• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
UMBEA: Sifa ya mwanamke sio kauli kali au ubabe, ni kubembeleza

UMBEA: Sifa ya mwanamke sio kauli kali au ubabe, ni kubembeleza

Na SIZARINA HAMISI

PAMOJA na kwamba mdomo ni mali yako na tena hulipii kodi, mdomo huu, huponza wengi.

Wapo akina dada ambao hutumia midomo, na kutapika maneno ambayo huwakimbiza waume ama wapenzi wao.

Wengine pia hutumia kauli tata kujaribu kuwadhibiti na kuwatawala waume zao.

Huwa inakuwa hivi, mwanaume hupenda kutawala ama kuhisi anatawala. Pale anapoona ama anapohisi anatawaliwa na mwanamke, hata akiacha kusema, hujikuta akianza kujihisi vibaya kuhusu nafsi yake na hatimaye kuhusu huyu mwanamke anayehisi anamtawala.

Katika uhusiano, baadhi ya akina dada hukosea kwa kuamini, ukali ama kuwa na maneno mengi ya kuudhi ni njia nzuri ya kupambana na wanaume zao katika yale mambo wanayotaka kudhibiti.

Kitu wanachosahau ni kwamba wanaume huchukia kufokewa, kufanywa bongo lala na kuhisi wanatawaliwa na wanawake.

Na kwa mwanamke mwenye tabia za kufoka kwa mume ama mpenzi wake, tabia ya kujihisi anamtawala mume wake, ajue sio tu kwamba anamtesa mume wake kifikra ila pia anatengeneza mazingira ya huyu mwanaume kuachana naye, kuwa na mwanamke wa pembeni ama kupenda kukaa mbali naye.

Wapo akina kaka ambao wakiwa kazini wanakuwa huru na amani zaidi kuliko wakiwa na wake zao. Pia wako wanaume wengi msisimko wa kihisia na wapenzi wao umeisha ama umepungua kwa asilimia kubwa kwa sababu ya kauli na tabia za ubabe walizonazo wanawake wao.

Iwapo wewe ni mwanamke, ama dada uliye katika uhusiano ama ndoa, ujue kwamba silaha ya mwanamke si kauli kali wala ubabe. Umejaliwa ngozi laini, sauti nzuri na uwezo mkubwa wa kushawishi hisia za mwanaume, bila ya kuweka sauti ya kazi, ama maneno makali.

Vitu hivi mwanamke anapaswa kuvitumia vyema ili kumfanya mume wake abadilike na si kujifanya mjuaji karibu kwa kila kitu.

Hakuna mwanamke aliyeshinda katika vita ya kutunishiana misuli na mume wake. Mwanamke hajaumbwa hivyo.

Sifa ya mwanamke ni kudeka, kumfanya mwanaume ajihisi mwenye hatia kwa sauti ama matendo yake.

Ukileta ujuaji kwa mwanaume,si tu unashindwa kufanikiwa katika lengo lako, pia unamfanya naye awe juu zaidi na kusababisha mahusiano kuwa na mawimbi makubwa ya kutokuelewana.

Huna budi kufahamu kwamba unaweza kubadili tabia na misimamo ya mumeo kwa matendo yako ya kike sio kuiga tabia za kiume.

Mwanaume anapofokewa na mwanamke mambo mawili huja akilini mwake haraka. Kwanza atafikiri mwanamke husika anamfanya juha. Pili atafikiri kutafuta sehemu nyingine apate utulivu na amani.

Ijulikane pia kwamba mwanamke anapokuwa na tabia zinazomkwaza sana mwenzake, ni sababu pia hata kiwango cha muhusika kujali na kuheshimu hupungua kama si kuisha kabisa.

Mwanamke si mwanamke kwa jinsia tu

Mwanamume anapokuwa na mwanamke, hutegemea mwanamke huyo kuonyesha uanamke wake katika tabia kauli na maamuzi yake.

Sio anakuwa mwanamke kwa jinsia huku matendo na tabia zinakuwa za kiume. Sifa ya mwanamke ni kubembeleza na kunyenyekea.

Mwanamke anapokosewa, harushi maneno makali kwa mumewe ila hutenda ama husema mambo ambayo yatamfanya mwanaume husika ajihisi mkosaji.

Ukileta ubabe kwa mwanaume, usishangae mwenzako akataka kukuonyesha yeye ni nani.

Hapa ndipo atachepuka nje ama akupige matukio mfululizo ubaki unajiuliza umekosea wapi.

Kauli na maneno ya kuudhi sio sifa ya mwanamke. Tathmini zinaonyesha wanawake wengi wakorofi hawadumu katika mahusiano na wachache wenye kudumu huwa hawako katika mahusiani yenye raha na furaha.

Kila binadamu anahitaji faraja. Nazo faraja hizo hutoka kwa watu tunaowapenda na kuwajali. Badilika, chukua hatua.

 

[email protected]

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Utunishaji misuli wampa tonge la siku

FATAKI: Mume au watoto wasiwe minyororo maishani!

adminleo