• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wakazi Kambiti walalamika kuhusu ubovu wa barabara

Wakazi Kambiti walalamika kuhusu ubovu wa barabara

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa Kambiti, Kaunti ya Murang’a wamelalamikia ongezeko la visa vya ajali eneo hilo.

Barabara kuu inayounganisha jiji la Nairobi na Embu na Nyeri, imepitia Kambiti.

Kulingana na wakazi, watoto wa shule ndio wameathirika pakubwa, ikizingatiwa kuwa hakuna matuta yaliyowekwa eneo hilo.

“Ukitazama kuanzia Kakuzi hadi hapa mtaa wa Kambiti, hakuna matuta ya kudhibiti kasi ya magari. Tumepoteza watoto wengi sana, hasa wanapoenda shuleni asubuhi na jioni wanapotoka,” John Mwaura mkazi, akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano katika eneo hilo.

Shule ya msingi ya Mathengeta na ya upili ya Kambiti ziko mita chache kutoka sehemu ya barabara inayotajwa kuwa hatari.

Mbali na wanafunzi, wahudumu wa bodaboda hasa wanapovuka inadaiwa huishia kugongwa dafrau na magari.

Mtaa wa Kambiti unaendeshwa shughuli mbalimbali za biashara, na Taifa Leo ilipozuru eneo hilo ilithibitisha barabara inayopitia humo haina matuta.

Isitoshe, eneo hilo halijawekwa mabango ya barabara hususan kutahadharisha wenye magari sehemu wanayovukia wanafunzi.

Maafa yanaendelea kushuhudiwa licha ya wanakijiji kueleza kilio chao kwa serikali kupitia viongozi.

“Si mara moja au mbili tumeandamana hapa tukiagiza tuwekewe matuta, kivukio au daraja, kufuatia watoto na watu wazima kugongwa na magari. Miezi kadhaa iliyopita waziri wa barabara na uchukuzi James Macharia alikuja na kuahidi matuta yatawekwa haraka iwezekanavyo, kufikia sasa hatujayaona,” akaeleza Bw Mwaura.

Majira ya jioni na usiku yanatajwa kama muda ambao maafa yanashuhudiwa zaidi.

“Kila Jumapili jioni hatukosi kupoteza mtu mmoja,” akasema mwanakijiji aliyeomba jina lake lisichapishwe.

La kushangaza, licha ya mtaa huo kuonekana wenye shughuli mbalimbali, madereva huendesha magari kwa mwendo wa kasi.

Tulipozuru mwendo wa jioni, baadhi ya watoto wa shule walionekana kukabidiliwa na wakati mgumu kuvuka barabara.

You can share this post!

ULIMBWENDE: Majani ya giligilani katika urembo

Sonko asema yuko tayari kujiuzulu ili achunguzwe

adminleo