• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
ONYANGO: Isiwe Mau pekee, wote wanaoishi misituni watoke

ONYANGO: Isiwe Mau pekee, wote wanaoishi misituni watoke

Na LEONARD ONYANGO

TANGU serikali kutangaza azma yake ya kutaka kufurusha maskwota kutoka katika Msitu wa Mau, kumekuwa na mjadala mkali ikiwa hatua hiyo inaongozwa na siasa za 2022 ama kweli inalenga kuhifadhi mazingira.

Katika awamu ya kwanza ya ufurushaji mnamo Julai mwaka jana, serikali iliondoa zaidi ya watu 7,700 kutoka katika ardhi ya ukubwa wa ekari 12,000 ndani ya Msitu wa Mau.

Lakini baadhi ya wanasiasa wa Bonde la Ufa walijitokeza kupinga vikali huku wakidai kwamba shughuli hiyo inalenga kumharibia Naibu Rais William Ruto safari yake ya kutaka kuingia Ikulu 2022.

Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko, wiki iliyopita alisema kuwa awamu ya pili ya kuwafurusha watu kutoka Msitu wa Mau itaendelea haswa katika maeneo ya Nkoben, Ilmotiok na Ololunga licha ya kuwepo kwa pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi kutoka Bonde la Ufa.

Bw Tobiko alisema serikali tayari imebatilisha hatimiliki 1,200 za mashamba ambazo maskwota hao walijipatia kupitia njia za udanganyifu.

Wafuasi wa Dkt Ruto wanahisi kwamba hatua ya serikali kufurusha watu kutoka Msitu wa Mau ina njama fiche ya kisiasa.

Mahasimu wa kisiasa wa Dkt Ruto na wanasema hatua hiyo ya serikali kama njia mojawapo ya kuhifadhi mazingira.

Hii ni kwa sababu Msitu wa Mau umekuwa ukitumiwa na wanasiasa kwa masilahi yao ya kisiasa uchaguzi unapokaribia.

Kwa mfano, kinara wa ODM Raila Odinga alijaribu kuwafurusha maskwota kutoka Msitu wa Mau alipokuwa Waziri Mkuu wakati wa Serikali ya Mseto na alikumbwa na ghadhabu ya wakazi wa Bonde la Ufa katika uchaguzi wa 2013 alipowania urais.

Chama cha Jubilee pia kilitumia Msitu wa Mau kujizolea kura katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Tobiko hana budi kujitokeza na kudhihirishia Wakenya kwamba hatua ya serikali kuwahamisha maskwota kutoka Msitu wa Mau inalenga kuhifadhi mazingira na wala si ya kisiasa. Kuthibitisha hilo, serikali haina budi kuhakikisha kwamba watu wanaotolewa ndani ya Msitu wa Mau wanapewa makao mbadala badala ya kuachwa kuhangaika.

Aprili mwaka jana, Bw Tobiko aliteua jopokazi la kuchunguza uharibifu wa misitu nchini.

Kwenye ripoti yake, jopokazi hilo lilibaini kwamba uharibifu wa misitu umeshika kasi katika karibu misitu yote nchini kama vile Mau, Mathews (Kaunti ya Samburu), Marsabit (Kaunti ya Marsabit), Chyullu Hills (Makueni/Kajiado), Loita Hills (Narok), Marmanet na Ol Arabel (Laikipia), Aberdares, Cherangani, Mlima Elgon kati ya misitu mingineyo.

Serikali inafaa kutumia ripoti hiyo kufurusha watu wanaoishi katika misitu yote iliyotajwa katika ripoti hiyo.

Kwa kufanya hivyo, Wakenya watakuwa na imani kwamba serikali kweli inalenga kutunza mazingira na wala hailengi jamii moja kisiasa.

You can share this post!

NGILA: KRA isikubali biashara za mitandaoni zikwepe ushuru

TAHARIRI: Mzozo wa seneti na bunge unaumiza raia

adminleo