• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wasimulia wanavyotumia sanaa kujilipia karo

Wasimulia wanavyotumia sanaa kujilipia karo

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Kwa muda mrefu sanaa na ufundi, kwa wengi ni shughuli inayofanywa kwa kujifurahisha tu. Kwa wengine, sanaa ni kitu wanafanya kwa raha zao baada ya kazi.

Lakini kazi hii inayoonekana kuwa ya kujituliza tu imegeuka kuwa muhimu sana kwa wanafunzi wawili wa taasisi ya mafunzo ya Rift Valley Institute of Science and Technology (RVST) kwenye Kaunti ya Nakuru.

Brian Ochieng, 23, na Brian Kiptoo, 25, hutengeneza sanaa ya uchoraji na uchongaji vinyago na kuuza hivyo kujilipia karo ya shule na matumizi ya kila siku.

Brian Ochieng na Brian Kiptoo wanasomea kozi za Uhandisi na Teknolojia ya Ujenzi mtawalia. Wawili hao, ambao pia wamelelewa katika kaunti mbili tofauti, walikiri kudhamini sanaa kutoka utotoni.

Ochieng alizaliwa na kulelewa katika Kaunti ya Kisumu. Alisema kuwa alipenda kuchora na kufinyanga udongo tangu utotoni. Ochieng alitoa kumbukumbu za awali ambapo wazazi wake walimkemea vikali alipokuwa akichora na kufinyanaga udongo, wakisema ni kupoteza wakati.

“Nakumbuka wazazi wangu hawakunipa wakati mzuri wa kuchora na kufinya udongo nikiwa mdogo. Walinikatisha tamaa kabisa lakini niliendelea kuchora kisirisiri kwa sababu nilipenda kuchora,” alisema.

Ochieng, mwanafunzi wa mwaka wa tatu, ambaye anasomea Uhandisi, anasema tabia ya kuchora haikukoma hata baada ya kujiunga na taasisi ya mafunzo ya RVIST.

rian Ochieng (kushoto) na Brian Kiptoo wakionyesha kazi yao ya sanaa katika taasisi ya ufundi ya Rift Valley Institute of Science and Technology(RVIST) Nakuru.Wawili hawa hupata faida ya kati ya Sh25,000 na Sh30,000 kila mwezi kutokana na sanaa. PICHA/ RICHARD MAOSI

Kwa upande mwingine, Kiptoo ambaye alilelewa katika Kaunti ya Baringo, anasema alipenda sanaa bila shauku na kutokana na hilo alichagua kufanya kozi ya Teknolojia ya Ujenzi katika taasisi ya mafunzo ya RVIST. Yeye pia anaweza kukumbuka upinzani alioupata akichora shuleni. “[Akicheka] Nilikuwa nachora tu darasani badala ya kusoma kama wengine. Nilikuwa nikitazama marafiki wangu na kuwachora wakiwa wanasoma,” anasema.

Wawili hawa wameshiriki pamoja kwa hafla nyingi sana mpaka mwishowe wakawa marafiki wa kufa kuzikana. Wawili hawa hapana shaka kuwa wana talanta za kipekee za kwenye Nyanja ya usanii jambo ambalo liliwafanya kufikirai njia mwafaka ya kutumia talanta zao.

“Niligundua kuwa rafiki yangu [Ochieng] ana talanta katika sanaa na aliipenda jinsi nilivyoipenda sanaa. Kwa hivyo sisi wawili tulikuwa na tabia sawa; tulidhamini sanaa. Ilitubidi tufikirie kuwa ni jinsi gani tunaweza kukuza uwezo wetu sehemu ya muda ule tupo kwenye mapumziko,” alisema Kiptoo.

Wawili hao walianza kuchonga kuni na kutengeneza vikorokoro mwaka 2017. Kwanza, Brian anaeleza kuwa walianza kwa kuchonga nembo ya taasisi ya RVIST kwa raha zao tu. Washika dau katika taasisi hiyo walivutiwa na nembo hiyo na wakajawa na tamaa ya kuinunua.

“Wakati shule ilipendezwa na kunua nembo ile, basi tulijawa na motisha. Tuliamua kuwekeza kikamilifu kiasi kidogo cha hela ambazo tulikuwa nazo, na ambazo zilitengewa matumizi ya kila siku ili kununa zana za kazi na vifaa,” alisema.

Kwa mfano, ili kutengeneza nembo unahitaji kifuniko cha kesi, na uzi. Wanasema kuwa kununua zana za kazi inaweza kugharimu takriban Shilingi 1,500.

Kulingana nao, nembo moja iliyoundwa vizuri inaweza kununuliwa kwa kiwango cha chini cha shilingi 3,500 hadi 5,000 kulingana na ukubwa wake.

“Vijana wanafaa kujaribu na kutumia uwezo wao vizuri. Watafute sehemu ambazo wanaweza kufanya vizuri na kutumia uwezo huo vizuri,” Kiptoo asema. Picha/ Richard Maosi

Brian Kiptoo na Brian Ochieng wanaweza kutengeneza faida ya kati ya shilingi 25,000 hadi 30,000 kwa mwezi mmoja na hivyo kuwa katika hali nzuri ya kujilipia karo ya shule na kugharamia matumizi ya kila siku.

Pengine unaweza kushangaa ni vipi wawili hawa wanaweza kujiuza kwa wateja wao. Wao hutumia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, ambapo wanajiundia mtangazo ya kibiashara na kuchapisha picha za bidhaa zao.

“Wakati wateja wetu wanavutiwa na bidhaa zetu, watupigia na kuitisha bidhaa ambayo wamependezwa nayo, tunajadili bei hadi tunaafikiana,”alisema Ochieng.

Wawili hawa sasa wanashukuru taasisi yao (RVIST) kwa kutambua na kuinua kazi yao kwa kununua bidhaa zao na pia kuwapa usafiri wa bila malipo pale wanapohitaji kusafiri.

Je, ni kwa njia gani wawili hawa wanaweza kumudu kusawazisha muda wa masomo na muda wa kuchonga? Walikiri kuwa muda wa masomo ni kizuizi katika kutengeneza vipande vya sanaa.Lakini wajaribu sana kusawazisha muda huo, ikizingatiwa kuwa ni wawili kwa idadi na wanafanya kozi tofauti hivyo wakati mmoja wao anahudhuria masomo, basi mwingine hushughulika kutengeneza ili kukidhi mahitaji ya wateja.

“Kiptoo anafanya kozi tofauti nami, na ratiba ya masomo ni tofauti. Kwa hivyo wakati niko darasani yeye hufanya kazi,” aliongeza Ochieng.

Kiptoo na Ochieng’ wanakariri kuwa kazi yao haikosi changamoto. Wanasema kuwa wakati mwingine katika harakati ya kuuza bidhaa zao, wanagundua kuwa watu wengine bado hawathamini kazi yao. Wengine hushusha bei ya bidhaa kimadharau tu.

Wawili hawa sasa wanatoa wito kwa serikali kuwajengea angalau kituo cha maonesho mjini Nakuru, mahali ambapo wanaweza kunyesha na kuuza bidhaa zao.

“Njia ya pekee serikali inaweza kupunguza ukosefu wa ajira ni kwa kunasa talanta changa zinazochipuka. Tunahitaji kituo cha sanaa mahali ambapo wasanii wanaweza kuonyesha kila ambacho wanaweza kufanya. Nadhani hii itasaidia wasanii kujiuza na kupanua biashara zao,” Kiptoo aliongeza.

Aidha wasanii hawa waliongeza kuwa sanaa hii imewasaidia kuzuia uvivu kwa sababu wanaweza kutenga muda wao vizuri kati ya kusoma darasani na kufanya kazi ya sanaa.

Waliwahimiza vijana na pia wasanii chipukizi kukoma kuzurura na badala yake kutumia muda wao wa ziada vyema ili kujenga maisha yao ya baadaye.

You can share this post!

Kenya kuvaana na UG bila Wanyama, Omollo na Okumu

SHANGAZI AKUJIBU: Nina kipusa akiguswa tu jamani anasalimu...

adminleo