• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Dereva anaswa kwa kukiuka sheria za usafirishaji viazi

Dereva anaswa kwa kukiuka sheria za usafirishaji viazi

Na WAIKWA MAINA

POLISI katika Kaunti ya Nyandarua wamenasa lori moja na dereva wake kwa kukiuka sheria kuhusu usafirishaji wa viazi.

Polisi hao walishirikiana na maafisa wa kaunti kutoka kitengo cha kilimo.

Mkurugenzi wa Kilimo katika kaunti hiyo, Bw Joseph Wathinja, alisema lori hilo lilinaswa mnamo Jumatano usiku na kundi maalum lililotumwa kuhakikisha kuwa sheria hiyo inazingatiwa.

Kulingana na sheria hiyo, viazi havipaswi kupakiwa kwa gunia linalozidi uzani wa kilo 50.

“Tulinasa lori hilo Jumatano usiku. Dereva na makanga wake wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kwa Haraka katika eneobunge la Kinangop. Dereva huyo alikuwa amebeba kiwango ambacho hakijaruhusiwa,” akasema Bw Wathinja.

Baada ya uchunguzi wao, ilibainika kuwa magunia hayo yalikuwa yenye uzani wa kati ya kilo 75 na 85. Magunia hayo vile vile hayakuwa yametimiza viwango ambavyo vinahitajika ili kusafirishwa. Lori hilo lilikuwa likielekea jijini Nairobi wakati liliponaswa.

“Tutaendelea na operesheni yetu ili kuhakikisha kuwa wasafirishaji wote wamezingatia sheria hiyo. Tunafurahi sana kwani wakulima wameanza kutuunga mkono. Ni operesheni ambayo imeanza kuzaa matunda,” akasema Bw Wathinja.

You can share this post!

Ripoti yafichua dawa za Sh15 milioni zimeharibikia...

Wizara ya Afya yaanza kutoa chanjo ya Hepatitis B kwa wakazi

adminleo