• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Gor Mahia na KCB zaanza Ligi Kuu kwa kasi

Gor Mahia na KCB zaanza Ligi Kuu kwa kasi

Na JOHN KIMWERE

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya KPL, Gor Mahia FC ilifungua kampeni zake kwa kupiga Tusker FC ya kocha, Robert Matano mabao 5-2 kwenye patashika iliyosakatiwa Moi Stadium, Kisumu.

Naye kocha, Zedekiah ‘Zico’ Otieno aliongoza KCB kulaza Sony Sugar mabao 3-0 Ugani Awendo matokeo yanayowapa makocha wa kikosi hicho matumaini ya kufanya vizuri muhula huu.

Wanabenki hao wanapigiwa chapuo kuibuka kati ya vikosi vitakavyozua upinzani mkali na kutesa kwenye mbio za kipute hicho.

Matokeo ya Gor Mahia FC na Tusker FC yalitamausha wengi kwa kuzingatia wana mvinyo hao walipigiwa upatu kuzua ushindani mkali dhidi ya wafalme hao lakini waliteleza na kupondwa magoli 5-2.

Naibu kocha wa KCB, Godfrey ‘Solo’ Oduor anahisi kuwa bado kikosi hicho kimekaa vizuri kuimarisha mchezo wacho zaidi kwenye ngarambe ya msimu huu.

”Tulipania kukunjua jamvi ya mechi zetu kwa ushindi na bila shaka tulitimiza azimio hilo ambapo kwa sasa tunalenga kusonga mbele,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa bado wanahitaji kushiriki mazoezi makali kukiweka kikosi hicho imara kukabili wapinzani wao.

Kocha huyo anadokeza kuwa muhula huu hawana la ziada mbali wamepania kufanya vizuri kinyume na msimu uliyopita. Matokeo hayo yamefanya KCB kutua katika nafasi ya pili nayo Gor Mahia FC ikiwa kifua mbele.

Kocha mpya wa Sony Sugar, James Nandwa akijitetea kufuatia kichapo hicho alisema walisajili wachezaji wapya kama wamechelewa ambapo kikosi chake hakijazoeana. ”Kamwe sina furaha kudondosha mchezo wa ufunguzi wala siwezi kulaumu wachezaji wangu mbali lawama nazielekeza kwa viongozi wangu,” Nandwa alisema na kuongeza kuwa pia alikosa huduma za wachezaji saba anaohisi wangebadilisha matokeo ya patashika hiyo.

KCB ni kati ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu muhula huu zilizofanya usajili wa nguvu kwenye jitihada za kujiweka vizuri kukabili makali ya wapinzani wao.

Menejimenti ya KCB ikiongozwa na ofisa wa kikosi hicho, Paul Russo ilisajili kocha mkuu kutoka Gor Mahia FC ili kuisadia kuhakikisha imefanya vizuri kinyume na muhula uliyopita ilipomaliza ya kumi kwa alama 45.

KCB inajivunia kunasa huduma za wachezaji tisa kwa kibarua cha msimu huu. Orodha ya sajili wapya inajumuisha:Golikipa Allan Owini (Uganda), kiungo Denis Odhiambo na strika Steven Waruru wote kutoka Sofapaka FC.

Pia ilinasa Pascal Ogweno (Gor Mahia FC), Regan Paul (Busia Olympics), Allan Owiny (Mathare United), Enock Agwanda (Sony Sugar), Ian Motanda na beki Moses Odhiambo wote kutoka Kisumu Allstars.

Nayo ‘K’Ogalo kando na kusajili vifaa kali pia ilipandisha ngazi wachezaji sita kutoka Gor Mahia Youth wakiwamo: Caleb Omondi, Alphonce Ombija, Lloyd Khavuchi, Godfrey Ombijo, Richdonald Bolo na Samuel Osok.

MATOKEO YA KPL WIKENDI

Gor Mahia FC 5-2 Tusker FC: K’Ogalo ilivuna ufanisi mnono kupitia nahodha, Kenneth Muguma alichangia kupata mabao matatu ambapo alifunga mabao mawili na kuchota frikiki iliyofungwa na Charles Momanyi.

Nao Nicholas Kipkirui na Boniface Omondi kila mmoja aliitingia goli moja. Tusker ilipata mabao hayo kupitia Boniface Muchiri aliyepiga kombora mbili safi.

Wazito FC 1-1 Nzoia Sugar: Wanasukari wa Nzoia walitangulia kupata bao hilo lililojazwa kimiani na Collins Wakhungu kabla ya mchezaji wa zamani wa Wazito FC, Elvis Rupia kusawazishia Nzoia Sugar.

Kisumu Allstars 0-2 Ulinzi Stars: Washiriki wapya, Kisumu Allstars ilikaribishwa kwenye mechi hizo inazoshiriki kwa mara ya kwanza kwa kipigo hicho mbele ya wanajeshi hao baada ya mfungaji bora msimu wa 2018-2019, Enosh Ochieng kutikisa wavu mara mbili.

Mchezaji huyo aliiweka wanajeshi hao kifua mbele dakika ya 46 baada ya kipa kutema shuti ya Elvis Nandwa. Hata hivyo Ochieng alikamilisha kibarua alipotia kimiani bao la pili dakika saba baadaye.

Mechi zingine: Sofapaka FC 1-2 Posta Rangers, Kariobangi Sharks 2-2 Western Stima, Mathare United 0-0 Bandari FC, Kakamega Homeboyz 1-0 AFC Leopards na Zoo Kericho 3-1 Chemelil Sugar.

You can share this post!

Kinyago yazikaranga MASA na Fearless bila uoga

‘Timu za mashinani hukuza wanasoka mahiri duniani...

adminleo