SHINA LA UHAI: Changamoto za kulea mtoto aliye na mtindio wa ubongo
Na PAULINE ONGAJI
MZIGO wa matatizo ya kiakili miongoni mwa watoto katika familia nyingi hapa nchini huwa mzito kiasi cha wengi kushindwa kustahimili.
Ni masaibu ambayo familia ya James Maina Gacira, mkazi wa kijiji cha Githaraini, Kinangop Kaskazini, Kaunti ya Nyandarua inapitia.
Baaada ya kifo cha mkewe, Lydia Wangui, Novemba 2018 aliachiwa mzigo wa kuwalea watoto wanane, kati ya miaka 13 na 35. Lakini mzigo mkuu ulikuwa ule wa kuwashughulikia wanawe wawili wa mwisho; John Mwai, 17, na Daniel Wanjohi, 13, wanaokumbwa na maradhi ya Mtindio wa Ubongo (Cerebral Palsy).
Mwai amekuwa na hali hii tangu azaliwe.
Hawezi kutembea na badala yake anatambaa, na japo anaelewa kidogo kila anapozungumziwa, hawezi kutamka lolote na majibu yake hasa ni kwa ishara za uso, vile vile mlio anaotoa akiwa na furaha au anapokumbwa na maumivu.
Kwa upande mwingine, Wanjohi hana uwezo wa kutembea na lazima abebwe kila mahali. Hawezi kutamka lolote na mawasiliano yake pia ni kama ya nduguye.
Wawili hawa hawajawahi kwenda shuleni na wanamtegemea baba yao kwa kila kitu. Lazima awabebe kuwatoa nje kuota jua, awaoeshe, awalishe na hata awapeleke msalani. Kwa upande wa Wanjohi, hawezi hata kujigeuza akiwa kitandani, na sharti babake aamke usiku wa manane kumpindua.
“Mimi huamka saa kumi na mbili asubuhi, kisha nawaandalia kiamsha kinywa, nawaamsha, nafua nguo zao, kabla ya kwenda shambani saa nne asubuhi. Kisha narejea saa saba adhuhuri na kuwaandalia chakula cha mchana na baadaye chajio,” aeleza.
Ni suala ambalo limemlazimu Bw Gacira kutumia wakati wake mwingi nyumbani na hata kuacha kazi aliyokuwa akifanya kama mlinzi, ili kuwashughulikia kikamilifu.
Aidha, hawezi kuondoka nyumbani na kuwaacha kwa zaidi ya masaa mawili, na hilo limeathiri kazi yake kama mkulima, na kipato vilevile. Kutokana na haya, imemlazimu kutegemea wahisani ili kukidhi mahitaji yao.
“Mara nyingi nategemea majirani na wahisani kuniletea chakula ambapo kuna wakati napata mfuko wa unga na bidhaa zingine za matumizi kama vile nepi za kuwafunga,” asema.
Mtindio wa ubongo ni nini?
Ni tatizo la utandio wa ubongo linaloathiri sehemu inayohusika na misuli.
Mara nyingi husababisha misuli kuwa dhaifu au migumu na mwili kutetemeka hivyo mtoto kushindwa kutembea, kumeza mate, kuzungumza, kukumbwa na matatizo ya hisia, kuona na kusikia.
Pia humfanya mtoto ashindwe kuketi, kula, ugumu wa kuwaza au kufikiria, kifafa, kushindwa kupumua na kudhibiti mkojo na kinyesi.
Mara nyingi hali hii hutokana na ukuaji usio wa kawaida au uharibifu wa sehemu ya ubongo inayodhibiti mwendo, usawa na hali ya mkao kabla, wakati au baada ya kuzaliwa, hasa kati ya miaka mitatu na mitano ya kwanza ya mtoto. Uharibifu huu wa ubongo waweza kusababisha matatizo kama vile kuona, kusikia na kujifunza.
Hatari zinazoongeza uwezekano wa kukumbwa na mtindio wa ubongo
Kulingana na muungano wa madaktari wa watoto Amerika, (American Academy of paeditricians) kuna mambo kadha wa kadha yanayoweza kuchangia hali hii ikiwa ni pamoja na uzani mdogo wakati wa kuzaliwa au kuzaliwa kabla ya siku ya kujifungua.
Utafiti uliofanywa bara Ulaya na Australia, ulionyesha kwamba hali hii ilikithiri kwa kati ya asilimia 35.0 hadi 79.5 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa katika kipindi cha kati ya wiki 28 na 31 za ujauzito, ikilinganishwa na kati ya 1.1 hadi 1.7 kwa watoto 1,000 waliozaliwa katika kipindi cha wiki 37 au zaidi za ujauzito.
Pia, unasema kwamba kukatizwa kwa damu na kiwango cha oksijeni kwenye ubongo kwaweza kusababisha hali hii.
“Hapa yaweza kutokana na mama kukumbwa na uchungu wa uzazi wa muda mrefu pasipo kushughulikiwa, suala linalosababisha kiunga mwana (umbilical cord) kujifunga kwenye shingo la mtoto, na kuzuia ubongo kupata oksijeni ya kutosha na hivyo kusababisha uharibifu wa ubongo,” aeleza.
“Mbali na hayo, maambukizi kwenye kuta za mji wa mwana (chorioamnionitis) au maambukizi mengine (ya damu na homa) kwa mama wakati wa uchungu wa uzazi yanaweza ongeza hatari ya kukumbwa na maradhi haya,” aongeza.
Utafiti unaonyesha kwamba chorioamnionitis imeonekana kusababisha asilimia 12 ya hali hii miongoni mwa watoto waliozaliwa baada ya kukamilika kwa kipindi cha ujauzito, na asilimia 28 miongoni mwa watoto waliozaliwa kabla ya kukamilika kwa kipindi cha ujauzito.
Mbali na hayo, anasema kwamba kuna masuala mengine yanayosababisha hali hii ikiwa ni pamoja na majeraha ya ubongo wakati au baada ya kuzaliwa. “Pengine mtoto anaweza kuanguka na agongeshe kichwa sehemu ngumu na kusababisha majeraha ya ubongo. Aidha, hali hii yaweza kusababishwa iwapo mtoto atakumbwa na maradhi yanayoathiri ubongo kama vile Menengitis, na asipate matibabu kwa wakati unaofaa,” aongeza.
Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya Centers for Disease control and Prevention- CDC, nchini Amerika, kati ya 10% na 15% ya maradhi haya yalitokea mapema maishani mwa mtoto huku yakisababishwa na majeraha ya ubongo kutokana na ajali au maambukizi ya maradhi yanayoathiri ubongo kama vile Meningitis.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani-WHO, kila wakati watoto 1,000 wanaozaliwa katika mataifa yanayostawi, ikiwa ni pamoja na Kenya, wanne hukumbwa na mtindio wa ubongo.
Humu nchini, hakuna takwimu rasmi kuhusu maradhi haya, lakini kuna baadhi ya wataalamu wanaokadiria kwamba kati ya watoto 100 nchini, watatu hukumbwa na maradhi haya.
Hii ni idadi kubwa ikilinganishwa na nchi kama Amerika, ambapo takwimu zinaonyesha kwamba hali hii hutokea kwa mtoto mmoja kati ya 500 wanaozaliwa.
Miaka mitatu iliyopita, madaktari na wahudumu wengine wa Kiafya walionyesha wasiwasi kutokana na ongezeko la visa vya mtindio wa ubongo katika eneo la Naivasha.
Takwimu zilionyesha kwamba hali hii ndio ilisababisha ulemavu kwa wingi miongoni mwa watoto eneo hilo.
Kulingana na takwimu kutoka hospitali ya Naivasha Sub-County, watatu kati ya wagonjwa wanne waliokuwa wakipokea matibabu katika idara ya kusaidia waathiriwa kuweza kutumia viungo walivyo navyo (occupational therapy) walikumbwa na hali hii.
Kulingana na George Kakala, mwenyekiti wa shirika la Cerebral Palsy Society of Kenya (CPSK), ongezeko la visa hivi humu nchini hasa latokana na ulegevu wa wahudumu katika hospitali.
“Tafiti kadha ambazo tumefanya katika hospitali mbalimbali zimeonyesha kwamba hali hii imekithiri sana ambapo sababu kuu imeonekana kuwa kutelekezwa kwa akina mama wakati wa kujifungua,” aeleza.
Aidha, anasema tatizo hili humu nchini husababishwa na akina mama wasiohudhuria huduma za kliniki wakati wa ujauzito.
“Hapa inakuwa vigumu kwa wahudumu kukagua mkao wa mtoto akiwa tumboni, suala ambalo mara nyingi husababisha matatizo wakati wa kujifungua,” aeleza.
Anasisitiza kuwa hili ni tatizo ambalo laweza kukabiliwa humu nchini.
“Serikali inapaswa kuingilia kati na kuhakikisha kwamba idadi hii inapunguzwa vilivyo. Hii itafanikishwa kwa kuhakikisha kwamba mafunzo zaidi yanatolewa kwa wakunga na wahudumu wengine wa kiafya,” aongeza.
Anasema kwamba hatua zinapaswa kuchukuliwa kukabiliana na matapeli wanaotoa huduma ya kuzalisha watoto licha ya kwamba hawajahitimu kitaaluma.
“Ni tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa kwani kosa moja laweza kuharibu kabisa maisha ya mtu,” asema.
Nancy Njoroge, mwanzilishi wa Agape Special Center, kituo kinachotoa huduma za matibabu na masomo kwa watoto wanaokumbwa na mtindio wa ubongo, anasema kwamba mzigo wa kuwashughulikia watoto hawa ni mzito sana.
“Ni ghali sana kuwashughulikia watoto hawa na inachukua muda na rasilimali nyingi, suala linalotatiza walezi wao na kuwazuia kujihusisha na shughuli za kujitafutia riziki,” aeleza.
Kulingana na CDC, gharama ya matibabu kwa watoto wanaokumbwa na hali hii ni mara kumi zaidi ikilinganishwa na watoto ambao hawana mtindio wa ubongo wala matatizo ya kiakili.