• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
MWANASIASA NGANGARI: Joseph Otiende: mwalimu maafuru na mpiganiaji uhuru

MWANASIASA NGANGARI: Joseph Otiende: mwalimu maafuru na mpiganiaji uhuru

Na KEYB

JOSEPH D. Otiende alikuwa mwalimu, afisa wa utawala, mwanasiasa, mpiganiaji uhuru, mbunge na waziri na angali anahusika na uongozi katika jamii eneo la Magharibi nchini.

Akiwa na wengine, walijitolea kutoa huduma ambazo zilileta uhuru wa kisiasa na kutoa mchango uliojenga utaifa wa Kenya.

Alihudumu kama waziri wa wizara kadhaa katika serikali ya Rais Jomo Kenyatta; Elimu, Kilimo, Afya na Makao.

Alipoteza kiti cha eneobunge la Vihiga mwaka wa 1969 na hakugombea tena, akaamua kustaafu siasa alipokuwa akielekea kutimu umri wa miaka 50.

Kwenye mahojiano hivi majuzi, Otiende alisema jukumu alilotekeleza maishani lilianza kutoka utotoni.

Anasema alipoanza masomo miaka ya 1920: “Baba yangu alikuwa mwalimu na mhubiri. Alitambua elimu na manufaa yake hata enzi hizo ambazo umuhimu wake haukuwa umekumbatiwa na watu wengi.”

Otiende alizaliwa 1917 katika kijiji cha Akelo village, Vihiga, ambako anaishi hadi wakati huu.

Anakumbuka kuwa baba yake hakuhakikisha alipata elimu mapema pekee, mbali alisomesha watoto wengine maeneo ya Maragoli, Kisumu na Maseno ambako alihubiri injili na kusisitiza elimu.

Kokote alikotumwa, alikuwa akienda na familia yake. Hii ilimuathiri sana Otiende hasa kwa kujifunza lugha na tamaduni za jamii nyingine mbali na Maragoli.

Nyumbani na Kanisani

Kabla ya kujiunga na shule yake ya kwanza, Butere Normal School, alikuwa amefunzwa kuwa na hekima yote hutoka kwa Bibilia. Hii ni kwa sababu baba yake alikuwa akisoma “kitabu hicho kikubwa” nyumbani na kanisani.

Wakati wamishenari wa Church Missionary Society walipofungua shule ya Maseno mwaka wa 1926 Otiende alikuwa mmoja wa wanafunzi wa kwanza. Alikuwa na Oginga Odinga na Askofu Mkuu wa Kanisa la Angilikana Festus Olang katika darasa moja.

Anakumbuka: “Hata kama tulikuwa wadongo, Jaramogi na mimi tulikuwa tukijadili siasa na tulikuwa tukilenga uongozi siku za baadaye.”

Olang alikuwa akitamani dini tangu akiwa na umri mdogo. Kwa sababu walikuwa wakilala shuleni, wanafunzi wa kwanza walishirikiana kwa karibu kama ndugu.

Otiende anasema kwamba Maseno ilikuwa na nafasi spesheli katika maisha kwa sababu wamishenari wazungu ambao walikuwa walimu waliwafunza misingi thabiti ya kidini na elimu ya kawaida.

Alipojiunga na shule ya Maseno, desturi nyingine tofauti na ya jamii yake aliyojifunza ilikuwa ya Waluo

Wakati huo, serikali ya wakoloni ilikuwa ikiendesha sera iliyofanana na ubaguzi wa rangi. Jamii tofauti hazikuruhusiwa kutangamana ili zisishirikiane kupinga wanyanyasaji wao.

Ikiwa wavulana kutoka jamii za maeneo mengine yasiyokuwa magharibi mwa Kenya waliomfunza desturi tofauti na jamii yake, hali ilizidi 1930 alipojiunga na Alliance baada ya kufunzu vyema Maseno.

“Kwangu, kuvunja vizingiti vya kikabila kulichukua mwelekeo usioweza kugeuzwa nilipojiunga na Alliance,” akumbuka.

“Kwanza, safari kutoka alikozaliwa North Kavirondo, jina la eneo hilo wakati huo, hadi eneo la Kati ya Kenya, ilikuwa ya uvumbuzi kwa tineja aliyekuwa na umri wa miaka 13 mwaka wa 1930. Sio Waafrika wengi waliokuwa wamepata nafasi ya kutembea nje ya walikozaliwa.

Anasema: “Mtazamo wangu kuhusu ulimwengu ulipanuka sana katika miaka niliyokuwa Alliance. Nilikutana na wanafunzi kutoka maeneo mengine ya nchi na nikaanza kukubali Kenya ina makabila mengi.”

Alikuwa shule wakati mmoja na Jackson Angaine na James Gichuru, ambao baadaye alihudumu nao katika Baraza la Mawaziri. Alliance ilikuwa taasisi ya masomo ya upili kwa wachache waliochaguliwa, nafasi ambayo shule hiyo ilidumisha kwa miaka mingi hadi baada ya uhuru na shule nyingine kuanzishwa.

Otiende anakumbuka nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya darasa ambayo wamishenari walihakikisha imedumishwa katika shule hiyo.

“Ingawa ilichukuliwa kuwa elimu iliegemea sana mtazamo wa wazungu kuhusu ulimwengu, tulijua kwamba ilikuwa muhimu kukumbatia Uafrika. Kwa hivyo, tulisoma historia tuliyofunzwa na kuibadilisha kuhusu jamii zetu.”

“Ingawa tulikuwa tukifunzwa ili kugeuza jamii zetu zikumbatie mtindo wa maisha wa wazungu, tulifahamu vyema kuwa haki na uhuru wa Waafrika zilikuwa zikikadamizwa,” asema

Alipofuzu vyema Alliance alijiunga na chuo kikuu cha Makerere, Kampala ambako alifunzwa kuwaandaa viongozi wachache Waafrika kuchukua nafasi katika utawala wa kikoloni.

Sayansi ya siasa

Otiende alitaka kusomea udaktari, taaluma ambayo haikuwa ikifunzwa waafrika wengi kwa sababu hawakuruhusiwa kuisomea. Wengi walisomea ualimu, sayansi ya siasa, historia na sayansi ya kijamii.

Alisomea ualimu kwa sababu watu wa jamii yake walimtaka aweze kufunza watoto wao wapate elimu ya wazungu. Alijifunza utabibu baadaye kupitia njia tofauti.

“Ninapotazama nyuma, ninafikiri uamuzi wa jamii ulikuwa unafaa. Maarifa yangu yalihitajika sana kufunza watu na kupanua ufahamu wao kuliko kuwatibu,” asema. Anasema safari yake ya elimu ilisaidia kuyeyusha vizingiti vya kikabila Makerere, kitaifa na hata kijiografia.

“Hakuna aliyejali kabila la mwingine. Ni uhuru ulipokaribia na katika mwongo wa kwanza wa kujitawala ambapo uovu huu ulijikita katika jamii na ukawa saratani ambayo tulishindwa kuponya. Ninaomba siku moja nchi hii itarudia usawa wa kikabila ambao ulikuwa miaka ya hamsini na iliyotangulia. Makerere ilikuwa mahali ambapo tulikuwa tukisikia na kusoma. Ingawa tulifahamu kwamba kugawanywa kwa Afrika na mataifa ya kigeni kulitenga Kenya kutoka Uganda, safari yetu huko ilitufanya tubaini uhalisi wa utengano huo.”

Huko Makerere, lugha iliyozungumzwa Uganda ilifanana na yake ya Maragoli na hakusumbuka kuelewa yaliyonenwa.

Alikutana na wanafunzi kutoka Uganda na Tanzania ambao walikuwa na maono sawa na yake ya kutumia elimu kuimarisha vita vya kisiasa kutaka ukombozi.

“Mojawapo ya mambo niliyojifunza ni kwamba Waafrika walikabiliwa na matatizo sawa-utawala wa wazungu bila wao kupenda. Kulikuwa na hisia kali za uzalendo miongoni mwa wanafunzi kutoka mataifa yote ya Afrika Mashariki,” anasema na kuongeza kuwa midahalo ilihusu jinsi wanafunzi wangekomboa nchi zao.

Otiende alifuzu kutoka Makerere mwaka wa 1936. Mnamo 1937, akiwa na cheti na kuelewa siasa, alianza kufanya kazi katika shule ya Kaimosi Intermediate School, iliyoanzishwa na wamishenari wa Friends (Quakers) Church kama mmoja wa walimu wa kwanza Waafrika katika mfumo wa elimu uliokuwa na wazungu wengi.

Taasisi za mafunzo

Alikuwa mmoja wa waliofanya Kaimosi kuwa kituo cha elimu hadhi ambayo kimedumisha hadi wakati huu kikiwa na taasisi kadhaa za mafunzo, shule za msingi na upili. Alifunza watu wengi kutoka mikoa ya Magharibi na Nyanza waliopata elimu enzi hizo.

Haukupita muda mrefu nafasi ya kazi ilitokea katika shule ya upili ya Alliance alikosomea wakati Eliud Mathu, mmoja wa walimu wa kwanza Waafrika na ambaye walihudumu pamoja serikalini baadaye, alipopata ufadhili wa masomo ng’ambo.

Maafisa wa elimu wa kikoloni, walimchagua Otiende kuchukua nafasi ya Mathu. Otiende aliungana tena na Gichuru, waliyesoma darasa moja Alliance na Makerere na baadaye wakahudumu pamoja katika Baraza la Mawaziri.

Walifunza wanafunzi ambao baadaye walihudumu katika nyadhifa za juu serikalini na kufanya kazi nao katika baraza la mawaziri —Paul Ngei, Nathan Munoko, Njoroge Mungai na Julius Gikonyo Kiano.

“Ingawa walikuwa wanafunzi, tulishiriki midahalo ya wazi nao kuhusu hatima ya nchi na tukajenga uhusiano ambao ulidumu hadi wakati huu,” alisema. “Mipaka kati ya walimu Waafrika na wanafunzi wao ulikuwa mwembemba sana,” alisema.

Ni akiwa mwalimu Alliance ambapo maisha yake kama mwanasiasa yalianza kuchukua mwelekeo mpya. Alishiriki vitendo vya kisiasa kwa kuzingatia maadili ya kazi ya ualimu japo Edward Carey Francis, aliyekuwa mwalimu mkuu maarufu, hakuviruhusu.

“Ubaguzi wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kupendelewa kwa walimu wazungu na kudhulumiwa kwa wenzao Waafrika, kulituchochea kushiriki katika makundi yaliyolenga kuwafungua macho Waafrika,” anaeleza.

“Tulikuwa tumepata elimu ya wazungu na tulifahamu vyema kuwa ubaguzi haungetetewa kabisa. Pia tulifahamu kuwa serikali ya wakoloni ilikuwa ikikandamiza haki za Waafrika. Lazima tungechukua hatua kurekebisha hali.”

Walimu Wafrika na baadhi ya wanafunzi walieleza hasira zao kuhusu ubaguzi kwenye mijadala ya kisiasa.

Otiende anasema Alliance, ilikuwa mahali ambapo vita vya uhuru vilichukua mkondo wa kielimu. Anamtaja Mathu kama mmoja wa walimu Waafrika walioweka mikakati ya kukomboa Waafrika.

Kuteuliwa kwa Mathu kuwa Mwafrika wa kwanza katika Legco iliyokuwa ya wazungu pekee, ilikuwa hatua kubwa. Kulikuwa msingi kwa Otiende kuendelea na shughuli zake za kisiasa.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke

You can share this post!

DINI: Ukitaka kesho nzuri toka katika shimo la jana,...

Uhuru aahidi wapwani vinono

adminleo