Sonko akosa tena kutaja naibu gavana
CHARLES WASONGA na HILLARY KIMUYU
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko, kwa mara nyingine, Ijumaa alikosa kutimiza ahadi yake ya kumtaja naibu wake.
Mnamo Alhamisi gavana huyo aliwaahidi wakazi wa kaunti ya Nairobi kwamba angependekeza jina la atakayekuwa naibu gavana na kuiwasilisha kwa bunge la kaunti ya Nairobi.
Vile vile, alisema kuwa yu tayari kujiondoa afisini kwa muda endapo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji atapendekeza afunguliwe mashtaka.
Bw Sonko anakabiliwa na sakata ya kuhusu utoaji zabuni ya uzoaji taka ambapo inadaiwa kuwa alipokea hongo kutoka kwa baadhi ya kampuni ili azisaidie kupata kandarasi hizo za thamani ya zaidi ya Sh300 milioni.
Isitoshe, juzi alihojiwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) kwa tuhuma za kukosa kuwasilisha ushuru wa Sh4.5 bilioni wa asasi hiyo tangu alipoingia mamlakani.
Wadhifa wa Naibu Gavana wa Nairobi umesalia wazi kwa zaidi ya miezi 21 tangu Januari 2018 wakati Polycarp Igathe alijiuzulu akisema gavana Sonko alikuwa akiingilia utendakazi wake.
Kuteua mwanamke
Kwenye mahojiano na wanahabari hapo awali, Bw Sonko alisema kuwa atateua mwanamke kwa wadhifa huo.
Miezi sita baada ya kujiuzulu kwa Bw Igathe, Sonko alimpendekeza wakili na mwanaharakati Miguna Miguna kwa wadhifa huo lakini chaguo hilo likakatiliwa na Bunge la Kaunti ya Nairobi.
Madiwani wa Jubilee ambao ni wengi, wakiongozwa na Spika aliyesimamishwa kazi, Beatrice Elachi, lilidai kuwa Bw Miguna hakuwa mwanachama wa Jubilee na kwamba utata umegubika uraia wake.