Habari Mseto

Mabalozi 11 waunga mkono azma ya Kenya kushinda kiti katika UNSC

September 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA na PSCU

JUHUDI za Kenya za kutaka kuwa mwanachana asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilipigwa jeki Jumanne wakati mabalozi wapya walipomhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kuwa nchi zao zitaiunga mkono Kenya kufikia azma hiyo.

Mabalozi wapya 11 walitoa ahadi hiyo ya kuiunga mkono Kenya wakati wa uchaguzi utakaofanyika Juni 2020 walipowasilisha vitambulisho vyao kwa Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Miongoni mwa mabalozi hao wapya ni: Balozi Jane Marriot wa Uingereza anayechukua nafasi ya Balozi Nic Hailey ambaye muda wake wa kuhudumu humu nchini umekamilika.

Balozi mwingine mpya aliyewasilisha vitambulisho vyake kwa Rais Kenyatta alikuwa Simon Mordue wa Muungano wa Ulaya (EU) anayechukua nafasi ya Balozi Antonio Stefan Dejak aliyeondoka.

Mabalozi wengine waliowasilisha vitambulisho vyao kwa Rais ni pamoja na; Dimitrios Zavoritis wa Ugiriki, Winpeg Moyo (Zimbabwe), Saqtain Syedah (Pakistan) na Martin Klepetko wa Jamhuri ya Czech.

Rais Kenyatta pia alipokea vitambulisho kutoka kwa mabalozi Oded Joseph wa Israeli na Jean Bosco Barege (Burundi) pamoja na mabalozi Toba Sebade (Togo), Sulayman Aliu wa (Gambia) na Hermann Immongault (Gabon) ambao watawakilisha mataifa yao bila kuwa na makazi humu nchini.

Balozi wa Ugiriki alisema nchi yake itaiunga mkono Kenya katika juhudi zake za kuwa mwanachama wa Baraza la UNSC huku akaiomba Kenya iiunge mkono nchi yake itakapogombea nafasi ya mwanachana asiye wa kudumu wa baraza hilo ifikapo mwaka wa 2024.

“Siwezi kutamatisha hotuba yangu Mheshimiwa Rais kabla sijaishukuru Kenya kwa kuunga mkono juhudi za nchi yangu ya Ugiriki za kugombea nafasi ya mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia moyo wa lipa wema kwa wema ,” akasema Balozi Zavoritis.

Balozi wa Zimbabwe, Winpeg Moyo, alisema taifa lake linaiunga mkono Kenya huku akielezea matumaini kwamba Kenya itashinda.

“Tafadhali pokea pongezi zangu na za Serikali yangu kufuatia kuidhinishwa kwa Kenya na Umoja wa Afrika (AU) kugombea nafasi ya baraza la UNSC.

Zimbabwe inaunga mkono juhudi hizo na inaamini Kenya itashinda uchaguzi huo huko New York,” akasema Balozi huyo wa Zimbabwe.

Mabalozi wa kutoka wanachama wa EU, kama vile, Uingereza, Israel, Pakistan, Togo, Burundi, Jamhuri ya Czech, Gabon na Gambia walisema Kenya ni mshirika muhimu kwa maslahi ya nchi zao na kwamba wataendelea kuunga mkono maslahi ya kiusalama ya Kenya.

Ushirikiano thabiti

Balozi mpya wa Uingereza alisema atafanya kazi kuleta ushirikiano thabiti na wenye manufaa kwa nchi hizi mbili katika masuala ya usalama na ulinzi hasa katika kukabiliana na ugaidi.

“Pia ningependa kutoa heshima zetu kwa kujitolea kwa vikosi vyenu vya usalama na ulinzi na viongozi wenu wa jamii kwa kupigana na ugaidi,” akasema Balozi Marriot.

Bi Marriot alisema Kenya na Uingereza “zinasimama imara kama nchi mbili za kisasa na zenye ukakamavu, na muhimu kwa ufanisi wa kanda zao na zenye majukumu muhimu katika Jumuiya ya Madola na katika kuunga mkono mfumo wa kimataifa wa utawala wa kisheria”.

Alisema Uingereza imejitolea kuunga mkono Ajenda Kuu Nne za Maendeleo akiongeza kwamba Kongamano la Uekezaji la Afrika la mwaka wa 2020 litakaloandaliwa jijini London linapiga jeki zaidi ajenda ya maendeleo ya Afrika na kubuni mazingira bora ya uwekezaji.

Kwa upande wake, balozi huyo wa EU alisema mataifa ya Uropa yanaichukulia Kenya kuwa yenye uwezo wa kiuchumi na kisiasa kufanya maamuzi makubwa kwa uthabiti wa eneo.

Alisema jitihada za Kenya kwa uthabiti wa eneo unadhihirika kutokana na mchango wake kwa kikosi cha AMISOM na kuwapa hifadhi wakimbizi zaidi ya 475,000.

“Uongozi wa sasa na ule ujao wa Muungano wa Ulaya unafahamu ukweli kwamba Kenya thabiti inayostawi ambayo inadumisha maadili yake ya kidemokrasia na uhuru wa kutoa maoni — jinsi ambavyo imekuwa ikipania kufanya chini ya uongozi wako — sio tu kwa maslahi ya Kenya lakini zaidi kwa maslahi ya Muungano wa Ulaya na raia wake,” akasema Balozi Mordue.

Rais Kenyatta aliwakaribisha mabalozi hao wapya jijini Nairobi na akawashauri kufanya kazi kwa karibu na serikali yake kwa manufaa ya Kenya na mataifa wanayowakilisha.

Aliwahakikishia mabalozi hao wapya usaidizi wake kamili wanapoanza kutekeleza majukumu yao hapa nchini akisema anatarajia kufanya kazi na kila mmoja wao kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na mataifa yao mbali mbali.