• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
DINI: Neno ‘Ahsante’ huashiria unyenyekevu, au sala inayomfanya mtoaji atoe zaidi

DINI: Neno ‘Ahsante’ huashiria unyenyekevu, au sala inayomfanya mtoaji atoe zaidi

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Shukrani ni mtihani. Kwa mtazamo wangu, shukrani ni utajiri, kutoshukuru ni umaskini. Shukrani ni furaha, kutoshukuru ni huzuni. Shukrani ni fadhila, kutoshukuru ni ulemavu.

Shukrani ni chanya, kutoshukuru ni hasi. Shukrani ni kicheko, kutoshukuru ni kilio. Shukrani ni ongezeko, kutoshukuru ni upungufu. Shukrani ni nguvu, kutoshukuru ni udhaifu. Shukrani ni kujipenda, kutoshukuru ni kujipendelea. Shukrani ni tabia njema, kutoshukuru ni tabia mbaya.

Mtunga Zaburi anasema, “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele” (Zaburi 106:1). “Hakuna kinachogusa moyo wa Mungu kama shukrani kwa ajili ya mema yake,” (Vincent de Paul).

Kushukuru ni kuomba tena. “Shukuru kwa ulivyonavyo; utaishia kuwa na zaidi. Ukifikiria ambavyo hauna, havitatosha kamwe,” alisema Oprah Winfrey.

Ulivyo navyo usivichukulie poa, vichukue kwa shukrani. “Ni mtu mwenye hekima ambaye halilii vitu ambavyo hana bali anafurahia vitu alivyonavyo,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki Epictetus.

Ni katika mtazamo huo Max Lucado alilinganisha kutoshukuru na dhambi ya asili. “Naamini kutoshukuru ni dhambi ya asili. Naamini kama Adamu na Eva wangekuwa ni watu wa shukrani kwa Bustani ya Eden waliyokuwa nayo wasingeweka mawazo yao kwenye mti mmoja ambao hawakuwa nao.”

Kutoshukuru ni kulipa jema kwa baya. “Mtu hapaswi kutupa jiwe kwenye chanzo cha maji alichowahi kutumia” (Talmud). Kutoshukuru ni uchoyo uliopindukia. Kutoshukuru ni kuwa mchoyo wa fadhila. Kutoshukuru kunaua mtunzi wake muda mfupi au baadaye (Methali ya Ivory Coast).

Kutoshukuru ni wizi wa furaha. “Huwezi kumuona mtu mwenye furaha ambaye hana shukrani (Zig Ziglar). Ingawa Honore de Balzac alisema, “Kutokuwa na shukrani labda hutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa,” uwezo wa kushukuru tunao. Uwezo wa kusema “Asante Sana,” tunao. Unapokunywa shukuru chanzo cha kinywaji hicho (Methali ya Kichina).

Maneno “Asante Sana” “yanaroga” mtoaji atoe zaidi. “Maneno nakushukuru ni sala nzuri sana ambayo mtu yeyote anaweza kusali. Naisali sala hiyo mara nyingi. Maneno nakushukuru yanabainisha shukrani isiyo na kifani, unyenyekevu na kuelewa,” alisema Alice Walker mshairi wa Amerika aliyezaliwa mwaka 1944.

Sema “Asante sana” kwa machache na makubwa, kwa vitu vya kawaida na visivyo vya kawaida. “Kile ambacho huwezi kukilipa kwa hela angalau kilipe kwa shukrani,” alisema Karl Simrock. Uhitaji pesa kusema maneno “Asante sana.” Kushukuru ni kulipa deni. “Yeyote anayepokea tendo jema kwa moyo wa shukrani tayari huwa amelipa awamu ya kwanza ya deni,” alisema Seneca mwanafalsafa wa Kigiriki.

Shukrani ina faida nyingi. Unaposhukuru hukatishwi tamaa. Kuna hadithi juu ya mtu aliyegundua ghala ambapo Shetani hutunza mbegu zake tayari kwa kupandwa kwenye moyo wa binadamu.

Aligundua mbegu za kukatisha tamaa zilikuwa nyingi sana kuliko mbegu nyingine. Alijifunza kuwa mbegu hizo zilifanywa kuchipuka karibu kila mahali. Shetani alipoulizwa juu ya mbegu za kukatisha tamaa kuweza kuchipuka kila mahali, alisita kidogo na kukiri kuwa kuna sehemu ambapo haziwezi kuchipuka. “Wapi?” aliuliza mtu huyo. Shetani alijibu kwa huzuni, “Katika moyo wa mtu mwenye shukrani.”

Shukrani ni dawa. “Dawa iliyobaki dhidi ya huzuni ni shukrani,” alisema Ida Friederike Gorres. Shukrani inazaa kuridhika. “Aliyeridhika anaweza akawa na furaha bali Yule mwenye shukrani huridhika,” alisema George Bernanos.

Shukrani huzaa furaha. “Shukrani hugeuza kumbukumbu kuwa furaha yenye ukimya. Inaleta ndani ya moyo jema la wakati uliopita, sio kama jambo linaloumiza bali kama zawadi yenye thamani,” alisema Dietrich Bonhoeffer. Unaposhukuru unaonesha wema. Kushukuru ni kuomba tena.

You can share this post!

Wanamaji kuandaa gwaride Mashujaa Dei

OBARA: Wanakibra wawe makini katika uchaguzi mdogo

adminleo