• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa Kisukari haubagui na huua kimyakimya

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa Kisukari haubagui na huua kimyakimya

Na BENSON MATHEKA

IDADI ya watoto wanaoambukizwa ugonjwa wa Kisukari Type 2 inazidi kuongezeka sawa na ya watu wazima.

Wataalamu wanasema maradhi haya yanatokana na mitindo ya maisha hasa wazazi kutokuwa waangalifu na aina ya chakula wanacholisha watoto wao.

Takwimu kutoka wizara ya Afya zinaonyesha kuwa asilimia 20 ya vifo nchini husababishwa na kisukari.

Wizara hiyo inasema kati ya watu 1.4 milioni na 2.1 milioni hupata kisukari kila mwaka. Hii inamaanisha mmoja kati ya watu 17 wana kisukari.

Aidha inasema watu 12,890 waliuawa na maradhi haya na msukumo wa damu 2014. Kulingana na shirika la kukabiliana na kisukari nchini, watu wazima 458,900 walipata kisukari 2017.

Takwimu za Shirika la Kukabiliana na Kisukari Duniani (International Diabetes Federation-IDF) zinasema kuna watu 425 milioni wanaougua kisukari ulimwenguni. Idadi hii iliongezeka kutoka 422 milioni mwaka 2014.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha watu 108 milioni walikuwa na kisukari 1980.

Nchini Kenya idadi ya wanaougua maradhi haya iliongezeka kwa asilimia 15 mwaka wa 2014. Nayo ripoti ya WHO inaonyesha asilimia sita ya Wakenya walikuwa na kisukari 2014 ikilinganishwa na asilimia 2.4 mwaka wa 1980.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Amref Health Africa, Dkt Githinji Gitahi, maradhi haya yanaathiri jinsi mwili unavyoshughulikia sukari ambayo huupatia nguvu.

“Wazazi wanapaswa kuacha kupatia watoto wao vinywaji na vyakula vinavyotengenezewa viwandani vilivyo na kiwango kikubwa cha sukari kama vile soda, keki na vibanzi na wapatiwe matunda kwa wingi kuwaepusha na kisukari Type 2,” aeleza.

Kulingana na Dkt Andrew Suleh, mwanaharakati na mtafiti wa afya, idadi ya watu wanaougua maradhi haya Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Kenya imeongezeka kutokana na ulaji wa vyakula vya hotelini, vyakula na vinywaji vilivyo na kiwango cha juu cha sukari, mvinyo, mfadhaiko na mitindo ya kisasa ya maisha.

“Sukari inaua wengi kuliko awali na hali itazidi kuwa mbaya kwa sababu wengi wanaendelea kukumbatia mitindo ya maisha inayoathiri afya yao,” asema Dkt Gitahi.

Wataalamu wanasema kwamba mtu hupata aina hii ya kisukari, mwili unaposhindwa kukabiliana na homoni ya insulini ambayo inadhibiti usambazaji wa sukari katika seli za mwili au mwili unapokosa kutoa homoni ya kutosha kudumisha viwango vya kawaida vya sukari.

Aina hii ya kisukari ilikuwa ikijulikana kama maradhi ya watu wazima lakini siku hizi watoto wengi wanagunduliwa kuugua kutokana na unene kupindukia unaoletwa na lishe duni.

Maradhi haya hayana tiba lakini madaktari wanapendekeza mtu kupunguza uzani wa mwili, lishe bora na mazoezi ili kukabiliana na makali.

“Kubadilisha lishe na kufanya mazoezi kukishindwa kupunguza makali ya maradhi haya, mgonjwa anaweza kupatiwa dawa za kukabili kisukari au kusawazisha insulini katika mwili,” asema Dkt Suleh.

Madaktatri wanasema dalili huanza taratibu na mtu anaweza kuwa na ugonjwa huo katika mwili wake kwa miaka mingi bila kujua.

Dalili

  • Kupata kiu kingi mara kwa mara
  • Kukojoa mara nyingi baada ya kunywa maji
  • Kuhisi njaa mara kwa mara
  • Kupunguza uzani
  • Uchovu
  • Kuona kiwi ( kutoona vyema)
  • Kupata vidonda vinavyochukua muda mrefu kupona
  • Kuambukizwa maradhi tofauti mara kwa mara
  • Sehemu za ngozi kwenye makwapa na shingo kuwa nyeusi kuliko kawaida.

Madaktari wanashauri watu kutafuta matibabu wakiwa na dalili hizi za kisukari.

“Mtu akiwa na ugonjwa huu, inamaanisha kuwa mwili wake hauwezi kuruhusu homoni ya insulini kufanya kazi au kongosho (pancreas) huwa haitoi insulini ya kutosha.

Sababu haswa ya hali hii haijulikani ingawa jeni na mazingira kama vile kuwa na uzani mkubwa na kutofanya mazoezi kunachangia,” wanaeleza matabibu kwenye tovuti ya www.mayoclinic.com.

Aidha watafiti wanasema kiwango cha sukari katika damu huongezeka badala ya kuingia katika seli za mwili.

Kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu husababisha seli zinazotoa insulini katika kongosho kutoa nyingi kupita kiasi ila hatimaye seli hizo kuharibika na mwili kukosa insulini ya kutosha.

Kutokana na mtindo wa maisha wa mtu, mwili unaweza kuharibu seli za kutengeneza insulini.

Walio katika hatari kubwa ya kupata maradhi haya ni;

  • Watu wanene: Ingawa wataalamu wanasema maradhi haya huwapata walio na uzani mzito, pia wanasema hata wasiokuwa na uzani mkubwa waweza kuambukizwa.
  • Mafuta mengi tumboni: Ikiwa una kiwango kikubwa cha mafuta katika tumbo, uko hatarini kuliko walio na kiwango kikubwa cha mafuta katika sehemu tofauti za mwili.
  • Kiuno kipana: Wataalamu wanasema wanaume walio na kiuno cha zaidi ya nchi 40 (sentimita 101.6 au wanawake walio na kiuno kinachozidi nchi 35 ( sentimita 88.9) wanakabiliwa na hatari kupata maradhi haya.
  • Kukosa kufanya mazoezi: Wataalamu wanasema kwamba watu wasiopenda kufanya mazoezi pia wanaweza kupata maradhi haya. Mazoezi hufanya mtu kupunguza uzani, kudhibiti presha ya damu, kujenga misuli na mifupa, kupunguza wasiwasi, kusawazisha sukari mwilini na kufanya seli za mwili kudhibiti insulini.
  • Familia: Endapo mzazi, ndugu au dada anaugua maradhi hayo, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuugua.
  • Rangi ya ngozi: Wataalamu wanasema haijulikani ni kwa nini Waafrika, Wahispania, Wahindi na Wamerika weusi hupata maradhi haya kwa wingi kuliko wazungu.
  • Umri: Ingawa maradhi haya yanawapata watoto siku hizi, wataalamu wanasema watu wanapoendelea kuwa na umri mkubwa hasa baada ya miaka 45, ndivyo wanavyokabiliwa na hatari zaidi. “Pengine ni kwa sababu katika umri huu, watu huwa hawafanyi mazoezi kwa wingi na uzani wa mwili huwa unaongezeka. Lakini siku hizi, watoto na vijana pia wako hatarini,” asema Dkt Suleh.
  • Kiwango cha sukari (Prediabetes): Hii ni hali ambayo kiwango cha sukari katika damu huwa juu kuliko kawaida kabla hakijafikia kiwango cha kuorodheshwa kama kisukari. Wataalamu wanasema hali hii ikikosa kutibiwa, huwa inabadilika na kuwa Type 2.

Aina mbili za Kisukari

Kuna aina mbili za ugonjwa wa kisukari.

1. Katika aina ya kwanza ni pale seli maalumu zinazotengeneza homoni ya insulini zinapokosekana katika kongosho.

Pia kongosho zinapoharibika kutokana na sababu yoyote ile, husababisha ukosefu kabisa au upungufu wa homoni hiyo kwenye damu.

Kwa mujibu wa wataalamu wa matibabu, aina hii ya kisukari ni hatari sana na huwaathiri zaidi watoto na vijana.

2. Aina ya pili ni wakati insulini huzalishwa kwa kiwango cha kutosha lakini inakosa kufanikisha utendakazi wake.

Mara nyingi mtu hupatikana na aina hii ya kisukari akiwa na umri mkubwa.

Hii inatokana na kupungua kwa utendakazi wa homoni ya insulini, au seli kushindwa kutumia insulini ipasavyo.

Wataalamu wanasema hali hii mara nyingi husababishwa na unene wa mwili, au hali ya kutofanya mazoezi kabisa.

Ugonjwa huu ukikosa kutibiwa unaweza kuathiri viungo muhimu vya mwili kama vile moyo, mishipa ya damu, neva, macho na figo.

Ili kuepusha hali hii, madaktari wanashauri watu kuhakikisha wanapimwa na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.

Athari zake

Kulingana na Dkt Suleh, mtu akikosa kutibiwa kisukari anaweza kupata;

  • Kiharusi: Kutokana na msukumo wa damu unaosababishwa na kudhoofika kwa mishipa ya damu, hali inayofahamika kama atherosclerosis.
  • Kuharibu neva: Kiwango cha sukari kikiongezeka katika mwili kinaweza kuharibu neva hali inayoweza kusababisha matatizo kama kutapika, kuhara na kwa wanaume kukosa nguvu za kiume.
  • Matatizo ya figo: Mtu anayeugua kisukari anaweza kupata matatizo ya figo na wakati mwingine zinaweza kuharibika kabisa.
  • Upofu na uziwi: Maradhi ya kisukari yanaongeza hatari ya kupata matatizo ya macho na masikio na hata kusababisha upofu na uziwi.
  • Kukosa kupata usingizi wa kutosha.

Kinga

Unaweza kuzuia maradhi haya kwa kupata lishe bora. Wataalamu wanashauri watu kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi, watumie matunda, mboga na nafaka.

Hivi ndivyo alivyoshauriwa Agnes Mumbua, 76, aliyegunduliwa kuwa na ugonjwa wa kisukari miaka 16 iliyopita.

“Nilikuwa nikihisi uchovu na kiu ajabu, maumivu ya hapa na pale hadi ilipogunduliwa nilikuwa naugua kisukari. Niliagizwa nile matunda na mboga kwa wingi na kuepukana na sukari na vyakula vyenye mafuta mengi. Na sasa licha ya umri wangu, najihisi mwenye afya,” asema.

Hata hivyo anasema huwa anamuona daktari kila baada ya miezi mitatu ili kupimwa kiwango cha sukari katika damu.

Aidha unapaswa kufanya mazoezi ya kadiri kwa kati ya dakika 30 na 60 au mazoezi makali kwa kati ya dakika 15 na 30 kwa siku ikiwezekana.

“Fanya matembezi kila siku, endesha baiskeli au ogelea. Mazoezi yanafanya mwili kuepuka maradhi kama kisukari,” aeleza Dkt Suleh.

Kwa watu wanene, wataalamu wanasema kupunguza kati ya asilimia tano na 10 ya uzani wa mwili kunaondoa hatari ya kupata kisukari.

“Usiketi kwa muda mrefu. Simama na kufanya matembezi baada ya dakika 30,” asema.

Gharama ya matibabu

Gharama ya kutibu kisukari nchini ni kubwa kuliko kufanya mazoezi.

Kulingana na shirika la kutathmini gharama ya matibabu ulimwenguni, matibabu ya kisukari ni takribani Sh50,000 katika hospitali za umma nchini na zaidi ya Sh130,000 katika hospitali za kibinafsi.

“Kwa sababu maradhi haya hayaponi, wanachofanya madaktari ni kupatia mtu dawa za kusawazisha insulini mwilini. Mtu anafaa kukumbuka kuwa kinga ni muhimu na kuepuka hali yoyote inayoweza kusababisha maradhi haya,” asema Dkt Suleh.

You can share this post!

Joho achunguzwe kuhusu bandari – Jicho Pevu

SHINA LA UHAI: Unene kupindukia shina la maradhi mengi...

adminleo