Mswada ‘Punguza Mizigo' waelekea kugonga ukuta
Na WANDERI KAMAU, BENSON MATHEKA na COLLINS OMULO
MSWADA wa kura ya maamuzi wa Punguza Mizigo unaopigiwa debe na Dkt Ekuru Aukot wa chama cha Thirdway Alliance unaelekea kugonga mwamba kutokana na pingamizi nyingi ambazo umepata kutoka kwa wanasiasa, mabunge ya kaunti na Bunge la Kitaifa huku magavana wakipanga kuzindua kampeni yao.
Tayari, mswada huo umepata pingamizi kubwa katika mabunge ya kaunti za Nyeri na Siaya, madiwani wakiukosoa kwa kutozingatia maslahi yao.
Wadadisi wanasema itakuwa vigumu kwa mabunge ya kaunti kutoka ngome za Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitisha mswada huo.
Wawili hao wamekuwa wakipigia debe ripoti ya kamati ya uwiano waliyoteua ambayo wanaamini itatatua matatizo ya Wakenya kupitia refarenda.
Tayari Bw Odinga ameagiza madiwani katika kaunti zote kuukataa.
Vilevile imeibuka kuwa wabunge wanapanga mikakati ya kuuangusha, kwa kuchelewesha kupitishwa kwake kimakusudi, ikiwa utapitishwa na angaa mabunge 24, kama inavyohitajika kikatiba.
Mswada huo unapendekeza kupunguzwa kwa idadi ya wabunge kutoka 416 hadi 147.
Duru zinaeleza kuwa wabunge wanapanga kutumia Kipengele 257 cha Katiba, ambacho hakijafafanua wazi kuhusu muda ambao Bunge la Kitaifa linapaswa kuchukua ili kujadili mswada unaopendekeza mageuzi ya katiba.
Wabunge kadhaa tuliozungumza nao walisema kuwa huenda wakatumia mwanya huo wa kisheria kuukataa mswada huo.
Wabunge wanasema kuwa hatua hiyo pia inachangiwa na mpango wa kuhakikisha kuwa mapendekezo ya BBI yatapitishwa.
Bw Odinga amewaeleza wafuasi wake kuukataa mswada huo, kwa msingi kuwa hauwakilishi maoni ya Wakenya.
BBI
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee (JP) Bw Raphael Tuju amesema kuwa chama hicho kinaunga mkono mapendekezo yatakayotolewa na BBI, ambalo sasa inaandaa ripoti ya mwisho baada ya kukusanya maoni ya Wakenya katika kaunti zote 47.
Wakili Bobby Mkangi, ambaye ni mtaalamu wa kikatiba, anakubali kwamba Bunge linaweza kutumia pengo hilo kuzuia mswada huo kuendelea.
“Italingana na taratibu ambazo Bunge la Kitaifa litazingatia. Wanaweza wakauchelewesha kimakusudi, ikiwa hakutakuwa na shinikizo zozote za kisiasa dhidi yao kuupitisha,” akasema Bw Mkangi.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale alisema kuwa mswada huo hautapita hatua yoyote baada ya kujadiliwa na mabunge ya kaunti.
“Nasema kuwa mswada huo hautaelekea pahali popote. Huwezi kupunguza idadi ya maeneobunge bila kutoa sababu halisi,” akasema Bw Duale.
Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi vilevile alieleza kuwa Bunge la Kitaifa linaweza kuamua kuuchelewesha mswada huo, hadi wakati wake wa kuhudumu utakapoisha.
“Mswada huo hauna umaarufu wowote miongoni mwa wabunge na maseneta. Tunaweza kuamua kutofanya lolote kuhusiana nao na kuuchelewsha tuwezavyo,” akasema.
Wakati huo huo, magavana wanatarajiwa kuzindua harakati za kushininiza mageuzi ya katiba kwa muda wa wiki moja.