• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 9:58 AM
FUNGUKA: ‘Sitaki hela zao, wakoleze utamu tu’

FUNGUKA: ‘Sitaki hela zao, wakoleze utamu tu’

Na PAULINE ONGAJI

MAREHEMU James Brown alisema kwamba ‘it’s a man’s world’ pengine kumaanisha kwamba kwa mambo mengi, madume wamejaliwa neema.

Na kwa kiwango fulani, kauli hii ina ukweli hasa katika masuala ya mapenzi ambapo ni rahisi kwa mwanamume kuwa na wake zaidi ya mmoja na kwa njia moja au nyingine kudumisha uelewano baina yao.

Lakini pia kuna wanawake ambao wametamalaki katika suala la kudumisha uhusiano wa kimapenzi na wanaume wawili au zaidi.

Maria ni mmoja wao. Hebu kwanza nikutambulishe kwake. Bibi huyu ana miaka 43. Marehemu babake alikuwa bwanyenye ambaye kabla ya kifo chake miaka minne iliyopita, alikuwa amekusanya mali kibao huku akiwekeza katika biashara mbalimbali katika sehemu tofauti nchini.

Alikuwa na nyumba kadha za kukodisha na pia alimiliki baa kadha jijini Nairobi.

Kwa hivyo alipofariki, alikuwa tayari amehakikisha kwamba wanawe wangeendelea kuishi maisha ya starehe pasipo matatizo ya kifedha.

Maria aliachiwa nyumba katika mojawapo ya mitaa ya kifahari jijini Nairobi, baa moja, vilevile ploti yenye nyumba kadha za kukodisha. Kwa hivyo kwa viwango vya kawaida ni salama kusema kwamba kimapato, binti huyu anaishi maisha yasiyo na bugdha ya kifedha.

Yeye ni mama wa binti mmoja ambaye anasomea katika mojawapo ya shule marufu za kimataifa.

Suala linaloibua utata hata hivyo ni maisha yake ya kimapenzi.

“Nachumbiwa na madume wawili ambao nawapenda sana, lakini cha kushangaza ni kwamba wanaume hawa wanajuana na kamwe siwafichi.

Mmoja wao ni baba ya binti yangu, na mwenzake ni rafiki ya huyu baba mtoto. Niliamua kurusha ndoano kwa rafikiye baada ya kugundua kwamba baba ya binti yangu alikuwa na uhusiano wa pembeni.

Lakini licha ya hayo, sikutaka uhusiano wetu uvunjike kwani atasalia kuwa baba ya mwanangu.

Rafikiye tayari ameshanitambulisha nyumbani kwao kama mke wa pili. Hii inamaanisha kwamba nimefungwa kimahusiano na wote wawili.

Kwa hivyo mimi huwaita kila wikendi kuja kwenye klabu yangu kuburudika kwa mvinyo ambapo sisi hupiga gumzo na kucheza densi pamoja.

Aidha, mimi huwaalika nyumbani ambapo wote wawili wana zamu tofauti ya kunihudumia kimahaba.

Kifedha najitegemea na hivyo wanasawazisha kwa kunisaidia katika majukumu ya uzazi. Kwa mfano, wameunda zamu ya kumpeleka mwanangu shuleni na kumrejesha nyumbani.

Na si kwamba huwa nawabembeleza, wana uhuru wa kuondoka endapo hawaridhiki lakini wanachelea kwa sababu wanajua kuna madume kibao waliopanga foleni kuchukua nafasi yao.

Kwa hivyo wote wanaelewa haya na hawana tatizo kuwa katika uhusiano nami, na hata kula na kunywa katika meza moja. Isitoshe, hii ni tabia ambayo wanaume wengi wamekuwa wakiifanya kwa miaka na mikaka, sembuse sisi kina dada?”

You can share this post!

TAHARIRI: Mashirika okoeni soka yetu isidorore

MWANAMUME KAMILI: Tatizo ni wanaojua ‘ukulima’ ila si...

adminleo