MWANASIASA NGANGARI: Kiano: msomi aliyetetea wafanyabiashara nchini
Na KENYA YEAR BOOK
DKT Julius Gikonyo Kiano alikuwa msomi na shujaa wa kupigania uhuru.
Yeye ndiye Mkenya wa kwanza kupata shahada ya uzamifu (PhD).
Alizaliwa mnamo 1926 katika eneo la Githiga, eneobunge la Kangema, Kaunti ya Murang’a, wakati huo ikiwa wilaya.
Alisomea katika Shule ya Msingi ya Weithaga na Shule ya Upili ya Kagumo, ambapo baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance kwa elimu yake ya kiwango cha juu.
Baada ya hapo, alienda katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda alikoongeza masomo yake. Katika kile kilichoonekana kuwa kiu kubwa ya masomo, alielekea katika Chuo cha Antioch, Ohio, nchini Amerika alikosomea shahada kuhusu masuala ya uchumi ambapo alimaliza mnamo 1952.
Akiwa chuoni humo, alianza kuvutiwa na mfumo wa vyama vya ushirika, ambavyo baadaye vilichangia sana katika ukuaji wa kilimo na sekta zingine muhimu baada ya Kenya kujinyakulia uhuru.
Kabla ya kuondoka nchini kuelekea Amerika, Kiano alikuwa na ufahamu mkubwa wa hali ilivyokuwa nchini (ukoloni); ambayo ilihitaji Wakenya waliosoma na wale ambao hawakuwa wamesoma kuungana kwenye vita vya ukombozi.
Alipomaliza masomo yake, alipata ufadhili mwingine wa kimasomo kufanya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Stanford kusomea sayansi ya siasa mnamo 1953.
Alikuwa amepata mshawasha mkubwa wa kushiriki kwenye harakati za kuikomboa Kenya kutoka kwa minyororo ya ukoloni kutoka kwa wanajeshi wa Kiafrika ambao walikuwa wakirudi nyumbani kutoka Vita vya Pili vya Dunia mnamo 1945. Wakati huo alikuwa katika shule ya upili.
Kiano, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa waziri wa kwanza wa Biashara na Viwanda, alielekea katika Taasisi ya Mafunzo ya Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, Amerika kusomea shahada ya uzamifu.
Shahada hiyo ilijikita katika masuala ya ukoloni na harakati za ukombozi katika mabara Afrika na Asia.
Akiwa chuoni humo, alishirikiana na wasomi wengine waliokuwa wamebobea katika masuala hayo.
Kwenye mahojiano mnamo 1996 alisema: “Uamuzi wangu kurudi chuoni kusomea masuala ya ukombozi ulichangiwa na masuala mengi. Niliona jinsi harakati za ukombozi zilichangia nchi kama India na Indonesia kupata uhuru. Niliona kuwa hiyo ndiyo njia pekee ingeharakisha ukombozi wa Waafrika kutoka kwa wakoloni.
“Mnamo 1951, Kwameh Nkrumah aliibuka kuwa kiongozi wa serikali nchini Ghana. Baadaye Ghana ikawa nchi ya kwanza ya Afrika kupata uhuru mnamo 1957. Nilioanisha masomo yangu na uanaharakati kama huo,” akaongeza.
Dkt Kiano alirejea nchini mnamo 1956 baada ya kukaa nchini Amerika kwa miaka minane. Alipata kazi kama mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, wakati huo kikijulikana kama The Royal Technical College. Alifunza masuala ya uchumi na sheria ya kikatiba.
Baadaye, aliacha kazi ya uhadhiri na kujitosa katika siasa. Alichaguliwa kuwakilisha ukanda wa Kusini wa Mkoa wa Kati mnamo 1958 katika Bunge (Legco).
Kiano na viongozi wengine kama Tom Mboya walifahamu kwamba walihitaji watu wengi wenye uwezo na waliosoma ili kuishinikiza serikali ya kikoloni kuipa Kenya uhuru wake.
Kutokana na hayo, waliwaandikia barua marafiki wao katika vyuo vikuu nchini Amerika kuwatafutia nafasi Wakenya kwenda kusomea huko. Mpango wao ulipokelewa vizuri kwani mamia ya wanafunzi Wakenya walipata mialiko na ufadhili wa kimasomo kusomea katika vyuo hivyo.
Viongozi hao wawili watakumbukwa sana kwa kuchangia Wakenya wengi kupata nafasi ya kusomea katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Amerika, kwenye mpango ulioitwa ‘Great Airlift’.
Kiano alimwoa mwanamke Mwamerika, aliyeitwa Ernestine lakini wakaachana. Baadaye, alimwoa Bi Jane Wanja ambaye alifahamika na wengi. Baadhi ya nyadhifa ambazo Bi Kiano alihudumu ni mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake (MYWO) na Baraza la Kitaifa la Wanawake Kenya (NCWK). Vilevile, alihudumu kama mwanachama wa Tume Maalum wa Jiji la Nairobi. Alifariki Oktoba 2018 akiwa na umri wa miaka 74.
Mnamo Desemba 1961, Dkt Kiano aliilaumu serikali ya kikoloni dhidi ya kuendesha jumba la mateso, ambalo lilitumiwa kuwahoji watu waliokuwa wamekamatwa na kufungiwa gerezani bila kufunguliwa mashtaka.
Mnamo 1963, aliteuliwa kama Waziri wa Biashara na Viwanda, baada ya kuchaguliwa kama mbunge wa Kangema. Hatua yake ya kwanza kama waziri ilikuwa ni kuwalaumu wafanyabiashara wenye asili ya Kihindi kwa kuwauzia Waafrika bidhaa mbalimbali kwa bei ya juu kinyume gharama yazo halisi.
“Unamwambia mteja kwamba gharama ya bidhaa ni Sh20 ilhali bei yake ni Sh5 pekee,” akasema.
Chini ya usimamizi wake, wizara hiyo ilianza mpango wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogowadogo wa Kiafrika kununua bidhaa za kuuza kwa bei ya chini. Mpango huo ulipitishwa na baraza la mawaziri.
Kabla ya hapo, wafanyabiashara hao walikuwa wakiuziwa bidhaa hizo kutoka kwa Wahindi kwa bei ya juu, kiasi kwamba hawangeweza kushindana nao kibiashara.
Katika juhudi za kuwashajiisha Wakenya kujiingiza katika biashara, alisafiri maeneo mbalimbali nchini akifungua maduka ya Kiafrika na biashara.
Mnamo 1964, kwenye Kongamano Maalum la Mawaziri wa nchi wanchama wa Jumuiya ya Madola, aliomba kubuniwa kwa shirika la kimataifa ambalo lingejikita katika masuala ya maendeleo na biashara chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa (UN).
Alitarajia kwamba shirika hilo lingekuwa na majukumu kama ya Shirika la Kilimo na Vyakula Duniani (FAO), Shirika la Kimataifa kuhusu Leba (ILO) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Baadaye, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) lenye makao yake jijini Geneva, Uswisi lilibuniwa mnamo 1976, ambapo alichaguliwa kama mkurugenzi wake mkuu wa kwanza.
Baadhi ya wizara zingine ambazo Bw Kiano alihudumu ni Elimu na Serikali za Mitaa. Baadaye katika miaka ya sabini, alirudishwa tena katika Wizara ya Biashara na Viwanda. Baada ya muda mfupi, alihamishiwa katika Wizara ya Maji. Kutokana na kubadilishwa kila mara, alibandikwa jina la waziri aliyehamishwa sana na Mzee Jomo Kenyatta
Mnamo 1975, Dkt Kiano aliagiza kufungwa kwa maduka 58, likiwemo duka la jumla la Nairobi Supermarket kwa tuhuma za kuingiza bidhaa mbalimbali kutoka nje bila kibali. Wafanyabiashara 11 walikamatwa kwa kuficha sukari.
Mnamo 1976, alipoteza nafasi yake kama mwenyekiti wa chama cha Kanu katika tawi la Mbiri.
Mnamo 1979, alishindwa kwenye uchaguzi wa ubunge wa eneo hilo na Bw Stanley Matiba, aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni ya kutengeneza vileo ya Kenya Breweries (KBL).
Aliwasilisha kesi mahakamani mnamo 1980 lakini hakufaulu.
Mnamo 1988, Bw Matiba, ambaye alikuwa ashateuliwa kuwa waziri, alijiuzulu nyadhifa hizo mbili kwa madai kwamba aliibiwa kura kwenye uchaguzi wa uenyekiti wa chama hicho katika eneobunge hilo. Eneo hilo lilibadilishwa jina kutoka Mbiri na kuitwa Kiharu (kama linavyojulikana hadi sasa).
Jaribio lake la kutwaa upya ubunge katika eneo hilo hazikufaulu baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mdogo wa 1989.
Rais Mstaafu Daniel Moi alimteua kuwa mwenyekiti wa Shirika la Utangzaji la Kenya (KBC), nafasi aliyohudumu hadi mwaka 2003, alipofariki kutokana na mshtuko wa moyo.
Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke