• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
JAMVI: Karata za kikabila zajitokeza Kibra

JAMVI: Karata za kikabila zajitokeza Kibra

NA CECIL ODONGO

Jamii ya Waluhya yadaiwa inaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba Benson Musungu anatwaa tiketi ya ODM huku Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Dagoretti Peter Ochieng Orero akipata uungwaji mkono wa Waluo hasa wabunge kutoka Luo Nyanza.

Bw Orero alikuwa mgombeaji mwenza wa aliyekuwa mbunge wa Kasipul Kabondo Oyugi Magwanga kwenye mbio za kuwania kiti cha ugavana wa Homa Bay katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Kulingana na takwimu ya IEBC mwaka wa 2017, eneobunge la Kibra lina wapigakura 118, 276. Kati ya idadi hii, inakisiwa kwamba karibu 40,000 ni Waluhya, Waluo 23,000, Wakikuyu 20,000, Wakamba 13,000, Wanubi 13,000 huku makabila mengine yakiwa ni 9,000.

Hata hivyo, inaaminika kwamba idadi kubwa ya wapigakura ya jamii ya Waluhya wanatoka kaunti jirani za Luo Nyanza kama Busia, Vihiga na Kakamega ambao mara nyingi hukumbatia mwaniaji Mluo.

Katika wadi zote tano za Sarang’ombe, Woodley, Makina, Laini Saba na Lindi, Wawakilishi Wadi watatu wanatoka Jamii ya Waluhya huku Waluo na Wakikuyu wakiwa na diwani moja kila moja.

Kuonyesha kwamba Waluhya wana azma ya kutwaa kiti hicho kivyvovote vile. kamati ya wazee wa jamii hiyo maarufu kama Obulala, wasomi na wanasiasa leo wanatarajiwa kuandaa mkutano mkubwa wa kuwachuja wawaniaji wa jamii hiyo katika uwanja wa Bukhungu, Kibra.

Lengo la mkutano huo kupata mwaniaji moja kutoka jamii hiyo kuchuana na wawaniaji wengine bila kutilia maanani chama atakachotumia kuwania kiti hicho.

“Mkutano wa Jumapili (leo) utalenga kuhakikisha kwamba jamii yetu inawasilisha mwaniaji moja kwenye mchujo wa ODM na njia mbadala ya kuhakikisha kwamba anaungwa mkono kupitia njia nyingine akikosa tiketi hiyo,” akasema moja wa waandalizi wa mkutano huo ambaye hakutaka jina lake linukuliwe na jarida hili.

Hata hivyo, kwenye mahojiano na Jamvi, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema hafahamu lolote kuhusu kuandaliwa kwa mkutano huo, akisisitiza chama hicho hakitajikita kwenye siasa za kikabila ila itaendeleza kampeni inayojumuisha jamii zote.

“Mimi sifahamu kama kuna mkutano ambao unaniambia. Mimi na Bw Osotsi (mbunge maalum) na Bw Malala (Seneta wa Kakamega) ndio viongozi wakuu wa jamii ya Waluhya na hatujaalikwa au kuhusishwa. Sisi tutaendesha kampeni zetu kwa msingi wa umoja wala hatutajihusisha na siasa za kikabila ambazo ni ujanja unaotumika na wapinzani wetu kutupiga vita,” akasema Bw Sifuna.

Aidha, alikanusha vikali madai kwamba ODM tayari ina mgombeaji maalum na mchujo unaotarajiwa ni wa kuwafumba macho wapigakura.

Vilevile aliondoa hofu kwamba mwanya wa siku moja wa kuyashughulikia malalamishi yatakayotokana na mchujo huo ni mdogo sana, akisema kura hiyo haitakuwa na malalamishi kwa sababu itakuwa yenye uwazi.

“Chama cha ODM hakitapendelea mwaniaji yeyote na mambo yangekuwa hivyo basi hatungepoteza zaidi ya Sh10 milioni kugharimia kura ya mchujo. Nakuhakikishia kwamba shughuli hiyo itakuwa na uwazi mkubwa na hakutakuwa na malalamishi. Kufikia Jumamosi jioni chama kitakuwa na mgombeaji ambaye atashabikiwa na wawaniaji wote walioshindwa,” akaongeza Bw Sifuna.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, itabidi Bw Odinga kuwa makini kuhakikisha kwamba ODM inapata mwaniaji ambaye anashabikiwa na jamii zote mbili ili asipate ugumu wa kumpigia debe.

“Kinyume na dhana kwamba Waluo ndio wengi Kibra, inaonekana Waluhya wamegutuka na sasa wanapigania kiti hicho wakitaka kipokezwe mmoja wao baada ya kushikiliwa na Waluo tangu mfumo wa vyama vingi uanzeDN body text:

“Japo ODM ndiyo chama maarufu Kibra, mkondo wa siasa utajulikana baada ya mchujo wa Jumamosi na mwelekeo utakaochukuliwa na watakaokosa kuridhika baada ya zoezi hilo. Hata hivyo, ishara zote zinaonyesha kwamba mwaniaji aidha atatoka jamii ya Waluo au Waluhya,” akasema Andati.

Hata hivyo, alisema uwaniaji wa Bw Owalo hautakuwa na athari zozote kwa sababu Bw Mudavadi hana ushawishi wowote katika siasa za Kibra huku uhasama kati ya mwaniaji huyo wa ANC na Bw Odinga ukididimiza zaidi matumaini ya chama hicho kutoa upinzani mkali.

“Bw Mudavadi hana ushawishi wa kisiasa Kibra na Bw Owalo naye anajaribu kutumia uwaniaji wake kama njia ya kulipiza kisasi dhidi ya Bw Odinga. Kumbuka hata Katibu Mkuu wa ANC Barack Muluka alikuwa mwandani wa Bw Odinga kabla ya kuhamia upande wa Bw Mudavadi,” akaongeza Andati.

Bw Mudavadi ambaye alizindua uwaniaji wa Bw Owalo Jumatano naye alisisitiza kwamba chama hicho kipo kwenye kiny’ang’anyiro hicho kikilenga kutwaa ushindi.

Eneobunge la Kibra limekuwa himaya ya kisiasa ya Bw Odinga ambaye alihudumu kama mbunge kutoka mwaka wa 1992 hadi 2013 kabla ya kumpisha marehemu Ken Okoth.

Chama cha Jubilee, jana kilimwidhinisha mwanasoka McDonald Mariga Wanyama kuwa mmoja wa wawaniaji 15 watakaomenyania tiketi ya chama hicho.

You can share this post!

WANDERI: Dawa ya masaibu ya Sossion ni kujiuzulu

JAMVI: Njama za Raila na Moi kuzima Ruto

adminleo