• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Gor Mahia kileleni ligi ikipisha mechi za mataifa kirafiki

Gor Mahia kileleni ligi ikipisha mechi za mataifa kirafiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Gor Mahia FC imechukua uongozi wa mapema wa Ligi Kuu ya msimu 2019-2020, ambayo itarejea Septemba 14 baada ya mechi za kimataifa.

Gor almaarufu K’Ogalo inawinda taji lake la 19 kwa jumla na nne mfululizo. Ilipepeta washindi mara 11 Tusker 5-2 kurukia juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 18.

Ilitumia vyema uwanja wake wa Moi kuzamisha wanamvinyo hao kupitia kwa mabao ya nahodha Kenneth Muguna (mawili) na Nicholas Kipkirui, Charles Momanyi na Boniface Omondi. Vijana wa Steven Pollack walifungwa mabao mawili kupitia kwa Boniface Muchiri.

KCB, ambayo iliajiri kocha msaidizi wa Gor Zedekiah Otieno kuwa kocha wake mkuu wiki chache zilizopita, inashikilia nafasi ya pili baada ya kulaza wenyeji SoNy Sugar 3-0 kupitia sajili wapya Enock Agwanda, Stephen Waruru na Dennis Odhiambo.

Zoo inafuata katika nafasi ya tatu. Ilijizolea alama tatu muhimu kwa kulemea wageni wake Chemelil Sugar 3-1 uwanjani Kericho Green kupitia kwa mabao ya wachezaji Kepha Ondati (mawili) na Derrick Anami. Chemelil ilijiliwaza na bao kutoka kwa Rashid Athman.

Mabao mawili kutoka kwa mfungaji bora wa msimu uliopita Enosh Ochieng’ yalitosha kusaidia washindi mara nne Ulinzi Stars kupata alama zote dhidi ya washiriki wapya Kisumu All Stars na kukalia nafasi ya nne.

Posta Rangers ni ya tano baada ya kunyamazisha wenyeji wao Sofapaka 2-1 kupitia kwa mabao ya Gerson Likono na Eliud Lokuwam. Mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka walifungiwa bao la kutoa machozi na mchezaji Elli Asieche.

Kakamega Homeboyz inakamilisha orodha ya timu zilizoshinda mechi za raundi ya kwanza. Iliendeleza ukatili wake dhidi ya washindi mara 13 AFC Leopards ilipowakaribisha mjini Kakamega kwa kichapo cha bao 1-0. Sajili mpya Stephen Etyang alitikisa nyavu za Leopards dakika za lala-salama.

Kariobangi Sharks, ambayo ilichapa klabu ya Everton katika mechi ya kimataifa jijini Nairobi mwezi Julai, inashikilia nafasi ya saba kwa pamoja na Western Stima kwa alama moja kila mmoja.

Sharks ilikabwa 2-2 nyumbani na Stima uwanjani Machakos. Mfungaji bora wa mwaka 2018 Eric Kapaito na Patrick Otieno walifungia Sharks nao Kennedy Owino na Samuel Odhiambo walipachika mabao ya Stima.

Bega kwa bega

Nzoia Sugar na Wazito ziko bega kwa bega katika nafasi ya tisa baada ya kutoka 1-1 uwanjani Kenyatta. Collins Wakhungu alifungia Nzoia kabla ya Elvis Rupia kusawazishia Wazito iliyokuwa nyumbani.

Bandari na mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United wanakamilisha orodha ya timu zilizoambulia alama katika mechi zao za ufunguzi wikendi. Bandari na Mathare zilizoa alama moja kila mmoja baada ya kutoka 0-0 uwanjani Ruaraka.

Sofapaka, Leopards, Chemelil, Kisumu All Stars, Tusker na SoNy zinashikilia nafasi sita za mwisho mtawalia bila alama.

Muchiri, Muguna, Ochieng’ na Ondati wanaongoza vita vya kunyakua tuzo ya mfungaji bora baada ya kila mmoja kucheka na nyavu mara mbili.

You can share this post!

Lengo la Arsenal ni kutinga 4-bora msimu huu – Emery

Bale aisaidia Madrid sare dhidi ya Villarreal

adminleo