• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
NDIVYO SIVYO: Kimbelembele, si kiherere huonyesha ‘kujipendekeza’

NDIVYO SIVYO: Kimbelembele, si kiherere huonyesha ‘kujipendekeza’

Na ENOCK NYARIKI

MARA nyingi neno kiherehere linapotumiwa na watu katika mawasiliano huibua dhana mbalimbali ambapo hakuna moja kati yazo inayoakisi maana halisi ya neno lenyewe.

Baadhi ya watu hulitumia neno lenyewe kumrejelea mtu ambaye daima hujipendekeza au hujifanya ili kuonekana bora zaidi ya wengine. Aidha, neno lenyewe huashiria hali yenyewe; yaani mtu ambaye hupenda kujipendekeza ili kupata faida fulani kwa watu wengine husemekana kuwa na kiherehere.

Neno Kiherehere pia hutumiwa kwa njia chanya kumrejelea mtu ambaye kila wakati hujibidiisha kuwa wa kwanza katika kutenda mambo au kujipalia sifa fulani.

Ijapokuwa hizi ndizo maana tatu za neno hilo ambazo watu wengi huzifahamu, hakika, tulivyosema katika utangulizi wa mjadala huu, hakuna moja kati ya maana hizo inayoafiki maana halisi ya neno lenyewe.

Kabla ya kuingia katika kitovu cha mjadala, ni muhimu kulitaja neno linalofafanuliwa kwa kijelezi cha kwanza katika utangulizi wa makala yetu: kujipendekeza au kujifanya kuonekana bora zaidi ya wengine.

Kamusi Elezi ya Kiswahili imeliweka neno kimbelembele katika ‘kategoria’ mbili.

Nimelitumia neno “kategoria” kwa maana ya aina za maneno ijapokuwa neno lenyewe linaweza pia kutumiwa kwa maana nyingine tofauti. Kwanza, kimbelembele ni nomino inayomaanisha mtu aliye na tabia ya kujipendekeza na kujifanya aonekane yeye katika shughuli fulani na pia aonekane bora zaidi miongoni mwa wengine.

Pili, kamusi hiyo imelipa neno hilo dhima ya kielezi kikiwa (kielezi hicho) na maana ya tabia ya kujipendekeza na kujifanya kuonekana katika shughuli fulani au kuonekana bora kuliko wengine. Kwa hivyo, si sahihi kulitumia neno kiherehere kumrejelea mtu au tabia ya kujipendekeza na kujifanya kuonekana bora kuliko wengine.

Kukosa utulivu

Neno kiherehere lina maana ya hali ya mtu kukosa utulivu kutokana na jambo fulani. Mfano: Juma ameingiwa na kiherehere kuhusu karo ya watoto wake.

Neno wahaka linaweza pia kutumiwa kwa maana ya wasiwasi na ukosefu wa utulivu ila hili la pili lina uzito zaidi unaoletwa na visawe vyake. Kisawe kimojawapo cha wahaka ni kihoro.

Katika mazungumzo, neno kihoro huibua maana zaidi ya ile ya kuwa na wasiwasi. Kihoro ni huzuni kubwa au majonzi anayoingiwa nayo mtu kutokana na msiba.

Alhasili, si sahihi kutumia neno kiherehere kwa maana ya mtu au tabia ya kujipendekeza au kujifanya kuonekana bora miongoni mwa wengine katika shughuli fulani.

Neno linalopaswa kutumiwa katika mazingira hayo ni kimbelembele.

You can share this post!

Walivyozimwa kwa minofu

ODM yawataka wanaolenga tiketi Kibra wajiepushe na vurugu

adminleo