• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
AKILIMALI: Ufugaji kuku njia ya lishe shuleni pamoja na pato

AKILIMALI: Ufugaji kuku njia ya lishe shuleni pamoja na pato

Na PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

KITU kisicho cha kawaida kilihusishwa katika uchaguzi wa viongozi wa baraza la wanafunzi katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Makueni mnamo Mei; nacho ni mayai.

Wengi wa wanafunzi waliowania nyadhifa mbalimbali za uongozi katika baraza hilo waliahidi kuhakikisha kuwa shule hiyo inaongeza idadi ya mayai ambayo shule hiyo huwapa wanafunzi kila wiki, kufikia angalau mawili kila wiki.

Walikuwa na sababu nzuri ya kutoa ahadi kama hiyo katika kampeni zao. Kisa na maana ni kuwa shule hiyo ina mradi wa ufugaji kuku ambao hutumiwa kuwafundisha wanafunzi mbinu za kisasa za ufugaji kuku wa mayai.

Ajabu ni kuwa mradi huo umenawiri kiasi kwamba huzalisha mayai mengi kukidhi mahitaji ya Shule hiyo ya hadhi ya kitaifa na hata kuuza masalio katika masoko ya karibu.

Shule hiyo ilinunua vifaranga 500 wa kuku wa kutaga mayai na kuyaweka katika kibanda kilichojengwa kwa mbao, mabati na nguo kuukuu.

Ajabu ni kwamba, wasimamizi wa Shule hiyo walisema kuwa shughuli hiyo iligharimu kiasi kisichozidi Sh2,000!

“Lengo kuu lilikuwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata vitamin muhimu inayotokana na mayai. Mradi huu pia unatumika kwa mafunzo ya utendaji kwa ajili ya walioteua somo la kilimo,” Mwalimu Mkuu Raphael Diwani akaambia jarida la Akilimali.

Naye Mwalimu wa Somo la Kilimo katika kidato cha nne, Bi Rosalina Kyalo anasema kuwa mradi huo huo huwasaidia wanafunzi kuelewa zaidi mafunzo ya kinadharia kuhusu faida za tasnia ya ufugaji kuku.

“Umesababisha wanafunzi wengi kuvutiwa zaidi na somo hili, jambo ambalo hurahisisha kazi yangu,” anaongeza.

Bw Paul Ndonye ambaye ni mfanyakazi mmoja wa shule hii aliyepata mafunzo kuhusu utunzaji kuku katika kampuni ya Kenchic ndiye husimamia mradi huu.

Wanafunzi hupewa kazi mbalimbali kwa zamu kama vile kulisha kuku, kukusanya mayai, kuyapanga mayai, kulingana na gredi mbali na kuwapa kuku dawa za kuangamiza magonjwa, dudu na minyoo, kufanya usafi katika kibanda cha kuku, miongoni mwa kazi nyinginezo.

Hii hufanyika angalau mara tatu kila wiki.

“Sisi hukusanya kreti 10 za mayai kila siku. Hata hivyo, shule huhitaji kreti 44 pekee za mayai kila wiki kwa matumizi ya wanafunzi. Lakini tumeng’amua kuwa wanafunzi sasa wanataka tuongeza idadi ya mayai tunayowapa kama sehemu ya lishe,” akasema Bw Diwani.

Mayai hayo pia huuziwa walimu na wafanyakazi wengine wa shule hiyo ambao huyanunua kwa wingi. Wao hununua kreti moja ya mayai kwa Sh300.

Shule hii pia huuza mayai haya katika duka kubwa la EdenMart Supermarket lililoko mjini Wote.

“Faida kutokana na mradi huu huelekezwa katika hazina ya shule ya kufadhili miradi midogomidogo yenye manufaa kwa wanafunzi.

Sehemu ya faida hiyo pia hutumiwa kuwanunulia zawadi wanafunzi na walimu waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za masomo na michezo mwishoni mwa mwaka,” akaongeza Bw Diwani.

Hata hivyo, mwalimu huyo mkuu alidinda kutueleza kiasi cha faidi ambayo mradi huo huzalisha mwaka mmoja akisema; “kimsingi, mradi huu umetuletea faidi kubwa kiasi kwamba baadhi ya wanafunzi sasa wamepatwa na ilhamu ya kuanzisha kazi hii watakapokamilisha masomo.”

Miradi yafaa

Mtaalam wa afya ya mifugo kutoka kampuni ya Unga Group Limited Marystellah Kanda anasema miradi ya ufugaji wa kuku inafaa kuanzishwa katika shule na vyuo kwa ajili ya kutolea mafunzo na kuleta mapato.

“Taasisi za mafunzo pia zina soko faafu kwa miradi ya ufugaji kuku. Na zinapaswa kuhakikisha kuwa zinagharimia lishe ya kutosha kudumisha miradi kama hii,” akasema.

Bi Kanda anaongeza pia kuwa ana tajriba pana katika fani ya utayarishaji lishe ya kuku,. Anasema kuwa lishe hubeba zaidi ya nusu ya gharama ya uzalisha.

“Wanaopanga kuanzisha mradi wa kuku pia wanapaswa kuwekeza katika ujenzi wa nyumba nzuri ya kuku ili kuzuia hasara kutokana na vifo vya ndege hao,” anashauri.

Na muhimu zaidi, anaongeza, ni kwamba mradi kama huo unapaswa kusimamiwa na wafanyakazi waliopokea mafunzo na wenye ari ya kazi hiyo.

You can share this post!

Wanahabari washajiishwa kuelewa ugatuzi kwa undani

Wakenya wanunua kwa wingi tiketi za VVIP kukaa pamoja na TD...

adminleo