Habari Mseto

Kenya itaanza kuonja faida ya mafuta baada ya miaka minane

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na ANTHONY KITIMO

KENYA inatarajiwa kuonja faida ya mapato ya mafuta ambayo ilianza kuuza nje ya nchi baada ya miaka minane kwa sababu ya madeni inayopaswa kulipa kwanza.

Hii inamaanisha kuwa faida ya kwanza inatarajiwa 2027.

Na kabla ya kuanza kunufaika, kampuni ya Tullow Oil ambayo inachimba mafuta hayo itajilipa zaidi ya Sh210 bilioni ambazo itatumia kujenga bomba la kusafirisha mafuta la urefu wa kilomita 890 kutoka Lokichar, Kaunti ya Turkana hadi Lamu.

Aidha, kuna gharama nyingine za zaidi ya Sh300 bilioni ambazo zinafaa kulipwa kwanza kabla ya Kenya kufurahia mapato ya mafuta.

Wiki jana, Rais Kenyatta alizindua uuzaji wa mafuta nje ya nchi meli iliyobeba mafuta ya kima cha Sh1.2 bilioni ilipoondoka bandari ya Mombasa kuelekea Malaysia.

Wakati wa hafla hiyo kampuni ya Tullow Oil ilisema kwamba mafuta ya Kenya yataanza kuuzwa kikamilifu 2022.

“Bandari ya Lamu itakapokamilika na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Lokichar-Lamu pia, itakuwa rahisi kutekeleza shughuli zetu na kuuza mafuta nje ya nchi,” kampuni hiyo ilisema.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), John Lonyangapuo (Pokot Magharibi) na Naibu Gavana wa Turkana Peter Lotethiro, waliomba serikali itekeleze sheria ya mafuta ikifafanua jinsi mapato yatagawanywa.

Historia imeonyesha kuwa jamii zinazoishi maeneo ambayo yana rasilmali muhimu hukubwa na umasikini mkubwa kwa sababu hazinufaiki.

Mafuta yaliyouzwa Malaysia yalikuwa ya kujaribu kuona jinsi mafuta ya Kenya yatapokelewa katika soko la kimataifa.