Shule mbioni kupaka mabasi rangi ya manjano muda ukiyoyoma
KALUME KAZUNGU na WANDERI KAMAU
Kwa ufupi:
- Dkt Fred Matiang’i alitoa agizo kwamba lazima mabasi ya shule zote za msingi na upili za umma yawe yamepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31
- Kwa kuyapaka rangi hiyo ya manjano, inakuwa rahisi kwa mtu kugundua kuwa hayo ni magari ya shule
- Katika maeneo mengiya nchi, mekanika wa kupaka rangi magari walionekana wakiwa katika hatua za mwisho, kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi
- Kenya inaonekana kuiga nchi kama Amerika na Canada, ambako magari yote ya shule huwa yana rangi ya manjano
ZIKIWA zimesalia siku tano kabla ya kukamilika kwa makataa kwa shule zote nchini kupaka rangi magari ya kubeba wanafunzi, walimu wakuu na wamiliki wa shule wamo katika harakati za mwisho kutimiza agizo hilo.
Aliyekuwa Waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiang’i alitoa agizo kwamba lazima mabasi ya shule zote za msingi na upili za umma yawe yamepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31.
Dkt Matiang’i alisema kwamba agizo hilo linalingana na Sheria ya Trafiki, ambayo ilipitishwa na Bunge mnamo 2016.
Hatua hiyo inaonekana kuchangiwa na ongezeko la ajali za barabarani, ambapo iligunduliwa kuwa baadhi ya magari yaliyokuwa yamekodishwa kusafirisha abiria, yalikuwa ya shule.
Kulingana na sheria hiyo, jina la shule husika linapaswa kuandikwa kwa rangi nyeusi.
Rahisi kutambulika
Kwa kuyapaka rangi hiyo ya manjano, inakuwa rahisi kwa mtu kugundua kuwa hayo ni magari ya shule, na kwa hivyo hatua za haraka zinaweza kuchukuliwa iwapo madereva wa magari hayo watapatikana wakiendeleza mambo yanayoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.
Sheria hiyo pia inayahitaji mabasi hayo kuwa na mikanda ya usalama katika viti vyake vyote.
“Shule zote zinapaswa kuhakikisha kwamba zimetimiza kanuni hizo kufikia Machi 30, kama inavyohitajika kisheria. Hatutakubali visingizio vyovyote kuhusu suala hili,” akasema waziri.
Sheria hiyo pia inasema kuwa mabasi hayo yanapaswa kuendeshwa kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa.
Mwendo wa kasi umekuwa mojawapo ya mambo ambayo yamechangia ongezeko la ajali za barabarani. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, kumekuwa na ajali kadha ambazo zimehusisha mabasi ya shule katika maeneo ya Nyanza na Kisii.
Kanuni nyingine ni kwamba yataruhusiwa kuhudumu kati ya saa 12 asubuhi na jioni pekee, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Kuiga mataifa ya Magharibi
Kulingana na wadadisi wa masuala ya elimu, Kenya inaonekana kuiga nchi kama Amerika na Canada, ambako magari yote ya shule huwa yana rangi ya manjano.
Katika kaunti ya Lamu, shule zote za mzingi na za upili zinazomiliki mabasi zimetimiza amri hiyo.
Akizungumza Jumapili na Taifa Leo, Afisa wa Elimu wa Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi, Bw Josphat Ngumi, alisema ni shule mbili pekee za upili – ile ya wavulana ya Mpeketoni na shule ya sekondari ya Mokowe ambazo zinamiliki mabasi kati ya jumla ya shule 26 za umma zilizoko Lamu.
Alisema shule ya kibinafsi ya Tamani Junior Academy iliyoko Mpeketoni ndiyo shule ya msingi ya kipekee ambayo inamiliki basi kati ya shule 104 zilizoko eneo hilo.
Kwa mujibu wa Bw Ngumi, shule zote tatu kwa sasa zimehakikisha mabasi yao yamepakwa rangi ya manjano kama ilivyoamriwa.
“Hapa Lamu kuna shule mbili pekee za upili zinazomiliki mabasi ambazo ni Mpeketoni na Mokowe. Pia kuna shule moja pekee ya msingi ya kibinafsi ambayo ni Tamani Junior Academy iliyoko Mpeketoni ambayo ina miliki basi. Shule zote tatu zimetii sheria kwa kuhakikisha magari yao yanapakwa rangi ya manjano,” akasema Bw Ngumi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya wavulana ya Mpeketoni, Bw Macharia Kagutha alisema basi lao lilipakwa rangi takriban wiki tatu zilizopita.
Gharama ya kupaka rangi
“Tulisafirisha basi letu hadi Mombasa ambako lilipakwa rangi na kampuni ya Assosiated Motors. Tulitumia Sh127,000 katika kutekelezewa huduma hiyo. Kwa sasa liko sawa,” akasema Bw Kagutha.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mokowe, Bw Thaddeus Mogute, alisema shughuli ya kulipaka rangi gari hilo tayari ishaanza na itakamilika juma hili.
“Tunalenga kutumia kati ya Sh 130,000 na Sh 150,000 ili kupaka rangi ya manjano basi letu na pia kulikarabati. Tayari niko Mombasa na shughuli itakuwa imekamilika kufikia mwishoni mwa wiki hii,” akasema Bw Mogute.
Katika maeneo mengine ya nchi, mekanika wa kupaka rangi magari walionekana wakiwa katika hatua za mwisho, kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi ya kupaka rangi hiyo ya manjano kwenye magari yaliyopelekwa katika gereji zao.
Kulingana na kanuni zilizotolewa na serikali, hata matatu na magari ya kibinafsi yatakayotumiwa kuwabeba wanafunzi wa shule, yatahitajika kuwa na rangi hiyo ya manjano.