Makala

TEKNOHAMA: Google si daktari, wasema watafiti

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

CHAPATI hupikwa vipi? Nawezaje kupata mchumba mwaminifu? Dawa ipi inatibu maumivu ya kichwa? Hayo ni baadhi tu ya mamilioni ya maswali ambayo watu hutafuta majibu mitandaoni.

Ripoti iliyotolewa na kampuni ya Google Kenya, mwaka 2018 ilifichua kuwa idadi kubwa ya Wakenya walitaka kujua jinsi ya kupika chapati kupitia mtandaoni, kuandika barua ya maombi ya kazi, kupata ujauzito, kupunguza uzani na kuanzisha biashara.

Siku hizi ni jambo la kawaida kwa mtu kutafuta majibu mtandaoni anapokuwa mgonjwa.

Wengi wa vijana wanapohisi maumivu au dalili za ugonjwa huenda katika intaneti kubaini wanachougua.

Lakini wataalamu sasa wanahofia kuwa huenda mtandao unachangia katika vifo au kuongezeka kwa maradhi yanayosababishwa na matumizi mabaya ya dawa.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Matibabu cha Brighton and Sussex (BSMS) cha Uingereza, ulibaini kuwa taarifa zinazopatikana katika tovuti nyingi kuhusu matibabu ya magonjwa mbalimbali zinapotosha.

Watafiti hao walichunguza taarifa zilizochapishwa katika tovuti 200 kuhusu chanjo ya ugonjwa wa akili miongoni mwa watoto. Walibaini kuwa asilimia 24 ya tovuti hizo zilikuwa na taarifa za kupotosha. “Tumegundua kuwa taarifa kuhusu matibabu zinazopatikana katika intaneti ni za kupotosha,” akasema Profesa Pietro Ghezzi aliyeoongoza watafiti hao.

“Utafiti huu umeweka wazi kwamba taarifa zinazosomwa mitandaoni kuhusu matibabu zina dosari na hiyo ni hatari kwa afya,” akaongezea.

Utafiti huo uligundua kuwa idadi kubwa ya vijana hukimbilia intaneti kutafuta dawa wanapohisi dalili za magonjwa yanayochukuliwa kuwa ya ‘aibu’ kama vile kaswende, kisonono na kadhalika, badala ya kutafuta ushauri wa daktari.

Wataalamu wa matibabu walioshiriki katika utafiti huo wanasema kuwa baadhi ya vijana hununua dawa kutibu ugonjwa wanaohisi wanaugua kulingana na ‘tabibu’ wa intaneti.

“Baadhi ya magonjwa yana dalili sawa. Kwa mfano, unapohisi maumivu ya kifua, tumbo, kichwa; hizo zinaweza kuwa dalili za maelfu ya magonjwa. Unapokimbilia kununua dawa zilizopendekezwa katika intaneti bila kupimwa na daktari, huenda unatibu ugonjwa tofauti,” wakasema watafiti hao.

‘Mawazo tele’

Wataalamu pia wanaonya kuwa kutumia Intaneti kutaka kujua maradhi yanayokusumbua pia huenda kukakuongezea mzongo wa mawazo.

“Kwa mfano, unaweza kusakura mtandaoni dalili za maumivu unayohisi mwilini lakini intaneti inakuonyesha kuwa unaugua ugonjwa hatari kama vile kansa. Hali hiyo inaweza kukusababishia mzongo wa akili ilhali unaugua ugonjwa tofauti na wala si kansa,” anasema Dkt David Ayoki wa jijini Nairobi.

Dkt Ayoki anasema kuwa baadhi ya wagonjwa huenda kumwona daktari wakiwa tayari ‘wanajua’ ugonjwa wanaodhani wanaugua kulingana na intaneti.

“Daktari anapotaja ugonjwa tofauti, huwa vigumu kwao kuamini na hata wengine hukataa kutumia dawa walizopewa na kwenda kutafuta ushauri wa daktari mwingine,” anasema.

Anasema kuwa taarifa zinazochapishwa hazizingatii ubora kwani hakuna idara au taasisi ya kuhakikisha kuwa mambo yaliyoandikwa ni sahihi.

“Madaktari wamesomea taaluma hiyo kwa miaka mingi na wala intaneti haiwezi kuchukua majukumu yao. Intaneti inaweza kukusababishia mzongo wa mawazo na hata kukusukuma kujitoa uhai kwa kukupa taarifa za kupotosha kuhusu maradhi yanayokusumbua,” anasema.

Utafiti uliofanywa na shirika la Pew Research Center mnamo 2013, hata hivyo, ulisema kuwa Intaneti inaweza kumsaidia mtu kufahamu hospitali inayoshughulikia maradhi yanayomsumbua.

Intaneti pia inasaidia kutoa taarifa mbalimbali kuhusu afya.

Kwa mfano, ripoti ya Google ya 2018, ilionyesha kuwa idadi kubwa ya watu nchini Amerika walitaka kujua: ikiwa kweli chembechembe za bangi zinaweza kupatikana katika mkojo wa wavutaji.

Wengine walitaka kujua kinachosababisha shinikizo la damu kati ya magonjwa na hali nyinginezo zinazohusu afya.