Habari

Joho achunguzwe kuhusu bandari – Jicho Pevu

September 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA SIAGO CECE

MBUNGE wa Nyali, Mohammed Ali (Jicho Pevu) ameitaka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na ile ya Kuendesha Mashtaka (DPP) kuchunguza familia ya Gavana Hassan Joho wa Mombasa kuhusu masuala ya Bandari ya Mombasa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule ya Penthouse Community eneo la Nyali, mbunge huyo alikashifu familia ya Bw Joho akisema imechangia kuzorota kwa biashara Pwani, hali ambayo imesababisha vijana wengi kukosa ajira na biashara nyingi kufungwa.

“Naomba DCI na DPP wachunguze madai kuwa familia moja ndiyo inayonufaika na bandari,” akasema Bw Ali.

Kauli ya Bw Ali ni kufuatia ripoti iliyochapishwa na gazeti la Sunday Nation juzi ikieleza kuwa familia ya Bw Joho imepangiwa kupewa kazi ya kusimamia eneo la mizigo katika kituo cha mizigo cha Nairobi (ICD) eneo la Embakasi.

Katika siku za majuzi Gavana Joho amekuwa akilaumiwa kwa kukosa kutetea wakazi na wafanyibiashara wa Pwani wakati Serikali Kuu inapoendelea kuhamisha biashara kutoka ukanda huo.

Kati ya hatua hizo ni kuagiza mizigo yote inayopakuliwa bandarini isafirishwe kwa reli ya SGR badala ya malori.

Kulingana na ripoti ya Sunday Nation, kampuni ya Autoport Freight Terminal imekuwa ikiomba Shirika la Reli la Kenya (KR) kuipa haki ya kipekee ya kusimamia eneo hilo la mizigo la ICD.

Bw Ali pia alitaka DCI na DPP kuchunguza kwa kina masuala ya ulanguzi wa dawa za kulevya katika Kaunti ya Mombasa.

“Siku chache zilizopita tumeona polisi wakisaka washukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya. Nataka niwaambie kwamba kuna wengine wengi hapa Mombasa ambao wanaharibu watoto wetu,” akasema Bw Ali.

Aliongezea kuwa ufisadi hauhusu tu maswala ya pesa lakini unahusisha pia kudhulumiwa kwa haki za wananchi.

Mbunge huyo aliwataka DCI na DPP wasiogope yeyote wanapofanya kazi yao.

“Nyinyi ndio macho ya wananchi kwa hivyo msitishiwe na yeyote mnapofanya kazi yenu. Nasimama na nyinyi kwa masuala ya haki na usawa,” akasema Bw Ali.