Raila mbioni kurai jamii ya Abagusii kukubali BBI
Na RUTH MBULA
KINARA wa ODM Raila Odinga analenga kuendeleza udhibiti wake wa kisiasa katika eneo la Gusii, huku akionekana kuwarai viongozi wa jamii hiyo kuunga mkono Jopokazi la Maridhiano (BBI) na kura ya maamuzi anayoipigia debe.
Kama njia ya kuhakikisha kwamba eneo hilo linarindima ngoma ya BBI na kura ya maoni, Bw Odinga Jumatano alikutana na viongozi wa jamii ya Abagusii afisini mwake Capitol Hill jijini Nairobi.
Ujumbe uliokutana na Bw Odinga uliongozwa na magavana James Ongwae wa Kisii na John Nyangarama wa Nyamira ambao ni wandani wake wa karibu wa kisiasa. Wengine waliohudhuria ni Seneta James Ongwae, Mbunge Mwakilishi wa Kike Janet Ong’era na wabunge Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini), Jimmy Angweny (Kitutu Chache Kaskazini), Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi) na Simba Arati (Dagoretti Kaskazini).
Duru ziliarifu kwamba magavana hao wawili ambao walichaguliwa kwa tiketi ya ODM, watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba wakazi wanakumbatia mapendekezo ya ripoti ya BBI ambayo inaendelea kutayarishwa na jopokazi lililoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Magavana hao wawili watakuwa na kibarua kigumu kuzima ufuasi wowote kwa Naibu Rais William Ruto ambaye anajivunia uungwaji mkono wa wabunge wengi wa jamii ya Abagusii pamoja na Naibu Gavana Joash Maang’i.
Taifa Leo ilifahamishwa kwamba Bw Odinga aliwashawishi viongozi hao kuungano mkono maridhiano kati yake na Rais Kenyatta maarufu kama ‘Handshake’ pamoja na nguzo nne za utawala wa Jubilee.
Walipofikiwa na Taifa Leo, magavana hao wawili pamoja na Bw Onyonka walikataa kutoa maelezo kuhusu mkutano huo wakisema tu ulikuwa wenye manufaa mno kwa Abagusii.
“Bw Odinga amekuwa akikutana na viongozi kutoka pembe zote nchini. Huwa hatuna shida kujadili masuala yetu na Bw Odinga kwa sababu yeye ni jirani yetu hapa. Sisi ndio tumenufaika pakubwa na ‘handisheki’ kwa sababu bidhaa zetu nyingi huuzwa eneo la Luo Nyanza,” akasema Bw Onyonka ambaye alishikilia kwamba Waziri huyo mkuu wa zamani ana historia ndefu na jamii ya Abagusii.
Bw Odinga alikuwa gunge wa kisiasa eneo la Gusii lakini uungwaji mkono wake uliyeyuka kidogo katika uchaguzi mkuu uliopita wapigakura walipochagua wabunge kutoka vyama vingine ila viti vya Ugavana, Useneta na Mwakilishi wa Kike vyote vikatwaliwa na ODM.
Hata hivyo, umaarufu wa Bw Odinga unaonekana kurejea kama zamani kutokana na uhusiano imara kati yake na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ambaye alipigia Jubilee kampeni kali na hata kuiwezesha kushinda viti viwili vya ubunge Nyaribari Chache na Kitutu Chache Kaskazini.
Ingawa baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakimrai kumuunga Dkt Matiang’i kuwania kiti cha Urais 2022, Bw Onyonka alithibitisha suala hilo halikujadiliwa kwenye mkutano wao na Bw Odinga.