• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
AKILIJIBU: Siku hizi samaki wangu hawali jinsi walivyokuwa hapo awali

AKILIJIBU: Siku hizi samaki wangu hawali jinsi walivyokuwa hapo awali

Na CHRIS ADUNGO

SWALI: Ninaitwa GIDEON SITIENEI kutoka Bomet. Nimekuwa nikiwafuga samaki kwa muda sasa. Hata hivyo, wamebadilisha sana mtindo wao wa kula katika siku za hivi karibuni. Je, sababu ni gani?

JIBU: Samaki kama viumbe-hai wengine huhitaji chakula ili waweze kukua na kuzaana kwa wingi. Samaki wapewe chakula angalau mara mbili kwa siku na muda unaopendekezwa ni saa tatu hadi saa nne asubuhi, na saa tisa hadi saa kumi jioni kwa sababu muda huo maji yanakuwa na hewa ya kutosha ambayo husaidia mmeng’enyo wa chakula kwa samaki.

Jambo jingine la kufanya kwenye ulishaji wa samaki ni kuwapa vyakula tofauti kutegemeana na silka ya aina ya samaki unaowafuga.

Kuna samaki wanaofaidika na vyakula vya nyama nyama kama vile kambare na sangara (hawa hawali pumba) na kuna samaki wengine kama sato wanaokula vyakula mchanganyiko wa nyama na mboga mboga na wapo wengine wanaokula vyakula vyenye asili ya mimea tu ambao kitaalamu wanajulikana kwa jina la Carps.

Kiwango cha hewa kikipungua sana majini, samaki hushindwa kula na kikizidi sana, maana yake ukijani unakuwa mwingi ndani ya maji hivyo samaki hushindwa kuona na kuleta athari kwenye ulaji wake wa chakula.

Kutokana na ukweli huo, inashauriwa kukagua kiwango cha hewa kilichopo kwenye maji angalau mara mbili kwa wiki.

Vifaa vya kufanyia ukaguzi vipo na vinapatikana katika maduka mbalimbali.

Pamoja na kuangalia kiwango hicho cha hewa, pia maji yanatakiwa yakaguliwe dhidi ya hewa chafu mfano kiasi cha tindikali au kiasi cha chumvi chumvi kilichopo kwenye maji, vilevile ukaguzi ufanywe dhidi ya taka ngumu kwa kutumia vipimo maalumu ambavyo vinaweza kugundua hewa chafu iliyomo majini, lakini yote kwa yote kilelezo cha ubora wa maji ni samaki mwenyewe, anachotakiwa mfugaji ni kuwa karibu na mifugo yake ili aweze kubaini kwa haraka mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika mifugo yake.

Ili kujua aina za vyakula vya samaki, ni lazima mfugaji ajue tabia za ulaji wa samaki. Tabia hizo zipo katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni samaki wanaokula nyama. Mfano ni pamoja na sangara na kambare. Kundi la pili ni samaki wanaokula mimea. Kundi la tatu ni samaki wanaokula vyakula mchanganyiko kama perege, sato na mwatiko (samaki wa maji ya chumvi). Kundi hili la samaki hutegemea zaidi upatikanaji wa vyakula vyenye asili ya nyama na mimea.

SWALI: Jina langu ni JUVENALIS MUUSYA kutoka Kitui. Nimeshangazwa na jinsi ambavyo kuku wangu wameanza kutaga mayai madogo. Je, ni nini kiini cha mabadiliko haya?

JIBU: Yapo mambo mengi yanayoweza kuchangia hali hii. Mojawapo ni umri wa kuku. Kuku wengi wanapoanza kutaga, huwa wanataga mayai madogo madogo lakini kadri siku zinavyozidi kwenda huongezeka ukubwa hivyo kama wana umri wa wiki 32 na kuendelea, hawawezi kuwa na tatizo hilo isipokuwa sababu zingine zinaweza kuchangia.

Vinasaba vya kuku, lishe, ugonjwa na msongo ni sababu nyingine. Kuna kuku wengine vinasaba vyao huwafanya kutaga mayai madogo tu na hivyo hata uwafanyeje, hawawezi kutaga mayai makubwa. Hivyo, hiyo ndio itakuwa hali yao ya kila siku. Msongo unaweza kusababishwa na joto kali ndani ya banda, ukosefu wa maji, ukosefu wa hewa ya kutosha pamoja kuzidi kwa mwanga ndani ya banda.

Vilevile wakati mwingine, msongo huweza kusababishwa na wanyama wakali kuingia bandani.

Mara nyingi kuku wenye wiki zaidi ya 32 wakikosa protini na chumvi ya kutosha husababisha kutaga mayai madogo. Pia inashauriwa sana kuhakikisha unabadili chakula mapema kutoka hatua moja ya ukuaji kwani nayo inaonekana kuwa ina mchango katika utagaji wa mayai madogo. Pia hakikisha kuku wako wanapata chakula wanachostahili pamoja na maji kwa siku.

Magonjwa kama vile ya minyoo na ‘egg dropping syndrome’ yanaweza kusababisha kushuka kwa utagaji na wakati mwingine kutaga mayai madogo madogo. Hakikisha kuku wako wanapata dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.

SWALI: Jina langu ni BONIFACE SULULU kutoka Mt Elgon. Nimeanza kujishughulisha na ufugaji wa nyuki majuzi. Naomba kujifunza zaidi kuhusu mbinu mwafaka za kutengeza mizinga kwa ajili ya ufugaji huu.

JIBU: Mizinga ya nyuki ni nyumba au makazi ya nyuki ya asili (matundu ya miti na mapango) au yaliyotengenezwa. Matumizi ya mizinga ni moja katika hatua muhimu za usimamizi na maendeleo katika kusimamia shughuli za ufugaji nyuki. Ili kuhifadhi mazingira, inashauriwa wafugaji wa nyuki watengeneze mizinga sahihi na ya gharama nafuu itakayokidhi mahitaji yao bila ya kuharibu mazingira.

Mahitaji hayo ni kuwa na mizinga mikubwa itakayowapatia mazao mengi zaidi. Mizinga huwekwa mahali ambapo wafugaji nyuki wanapataka wenyewe kulingana na taratibu za ufugaji nyuki na mpangilio wa matumizi endelevu ya ardhi kwenye eneo husika. Kuna aina kuu mbili za mizinga ya kisasa: Top Bar Hive (TTBH) yenye pande zilizosimama na inatumia viunzi 28.

Pia kuna Transitional Bee Hive ambao una viunzi 28 na kifuniko cha kufunika sanduku la chini yake.

Mizinga hii ya biashara ina masanduku mawili yanayolingana, kila sanduku likiwa na viunzi. Utengenezaji wa mzinga wa biashara hautofautiani sana na ule wa mzinga wa kati. Tofauti inakuwa tu kwenye vipimo. Mbao zinazotumika ni za unene na upana uleule.

Mzinga huu hubebea viunzi 13 na mchi wa juu wa kiunzi ni wa urefu ule ule inchi 19. Ukubwa wa mzinga huo hubadilika kwa kuongeza sanduku moja juu ya jingine. Sanduku la chini huwa ni la kukuzia nyuki wadogo na ndimo mnamoishi malkia.

Sanduku lolote linalowekwa juu ya sanduku la kukuzia nyuki wadogo huwa ni la kuhifadhia asali. Juu ya sanduku la kukuzia nyuki wadogo, huwekwa chombo kinachoit- wa kitenga malkia ili kumzuia malkia asitage mayai au kukuzia nyuki wadogo humo. Kwa sababu masanduku ya mzinga huu ni madogo, kifuniko chake huwa ni kimoja tu.

Katika utengenezaji wa TBH, lazima uzingatie vipimo thabiti vya mchi. Mchi lazima uwe na upana wa milimita 32 kamili ili kuwezesha nyuki kujenga masega ambayo yatakuwa na 32mm au 33mm kutoka katikati ya sega moja hadi katikati ya sega jingine jirani au linalopakana nalo.

Mpangilio huu huacha nafasi ya 8mm au 9mm kati ya nyuso za masega yanayopakana (yaliyokaa sambamba), ilimradi nyuki wawili wanaweza kupishana kwa kugeukiana migongo kwenye nafasi hiyo.

Mzinga huu una uwezo wa kuzalisha hadi lita 20 za asali (sawa sawa na kilo 30) kwa msimu mmoja. Gharama yake si kubwa sana. Miongoni mwa sifa za mzinga ya masanduku ni kwamba lazima uwe mkubwa kutosheleza mahitaji ya kupanuka haraka kwa kiota cha nyuki wa Afrika; Uwezo wa kuzalisha hadi lita 20 za asali (sawa sawa na kilo 30) kwa msimu mmoja.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Niliacha mume wangu, nikashikana na...

AKILIMALI: Atia fora katika kilimo cha nyanya Vihiga

adminleo