• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
WASIA: Ziambae sauti za kukufisha moyo na kukukatisha tamaa muhula huu

WASIA: Ziambae sauti za kukufisha moyo na kukukatisha tamaa muhula huu

Na HENRY MOKUA

KUNDI la vyura liliondoka kwenda safarini.

Katikati mwa safari, wawili kati ya vyura wale, walianguka kwenye tundu fulani.

Shimo lenyewe lilikuwa la kina cha kadri; si kirefu, si kifupi. Wenzao walipogundua hawapo pamoja nao na kuanza kuwasaka ndiyo waliwasikia wakisononeka ndani ya shimo lile, wanajaribu kujiokoa wasiweze.

Wenzao waliemewa, wakaamua hawana msaada mwingine ila kuwashauri: humo hamtoki kamwe, heri mkubali mngoje kifo!

Waliendelea kujaribu na baada ya muda mfupi, chura mmoja alitia maanani ushauri wa wenziwe na kukoma kujaribu. Aliamua kukikabili kifo sasa, uso kwa macho. Baada ya saa kadhaa, alikufa.

Muda huu wote, yule chura mwingine alikuwa akijitahidi ingawa angejipa dakika chache za kupumzika.

Ghafla, wenziwe waliokuwa wanazidi kumshauri akome kujisumbua, walimshtukia ametoka shimoni. Walishangazwa sana na jitihada zake, lakini zaidi, na kuwapuuza alikowapuuza. Ni katika harakati ya kutaka kujua mbona hakuwasikiliza walipogundua kwamba kumbe alikuwa kiziwi! Ajabu iliyoje!

Je wewe umewahi kujikuta katika hali sawa na ya vyura walioanguka shimoni? Ulichukua hatua gani kujitoa mle? Yawezekana umo shimoni hata unaposoma makala haya? Unapohimizwa na wenzio kwamba somo fulani ni gumu, waliona hili kama shimo? Mara kwa mara tunajikuta katika hali za kutatanisha na kutamausha.

Ikitokea kwa bahati mbaya ukazungukwa na watu wanaoifanya hali yako kuwa mbaya zaidi, hata kifo huwa hakipo mbali nawe – labda cha kiroho, kiuchumi, kijamii, kihisia, kiafya au kiakademia.

Ijapo hatugundui sana, rafiki zetu huwa na mvuto wa ajabu kwetu. Hata ninapoandika makala haya nawakumbuka wanafunzi wangu wengi wa sasa na wa awali ambao rafiki zao wa karibu ama wamewafaa au kuwasababisha kufeli. Kwa hivyo? Chunguza umezungukwa na nani, unatangamana na nani na nani unatagusana naye kwa karibu. Watu hawa waweza kukudimiza ajabu.

Ikitokea kwamba watamaushi wamekuzunguka bila wewe kupangia wala kuruhusu, jitie uziwi. Maneno uyasikiayo mara kwa mara, japo uyakatae mwanzoni, hatimaye huanza kuyaamini na yaweza kukuathiri.

Fanya hiari kumkimbia kila mwenye kauli za kukukatiza tamaa. Ikibidi, zikabili kauli hizo kwa kauli za kujipa tumaini muradi unachukua hatua mwafaka zinazofungamana na ufanisi.

Kwa mfano, wazo la namna Kiswahili kilivyo kigumu linapowasilishwa, tia kauli yako kwamba hata hivyo, wapo wengi na ambao unawafahamu na wanakimudu.

Ikiwa ni suala la wanafunzi kutoka shuleni mwako kutowahi kupata alama fulani, jipe kuamini kwamba walikuwepo wakati wao na sasa mambo yamebadilika na nafasi ya kuwapiku ipo; hasa zaidi, wao ni wao na wewe ni wewe; kila mmoja na uwezo wake!

Habari njema ni kwamba hujachelewa sana kuchukua hatua ya kujikomboa. Ninaweza kukiri kwamba nimewasaidia na kushuhudia wanafunzi wengi kubadili nia kisha mambo yakawatengenea.

Hatua ya awali zaidi ni kufanya uamuzi kwamba wakati umewadia kwako kufanya badiliko. Jiaminishe kwamba hapana wakati mwingine utakaofaa zaidi kwako kujinusuru kuliko sasa.

Jihakikishie aidha kwamba hamna mtu anaweza kukupenda zaidi ya ujipendavyo wewe; kwa hivyo, usipojiokoa mambo yako yatazidi kuvurugika tu. Mbona uyaruhusu yavurugike lakini kana kwamba upo katika awamu ya majaribio na fursa ya kuishi hasa ipo mbele?

Hakika ni kwamba hukuwa na usemi katika harakati nzima ya kuingizwa ulimwenguni, lakini hatima yako inakutegemea wewe, naam, wewe tu! Ukilitelekeza jukumu hili ujue una maswali mengi utakyohitajika kuyajibu.

Muhula mfupi

Mengi ni ya wategemezi wako wa halafu, na mengi zaidi, ya muumba wako!

Ni lipi la kufanya basi katika muhula huu ambao unaaminiwa kuisha hata kabla haujaanza? Muhula ni mfupi ndivyo lakini si kwako tu – u mfupi kwa washindani wako pia. Katika siku ya tatu hii ya muhula, jiketishe na kushauriana kwa kina na nafsi yako.

Hivi, ndoto yangu ni ipi katika muhula huu? Ikiwa wewe ni mtahiniwa jiulize: uwezo wangu waweza kunifikisha kwenye alama gani nikifanya yanipasayo? Fanya uamuzi kisha uteue mtu ambaye mnaweza kuelewana na kuhimizana katika azma hii.

Ukijiamini na mwenzio aliyemakinika akakuhakikishia unaweza, uwezekano mkubwa ni kwamba utafuzu – hata ukakosa alama uliyoitazamia, angaa itakuwa afadhali kuliko ile ambayo ungepata bila uamuzi huu.

Usisite kuhusisha pia mwalimu unayeweza kumwaminia ndoto zako. Shauriana naye mara kwa mara, kila siku ikiwezekana ili akupe mwongozo hatua kwa hatua. Tenga muda wa kufanya mazoezi, wala usiutenge tu; fanya mazoezi ili kuichangamsha akili yako.

Mwisho, jikabidhi kwa Muumba wako na kutumai atakutengeza vilivyo sawa na udongo usivyopishana na mfinyanzi.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Samuel Mwenda

‘Jinsi nilivyofurahia likizo’

adminleo