• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
Jinsi Rais alivyowapelekea wanamuziki ‘minofu’ mazishini

Jinsi Rais alivyowapelekea wanamuziki ‘minofu’ mazishini

Na MWANGI MUIRURI

BAADA ya kulemewa kujipanga ili wazuru Ikulu kula nyama choma ya mbuzi walioahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Oktoba 11, 2018, wanamuziki wa Mlima Kenya sasa inaonekana watatimiziwa waliyokuwa wakadai Ikulu bila shibe ya huyo mbuzi.

Kukumbusha tu kidogo, Rais Kenyatta akihudhuria na kuhutubia hafla ya mazishi ya msanii maarufu, Joseph Kamaru wa Wanjiru katika Kaunti ya Murang’a, aliwapa mwaliko wanamuziki hao hadi Ikulu akawachinjie mbuzi.

Mazishi hayo yakiwa siku ya Alhamisi, Rais aliwaalika Jumatano iliyokuwa inafuata ya Oktoba 16.

Mwanamuziki Ben Githae ambaye ni mwandani wa Rais na ambaye ndiye alitunga ule wimbo wa kampeni za Jubilee 2017 unaofahamika kama ‘Uhuru-Ruto Tano Tena’ anasema kuwa mambo yalianza kuharibika nukta moja tu baada ya Rais kutoa mwaliko huo.

“Hata kabla ya tumzike Kamaru, kuna wasanii waliokuwa katika mazishi hayo ambao waliondoka ghafla baada ya Rais kutoa mwaliko huo. Wengine waliokuwa wakifuatilia mazishi hayo kupitia runinga walianza mikakati ya kujipanga kuhudhuria mwaliko huo. Kabla ya muda wa saa 10 kuisha, kulikuwa na makundi 10 ya WhatsApp ambayo yalikuwa yameundwa, yote yakipanga mkutano huo wa Rais,” asema.

Anasema kuwa kuliandaliwa zaidi ya mikutano 12 ndani ya muda wa saa 12, yote ya usiku wa manane na ambapo mada katika mikutano hiyo yote ilikuwa jinsi ya kuhudhuria mkutano huo wa Ikulu wa kula mbuzi.

Na ikaishia kuwa hawakuhudhuria Ikulu na hawakula yule mbuzi wa Rais.

Lakini mwaka haukuisha kabla ya kutokea kifo cha msanii mwingine maarufu wa eneo hilo na ambaye alimtoa Rais Kenyatta kutoka Ikulu hadi katika Kaunti ya Murang’a kumzika.

Mwanamuziki huyo ni John De’ Mathew ambaye aliaga dunia Agosti 18 katika barabara kuu ya Thika alipokuwa akielekea nyumbani kwake. Gari lake liligonga upande wa nyuma wa lori lililokuwa katika safari ya kuelekea Sagana.

De’ Mathew akaaga dunia, akiwa mwenyekiti wa wanamuziki hao wa Mlima Kenya na katika mazishi yake, ikizingatiwa kuwa katika uhai wake alikuwa rafiki wa dhati wa Rais na Naibu wake, Dkt William Ruto, wanamuziki wale wale waliolemewa kujipanga wafike ikulu kula mbuzi wakawa wameungana katika maombolezi ya De’ Mathew na wakawa katika jukwaa moja na Rais.

Wakati huu, Rais aliwakejeli akiwaambia: “Ninyi mnajua sikuwa na shida na nyinyi na huwa nawajali sana lakini niliwaitia mbuzi na mnajua mambo yaliishia namna gani na ninyi ndio mlifeli.”

Hata hivyo, Rais hakuthubutu kuwapa mtihani mwingine tena wa kuwashinikiza wawe na umoja na uwiano wa kuafikia misaada kama jamii moja, wala sio katika migawanyiko.

Badala ya kuwaalika Ikulu tena, akawatangazia kuhusu sera ambazo serikali yake iko mbioni kuzitekeleza kuwafaa wanamuziki, sera ambazo ikiwa zitatekelezwa, bila shaka wanamuziki hao watapata mwamko mpya katika safu ya pato.

Rais aliwaahidi kuwa ameamrisha Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia (ICT) kutwaa majukumu ya yanayohusu hatimiliki, akisema kuwa kwa sasa iko katika afisi ya mkuu wa sheria (AG) na ambapo hakuna uwiano wa bongo za uwakili zilizo ndani ya afisi hiyo na muziki ambao huchezwa sana katika safu za teknolojia za mawasiliano.

Wanamuziki walionekana kutabasamu, Rais akiendelea mbele kutoa amri kwa waziri wa ICT Joe Mucheru aliyekuwa amesimama wima kupokezwa amri hizo, ahakikishe kuwa hakuna leseni ya biashara ambayo hutumia muziki wa wasanii itaidhinishwa upya kabla ya kukaguliwa na kubainika kuwa biashara hiyo imelipia utumizi wa huo muziki.

Watakaoathirika zaidi katika amri hii ni pamoja na vyombo vya habari vinavyotangaza kwa njia za kieletroniki pamoja na mikahawa mikuu na maeneo husika ya burudani sambamba na makampuni ya kutoa huduma za simu.

Aidha, Rais aliamuru Mucheru ahakikishe ametoa vifaa vya Sh10 milioni katika studio mpya itakayozinduliwa katika kaunti ndogo ya Gatanga; Gatanga ambayo ni ngome ya vipawa tele vya muziki katika Kaunti hiyo ya Murang’a. Studio hiyo ikiwekwa katika mtaa wa Kirwara.

Rais alitangaza kuwa atasaidiana na wanamuziki hao kwa hali na mali, akiwaahidi mchango wake na wa Naibu Rais wa kuwasaidia wanamuziki hao kuzindua uwekezaji wa nyumba za kibiashara katika mtaa wa Kenol ulioko Murang’a ambapo kupitia ushirika wao wa uanamuziki ujilakanao kama Tamco, wamejinunulia kiwanja kwa gharama ya Sh10 milioni na ujenzi wanaonuia kutekeleza ukitathminiwa kuwa wa Sh80 milioni.

Kwa mujibu wa Naibu wa Mwenyekiti wa Tamco, Epha Maina, “huyo ndiye mbuzi ambaye tulikuwa tukamle Ikulu.”

“Rais kwa busara yake amemchinja na akatuletea minofu yake hapa nje na ambapo kauli hizo zake zikitekelezwa, basi nakuahidi msanii atakayekiwa na uzani wa chini zaidi miongoni mwetu katika ushirika wa tamco atakuwa na kilo 100 ongeza bila kupunguza kwa kuwa tutakuwa na pesa sabuni ya roho mikobani mwetu,” akasema Bw Maina.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Uislamu ni dini ambayo inahimiza...

KIPWANI: Achanganya beats kunasa mashabiki

adminleo