MWANAMKE MWELEDI: Ajizolea heshima tele kupigania lishe bora
Na KEYB
ALIKUWA profesa wa kwanza katika masuala ya lishe nchini na wa kwanza wa kike katika mataifa yaliyo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ni suala lililomfanya Profesa Ruth Khasaya Oniang’o kutambuliwa kwa kuchangia katika fani ya lishe ya jamii.
Ustadi wake katika masuala haya ulimzolea heshima kiasi cha kutambuliwa katika majukwaa mbalimbali.
Kama mtaalamu mwasisi wa kike wa lishe nchini, Prof Oniang’o amepokea tuzo kibao nyumbani na kimataifa.
Kwa mfano, aliwahi kupokea tuzo ya Silver Star Medal na Distinguished Service Medal.
Aidha, shirika aliloanzisha la Rural Outreach Africa-ROA limewahi kupokea hati ya utambuzi kutoka kwa serikali ya Kenya na pia shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO).
Aidha, ufanisi huu umemzolea heshima na kumfanya kupewa fursa ya kusimamia majukwaa tofauti. Kwa mfano, kati ya mwaka wa 2013 na 2015, alihudumu kama naibu mwenyekiti wa Global Forum for Agricultural Research (GFAR) ambapo jukumu lake hasa lilihusisha jinsia na lishe katika sekta ya kilimo.
Prof Oniang’o alijifunza maadili ya nidhamu na ubora wa elimu kutoka kwa wazazi wake, suala lililomfanya kujishindia fursa nyingi za ufadhili wa kimasomo Amerika, na ni hapa ndipo safari yake ya kuwa profesa wa kwanza katika masuala ya lishe nchini ilianza.
Penzi lake katika lishe lilianza mapema maishani. Akiwa mdogo, alishuhudia binamuye akishindwa kutembea kutokana na kuugua maradhi ya kwashiorkor, bali na kushambuliwa na minyoo.
“Nilijiuliza ni kwa nini tumbo lake lilikuwa likizidi kunenepa na kwa nini ni yeye pekee aliyekumbwa na maradhi haya, ilhali watoto wengine walionekana wenye afya nzuri?” akumbuka.
Aidha, penzi hili lilikolezwa hata zaidi alipowapoteza sita kati ya nduguze 11 katika umri mchanga.
“Walikuwa wakikumbwa na mtukutiko wa maungo kisha kufa kutokana na hali ambayo baadaye niligundua kwamba ilikuwa aina ya maradhi ya malaria ambayo yalikumba jamaa zangu kutoka upande wa baba. Nilishuhudia mama akiteseka na hivyo nikaahidi kwamba nitazaa watoto 20 ili wachukue nafasi iliyoachwa na watoto aliowapoteza,” aeleza.
Badala yake hata hivyo, matukio haya yalichochea kiu yake ya kutaka kuimarisha afya kupitia lishe.
Baada ya kukamilisha masomo, Profesa Oniang’o alirejea nyumbani kuhudumia taifa lake, kulingana na maagano ya udhamini. Alihudumu kama mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), huku pia akijisajili kusomea shahada ya uzamifu katika masuala ya chakula na lishe.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta baada ya kuhitimu, na kisha baadaye akahamia Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).
Katika utafiti wa shahada yake ya uzamifu, alizuru maeneo mengi nchini, suala liilomchochea kuanzisha shirika la Rural Outreach Program, kumarisha jamii kupitia miradi ya kilimo na ujasiriamali.
“Nilitembelea sehemu nyingi nchini lakini eneo la Embu ndilo lililonivutia zaidi. Nilikutana na wakulima waliokuwa ana vipande vidogo vya ardhi, ilhali walikuwa wamejenga nyumba za mawe, vile vile walikuwa wameelimisha wanao, kununua magari na hata kujenga mabomba ya kusambaza maji nyumbani, huku rikizi yao ikitokana na upanzi wa matunda ya pesheni na ufugaji ng’ombe,” aongeza.
Hii ilikuwa kinyume na wakulima kutoka sehemu zingine nchini waliokuwa na vipande vikubwa vya ardhi, ilhali mbinu mbovu za ukulima ziliwanyima riziki.
Baada ya kukamilisha shahada yake ya uzamifu mwaka wa 1983, alianza kutafuta ufadhili wa kuanzisha shirika lake na likang’oa nanga rasmi 1992 ambapo baadaye lilibadilishwa jina na kuwa Rural Outreach Africa (ROA).
Shirika hili limekita kambi hasa mashinani katika kusaidia watu kujitafutia riziki kupitia kilimo kama mbinu ya kukabiliana na umaskini. Aidha lilipanua huduma zake na kuangazia pia elimu na afya ya kiakili.
Ili kushughulikia shirika hili zaidi, Prof Oniang’o alichukua likizo kutoka nafasi yake kama profesa wa masuala ya chakula na lishe na mkurugenzi mwanzilishi wa kozi hii katika chuo kikuu cha JKUAT.
Mbali na masuala ya elimu na shirika lake, Prof Oniang’o pia alijaribu bahati yake katika fani ya siasa. Mwaka wa 2002, aliteuliwa kama mbunge. Akiwa mbunge, alihudumu kama waziri hewa wa elimu ambapo pia alikuwa naibu mwenyekiti katika muungano wa wabunge wanawake.
Aidha, alijumuisha kikosi kilichoshughulikia mswada wa makosa ya dhuluma za kimapenzi na hata kupigania mswada wa usalama wa kimazingira, vile vile ule wa wataalamu wa masuala ya lishe.
Akihudumu kama waziri hewa, Prof Oniang’o alikuwa mwanachama wa kikosi kilichotupilia mbali deni za karo za wanafunzi waliokamilisha kidato cha nne na kuamuru shule ziwape hati zao. “Hii ilikuwa mojawapo ya maafikio makuu na yenye fahari kwangu nikiwa bungeni,” asema.
Lakini Prof oniang’o hakudumu kwenye siasa kwa muda mrefu, huku uamuzi wake wa kugura ukitokana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.
Kwa sasa, Prof Oniang’o anazidi kujihusisha na miradi ya kuimarisha maisha ya jamii kupitia kilimo.
Lakini ufanisi huu haukukosa changamoto. Alikumbana na ubaguzi wa kijinsia ambapo ililazimu kutetea nafasi yake hadi akaidhinishwa kama profesa kamili katika JKUAT.
Anawashauri wanawake kutopoteza matumiani wala kulegeza maadili yao, na badala yake kutia bidii na kuitisha wanachostahili bila woga.