Waelezea jinsi wanavyopata soko kutokana na matangazo ya vifo na shughuli katika mochari
Na MWANGI MUIRURI
NI sawa tu mpendwa wenu ameaga dunia ndio, lakini sisi tulio hai ni lazima tulisukume gurudumu la maisha, hilo ndilo wazo la mfanyabiashara James Mburu ambaye huchuuza bidhaa zake katika hifadhi za maiti akilenga wateja waombolezaji.
“Mimi hujitokeza katika mochari mbalimbali za eneo la Mlima Kenya nikiwa nimebeba bidhaa kama keki, soda, maji safi ya kunywa na kadi za mjazo wa simu za rununu,” asema Bw Mburu.
Anasema kuwa hata ikiwa hujifahamisha sana na mahangaiko ya kihisia katika bongo za waombolezaji, “bado ninatambua kuwa hawa walio hai maisha yao lazima yaendelee kama kawaida na katika hali hiyo, watahisi kiu, njaa na hitaji la kula vitamu; hivyo ninawauzia.”
Mchuuzi mwingine, Bi Mercy Waithera, naye anasema kuwa mochari hukusanya watu wengi pamoja na hilo ni soko.
“Labda niseme tu kwamba kwa kuwa ushindani wa kibiashara hauko juu katika maeneo haya, huwa tunaongeza pesa kidogo juu na faida huwa ya kuridhisha,” asema Bi Waithera.
Anasema kuwa kwa kuwa ni mpango wa Mungu kuwa kuwe na siku ya kuzaliwa na siku ya kuaga dunia, na katika hali hiyo kuwe na wengine wa kubakia wakiwa hai, ni lazima maisha ya kila safu kuendelea mbele, la mno harakati za kujiongezea ubora wa kimaisha kupitia riziki.
Mwingine ni Harry Kimani kutoka Kaunti ya Murang’a ambaye huwa na wazo lingine la kipekee kibiashara.
“Huwa ninachukua gazeti la Daily Nation na kupekua sehemu ya matangazo ya vifo. Hasa ninaangalia ni wapi kuna uwezekano wa miili ya familia zinazojiweza hutolewa ikielekezwa kuzikwa na nikichambua ndugu za marehemu nione wana majina makubwa ya kitaaluma, basi ninajua wazi kuwa waombolezaji watakaojitokeza watakuwa si wa kuishiwa na fedha,” asema Bw Kimani.
Anasema kuwa huwa anafuatilia wale ambao ndugu zao wanafanya kazi za uhandisi, uwakili, ni wafanyabiashara shupavu, au ndugu na jamaa walio katika mataifa ya kigeni.
Hapo hujipa wazo kuwa akiunda mradi wa kibiashara akiwalenga, hataenda nyumbani mkoba ukiwa umechanika.
“Si unajua hata mkoba wa pesa ukiwa na uzee wake na pia uchafu lakini uwe umejaa mabunda ya pesa mara moja hubadilika na kuwa mpya?” azua ucheshi.
Akikutana na Taifa Leo, ilikuwa ni Jumanne ya Agosti 27 katika hifadhi ya maiti ya Montezuma Monalisa tawi la Murang’a lililoko katika Kaunti ndogo ya Gatanga na ambapo shughuli kati ya zingine ilikuwa kutwaa mwili wa marehemu mwanamke mmoja ambapo ulikuwa usafirishwe hadi kijiji cha Hiriga, Kaunti ya Nyeri kuzikwa.
“Huyu marehemu niligundua kuwa jamaa wake ni wadosi. Nilichukua picha yake kutoka kwa gazeti na nikainakili na nikatengeneza upya kwa urembo na nakshi na nikaipa ujumbe “Kusherehekea Maisha ya *Mwafulani”. Nilijitokeza na picha hizo mpya zikiwa 200 na niliziuza kila moja kwa Sh50. Walinunua zote na nikajipa pato langu la siku la Sh10,000,” asema.
Hatua yake hii muhimu kusema hapa huenda inakiuka mambo muhimu ya kimaadili.
Kwa siku sita akifanikiwa, kwa kuwa eneo hilo wengi hawaziki wendazao Jumapili, basi anakuwa wa kupata hata Sh60,000.
“Ninajua wengine ambao ni vibarua mashambani ambao hujipa Sh200 kwa siku. Wasaidizi wa mafundi hujipa Sh500 kwa siku. Unahitaji tu kuwa mbunifu na utapata kuwa kilio kuwa hakuna nafasi za kazi ni kelele tu zisizo na msingi. Kwa mwezi ninaweza nikajihakikishia pato la Sh240,000 kutoka kwa biashara ndani ya hifadhi za maiti,” asema.
Wengine ambao huvuna nafuu ni wauzaji wa maua, wapigaji picha na wauzaji vitambaa spesheli vya rangi nyeupe ambavyo mara nyingi hutumika katika mazishi.
Pia, kuna baadhi ambao hujitokeza katika hifadhi hizo wakiwa na nia ya kupora waombolezaji na wakifahamu kuwa wengi wamechanganyikiwa katika hali ya maombolezi na kwa kufahamu kuwa huwa hakuna doria za polisi, huvuna kutoka kwa majonzi, ingawa yasemwa wazi kuwa hivyo vya bwerere havifai kunenepesha yeyote.