Michezo

Shujaa watawazwa washindi wa Victoria Falls Sevens Zimbabwe

March 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

SHUJAA ya Kenya imeibuka mshindi wa makala ya pili ya raga za wachezaji saba kila upande za Victoria Falls Sevens nchini Zimbabwe, Jumapili.

Kenya ilivuna taji kwa kuzaba wenyeji na mabingwa watetezi Zambezi Cheetahs 10-5 katika fainali ngumu mjini Victoria Falls.

Ushindi huu muhimu ulipatikana kupitia miguso ya wachezaji wapya kikosini Levy Amunga na Brian Wahinya katika kipindi cha kwanza.

Ingawa Zimbabwe ilianza kipindi cha pili kwa kishindo kwa kupachika mguso kupitia Rian O’Neill, ufufuo wake ulizimwa na ulinzi imara kutoka kwa Shujaa.

Kenya, ambayo haikusafiri na kocha mkuu Innocent Simiyu, ililemea mabingwa wa Afrika Uganda 17-10 katika nusu-fainali. Ilihitaji mguso katika sekunde ya mwisho kutoka kwa Samuel Ng’ethe kuingia fainali.

Shujaa, ambayo ilishinda taji la Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015, iliongoza 10-0 wakati wa mapumziko.

Hata hivyo, Uganda ya kocha Mkenya Tolbert Onyango, ambayo ni bingwa wa Afrika mwaka 2016 na 2017, iliziba mwanya huo kupitia mguso miwili bila mikwaju kutoka kwa Solomon Okia 10-10 kabla ya Ng’ethe kupata mguso wa ushindi na mkwaju wake.

Katika mechi ya robo-fainali, Kenya ilibwaga Spartans ya Botswana 43-0 kupitia miguso ya Mark Kwemoi, Frank Wanyama, Bush Mwale, Derrick Mayar, Augustine Lugonzo na Ian Minjire.

Shujaa ilikuwa alama 19-0 juu wakati wa mapumziko kupitia miguso ya Kwemoi na Wanyama kabla ya Mwale, Mayar, Lugonzo na Minjire kuongeza alama zaidi katika kipindi cha pili.

Kenya ilifuzu kushiriki robo-fainali baada ya kupepeta False Bay (Afrika Kusini) 17-0, Zambia B 31-0, Lesotho 26-0 na Zambezi Cheetahs ya Zimbabwe 14-12 katika mechi za makundi Jumamosi.

Shujaa, Uganda na Zimbabwe zilitumia Victoria Falls Sevens kujiandaa kwa mashindano ya dunia ya Hong Kong Sevens yatakayofanyika Aprili 6-8. Kenya inashiriki Raga za Dunia msimu 2017-2018 nazo Zimbabwe na Uganda zitakuwa zikipigania tiketi ya kuingia Raga za Dunia msimu 2018-2019.

Timu za Kenya, Uganda na Zambia pia zinajitayarisha kwa mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Aprili 13-15 nchini Australia.

Matokeo (Machi 25)

Fainali

Kenya 10-5 Zambezi Cheetahs (Zimbabwe)

Nusu-fainali

Shujaa (Kenya) 17-10 Uganda

Zambezi Cheetahs (Zimbabwe) 19-0 Zambia A

Robo-fainali

Shujaa (Kenya) 43-0 Spartans (Botswana), Zambezi Cheetahs (Zimbabwe) 31-0 Zambezi Steelers (Zimbabwe), False Bay (Afrika Kusini) 14-19 Uganda; Spartans (Botswana) 14-33 False Bay (Afrika Kusini), Goshawks (Zimbabwe) 21-17 Zambezi Steelers (Zimbabwe). Mechi ya kuorodhesha nambari tisa na 10 – Zambia B 28-7 Lesotho.