Makala

VIDUBWASHA: Kupima upungufu wa damu mwilini (Emory Anemia Detector)

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

UNAPOJIHISI mchovu mara kwa mara, kupungukiwa pumzi, maumivu ya kichwa na kifua au ngozi kubadili rangi, kuna uwezekano mkubwa kwamba una upungufu wa damu mwilini.

Upungufu wa damu mwilini (maarufu anemia), hutokea kunapokuwa na chembechembe chache zinazosambaza oksijeni mwilini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watu bilioni 2 kote duniani wanaugua maradhi ya anemia.

Watumiaji wa simu zilizo na kamera huenda sasa wakafahamu ikiwa wanaugua maradhi ya anemia au la.

Hii ni baada ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Emory, Amerika kugundua Emory Anemia Detector, programu ya simu (app) inayoweza kupima anemia kwa kutathmini picha ya kucha.

Kulingana na matokeo ya utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Nature Communications, apu hiyo inaweza kubaini upungufu wa seli zinazosafirisha oksijeni mwilini au ukosefu wa madini ya chuma.

Rangi ya kucha

Aidha inaweza kutambua ikiwa mtu ana anemia au la kwa kuchunguza rangi ya kucha.

Apu hiyo iligunduliwa na mwanafunzi wa Uzamifu chuoni hapo Rob Mannino, ambaye alikuwa akiugua anemia.

Mannino anasema kuwa alichoka kwenda hospitalini kupimwa kiwango cha chembechembe zinazosafirisha gesi ya oksijeni mara kwa mara.

Alimhusisha mwanafunzi mwenzake wa uzamifu katika kuunda programu hiyo.