Makala

MWANAMUME KAMILI: Tatizo ni wanaojua ‘ukulima’ ila si upaliliaji na uvunaji zao

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DKT CHARLES OBENE

NATUMAI kwamba nyote mmekwisha kuwaona ama kuonana ana kwa ana na wangwana wanaojitahidi kuipa serikali idadi halisi ya watu “wanaotarajia huduma za serikali!”

Ndivyo, ni matumaini yangu kwamba kila mwanamume atajitahidi vilivyo kujibu maswali yanayoulizwa na Wakenya wakakamavu ambao haja yao hasa ni kujua “idadi ya wanawake wenye watoto wasiojua baba zao!”

Jibu alilotoa mzee mmoja alipoulizwa juu ya idadi ya wanawake kwenye himaya yake lilinikumbusha kazi nzuri ya wakulima wetu. Mzee yule alisema, “heri serikali ingejitahidi kujua idadi ya mapande ya ardhi anayomiliki ambayo hajayaatika mbegu wala kutia mbolea. Mapande yale yasiyolimwa ndiyo yanayokwamiza ukuaji wa uchumi nchini! Idadi ya wanawake ni shughuli ya mtu binafsi tena kwa makubaliano!” Hapo sasa! Waliocheka walicheka upeo wa kicheko. Lakini alikuwa na wazo nzuri mzee yule asiyekwisha hekima.

Hongera kwa kazi nzuri nyinyi mnaojua hekima ya ukulima bora! Yaweza kuwa ukulima “wa mashamba yanayosubiri mbegu na mbolea ya serikali” ama “mashamba binafsi tena yanayolimwa kwa makubaliano!” La muhimu ni kwamba kazi ya mwanamume kamili ni kujitahidi kivyovyote kuandaa shamba barabara, kuatika mbegu bora na kusubiri kuona miche ikichanachana ardhi na kuota! Kufanya hivyo ndivyo kudhihiri sifa nzuri ya mwanamume kamili.

Tatizo langu ni kwamba baadhi ya “wakulima wa mashamba” hawana subira ya ukulima bora!

Lau wangalijua ungwana wa kusubiri watoto kuzaliwa na kuwajibikia malezi yao labda serikali isingalikuwa na haja ya kukadiria idadi ya watoto wanaotaka huduma ila baba zao walikwisha tokomea nyikani! Serikali isingalikuwa na haja ya kujua idadi ya wanawake wanaosubiri kuzalishwa ila hawana kazi wala bazi. Ya nini kuzaa kama hamna haja kulea?

Hekima ya maisha ni kwamba mja hujizatiti kujizoazoa angalau kushikamana ashikwapo! Vipi mtatarajia serikali kuwabeba mgongoni ilhali mmelegea na kulegeza viungo kama vinyago vya watoto wa chekechea? Hebu wajibikeni kuipa serikali kazi rahisi kukadiria idadi ya wanawake na watoto walioachwa na kumbukizi viganjani. Elezeni bayana idadi ya wake zenu. Hivyo ndivyo afanyavyo mwanamume kamili.

Tatizo kubwa linalosibu jamii ni ujaji wa wanaume hadaa wanaojua “ukulima” ila upaliliaji na uvunaji wa mazao ya ukulima bora! Wanajua kupanda katika mashamba huru ila hawataki kusubiri miche kuota na kuinyunyuzia maji ya maisha.

Iweje mwanamume kujitahidi kiume kumpa mke himila kisha kumwacha kana kwamba hajafanya kitu?

Hizi tabia za wanaume kujihusisha kimahaba na wanawake bila nia njema inahuzunisha mno! Wala sitaki kujua mchango wa wanawake katika hizi himila za pata potea!

Sina muda wa kuchana ncha za nywele! Watoto ni shughuli, tena kazi ya mwanamume. Hekima nyingine mtaipeleka kilingeni.

Sisemi kwamba “makubaliano binafsi ya wakulima” sharti kudumu milele. Hayo ni yenu wenye mashamba yanayolimwa kwa makubaliano! Lakini watoto wasijeachwa wakiteseka na kula jalalani eti kwa sababu mahaba yalikwisha tamatika! Mahaba ni raha ya watu wazima wenye ridhaa. Walikosani watoto wanaoachwa wakitapatapa kama makinda yaliyoangukiwa tawi na kiota? Heri mwanamume kulala chini na kula jalalani lakini wanawe waishi kama kifalme ama kimalkia! Huo ndio uume! Mengineyo ni ugumegume tu.

Kina babu, baba na kaka zetu wa leo ndio kwanza wajuvi wa mambo ya mashamba! Wanajua kupenda – kama upanzi wa mbegu ni mapenzi – ila kuvuna na kulea kwa heshima ni kazi kwao. Wanajua kushawishi hali na kuziteka hisia za wanawake ila kustawisha maisha na kuwapa watoto matumaini ni kazi ya sulubu.

Jamii inahitaji wanaume farisi wanaopanda na kuvuna haki yao. Lakini tuwapate wapi katika tambara hili bovu liitwalo dunia? Afadhali tuhesabiwe tujue ukweli angalau tulipe kodi kuwafaidi watoto walioachwa na gumegume wanaume wa leo. Hayo ndiyo mawazo ya mwanamume kamili.

 

[email protected]