• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MUTUA: Majukumu ya magavana wasaidizi yawekwe wazi

MUTUA: Majukumu ya magavana wasaidizi yawekwe wazi

Na DOUGLAS MUTUA

WALE wanaotaka Katiba ya Kenya irekebishwe wakifanikiwa, basi mojawapo ya marekebisho lihusishe usimamizi wa serikali za kaunti ili ueleweke vyema.

Matatizo tunayoshuhudia kwenye kaunti mbalimbali nchini hayangekuwepo Katiba ingetoa mwelekeo bora badala ya kumrundikia gavana mamlaka yote.

Hali ilivyo sasa, naibu gavana anatambuliwa kama msaidizi mkuu wa gavana tu ilhali ikitukia kwamba gavana ameaga dunia, atachukua hatamu za uongozi.

Mtu ambaye hajawahi kuwa na majukumu mahsusi, isipokuwa pale alipotumiwa na mkubwa wake kama tarishi, ana tajiriba gani ya kusimamia kaunti?

Ukosefu wa kazi maalum una maana walipa ushuru wanaweza kumlipa mshahara asioufanyia kazi iwapo atakosana na mkubwa wake na kunyimwa kazi.

Tayari, tulikwisha shuhudia hali hiyo katika Kaunti ya Machakos kati ya 2013 na 2017 ambapo Gavana Alfred Mutua na Bw Bernard Kiala walilozana kila wakati.

Hitilafu hiyo imemwezesha Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kulisimamia jiji zima peke yake kama shamba lake; naibu awepo asiwepo, hazidishi hapunguzi.

Tangu aliyekuwa naibu wake, Bw Polycarp Igathe, ajiuzulu katika mazingira tatanishi takriban miaka miwili iliyopita, Sonko ametucheza shere kuhusu uteuzi wa naibu mpya.

Amewasilisha majina ya watu aliojua hawangekubalika mbele ya baraza la Kaunti, akawahoji wengine na hatimaye kuamua kutowapa kazi bila sababu sadikishi.

Hali ingekuwa tofauti, michezo ya kitoto kama hiyo haingeshuhudiwa. Cheo chenyewe hakingetumiwa kama chambo cha kuwanasa wanaokitamani wamsujudie Sonko.

Vilevile, Kaunti ya Pokot Magharibi haingekuwa bila naibu wa gavana; waliyechagua mnamo 2017, Dkt Nicholas Atudonyang, aliabiri ndege na kurejea kwake Amerika.

Angali huko akiendelea kufanya kazi ya udaktari huku Gavana John Krop Lonyang’apuo akitetea kutokuwepo kwake.

Mamlaka ni matamu; kwa Gavana Lonyangapuo haidhuru kuyatumia kama mayai eti. Sheria ingekuwa wazi, ufisadi wa aina hiyo haungeendelea.

Dkt Atudonyang, kwa kuipenda mno kazi yake ya udaktari, angesalia Amerika nacho cheo anachoshikilia nchini Kenya kingekuwa cha mtu mwingine anayehitaji kazi zaidi.

Katiba ingefafanua kuhusu kazi ya naibu gavana, hali ya taharuki inayotanda pale gavana anapoingia hali taabani ingepungua.

Kumbuka, wakati wa kampeni, kila gavana hutafuta mgombea mwenza anayeweza kumsaidia kuzoa kura nyingi zaidi, hivyo huo ni ubia wa makundi mawili yenye nguvu.

Gavana akipata matatizo yoyote asiweze kuketi ofisini, kundi lake hufanya kazi kubwa ya kulizuia lile la naibu wake kuchukua usukani wa kaunti.

Tulishuhudia hayo huko Bomet pale marehemu Gavana, Bi Joyce Laboso, alipolazwa hospitalini Uingereza na India, alipoonekana kuzidiwa vurugu zikazuka ofisini kwake.

Kundi lililomuunga mkono Bi Laboso lilipigana na la naibu wake, leo Gavana Hillary Barchok, naye Bw Barchok akadai kuidhibiti Kaunti kikamilifu! Ilibidi polisi wadhibiti hali. Hayo yalifanyika kabla ya Bi Laboso kufariki.

Ili kukipa heshima cheo cha naibu gavana na kumwondolea sifa mbovu za mpiga ubwete anayesubiri gavana aanguke amrithi, Katiba inapaswa kumpa mamlaka mahsusi.

[email protected]

You can share this post!

ONYANGO: Baringo sasa ni kitovu cha malaria, serikali iwe...

NGUGI: Mabinti wa kisasa wakome kuwananyanyasa waume katika...

adminleo