ya kuwaelimisha wenzake ili watetee haki ya nchi yao.