MAZINGIRA NA SAYANSI: Moshi wa magari unaweza kusababisha upofu uzeeni
Na LEONARD ONYANGO
IKIWA unaishi au kufanya kazi katika maeneo yaliyo na moshi mwingi wa magari kama vile steji ya mabasi au barabara yenye msongamano wa magari, uko katika hatari maradufu ya kuwa kipofu uzeeni.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi nchini Taiwan unaonyesha kuwa moshi wa magari huharibu sehemu ya jicho ambayo husaidia watu kuona.
Watafiti hao wanasema kuwa watu wanaotumia barabara zilizo na msongamano mkubwa wa magari kama vile barabara kuu za Thika, Jogoo na Mombasa za jijini Nairobi, pia wako katika hatari ya kukosa kuona watakapotimiza umri wa miaka 50 na zaidi.
“Moshi wa magari huchangia kwa kiwango kikubwa kwa ugonjwa unaofahamika kama Age-Related Macular Degeneration (AMD) ambao husababisha watu wa umri mkubwa kupoteza uwezo wa kuona. Ikiwa watu wataepuka maeneo yaliyo na moshi mwingi wa magari, basi wataepuka maradhi hayo,” anasema Prof Suh-Hang Hank Juo, mmoja wa watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha China, nchini Taiwan.
“Unapofanya mazoezi asubuhi kando ya barabara iliyo na magari mengi, unajiletea shida ya macho,” akaongezea.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika jarida la Journal of Investigative Medicine, watafiti hao walichunguza watu 39,819.
Waligawa watu hao katika makundi manne kulingana na maeneo wanayoishi au maeneo wanayofanyia kazi.
Wanasayansi walikuwa wakiwafuatilia watu hao mara kwa mara kwa kipindi cha miaka 11.
Baada ya miaka 11, walibaini kuwa asilimia 84 ya waliokuwa wakiishi au kufanya kazi katika maeneo yaliyo na moshi mwingi wa magari, walikuwa na ugonjwa wa AMD unaosababisha macho kushindwa kuona.
Wanasayansi hao, hata hivyo, walikiri kuwa hawajui kemikali iliyoko ndani ya moshi unaotolewa na magari inayosababisha maradhi ya AMD.
Ugonjwa huu umekuwa ukihusishwa na uvutaji sigara. Watafiti hao wanaamini kuwa huenda moshi wa magari una madhara sawa na sigara kwa macho.
Moshi unaotolewa na magari umesheheni hewa hatari ya kaboni monoksaidi, nitrojeni oksaidi na kemikali nyinginezo. Kemikali zinazotolewa na dizeli zimethibitishwa kusababisha maradhi mbalimbali, ikiwemo kansa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa moshi wa magari huchangia asilimia 25 ya kansa ya mapafu. Moshi huo pia husababisha maradhi ya pumu(asthma).
Ripoti iliyotolewa Februari mwaka huu na shirika la usalama wa usafiri nchini Amerika (ICCT) ulionyesha kuwa watu 385,000 walifariki mapema kabla ya wakati wao kutokana na moshi unaotolewa na magari kote duniani mnamo 2015.
Ripoti hiyo ilisema magari yanayotumia dizeli yalichangia zaidi katika maafa hayo. Magari yanayotumia dizeli yaliangamiza asilimia 47 ya waathiriwa. Moshi wa dizeli uliua asilimia 66 ya waathiriwa katika mataifa ambapo idadi kubwa ya magari hutumia dizeli kama vile Ufaransa, Ujerumani, Italia na India.
Watafiti hao walibaini kuwa sekta ya usafiri huchangia asilimia 11 ya vifo vyote vinavyotokana na hewa chafu.
Kulingana na ripoti, watu 114,000 walifariki nchini China kutokana na moshi unaotokana na magari mnamo 2015 huku watu 22,000 wakiaga dunia nchini Amerika.
Ripoti kuhusu Hali ya Uchumi ya 2018 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) ilionyesha kuwa zaidi ya watu 14 milioni walienda katika hospitali mbalimbali nchini wakiwa na matatizo ya kupumua.
Hewa chafu inayotolewa na vyombo vya usafiri inatarajiwa kuongezeka mara tatu kati ya 2010 na 2030 kulingana na Mpango wa Serikali wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Hali ya Anga 2018-2022.
Kulingana na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, lililoko na Makao Makuu yake jijini Nairobi, Joyce Msuya, watu wanaopumua mara kwa mara hewa chafu inayotolewa na magari pia wako hatarini kuugua maradhi ya kusahau, maarufu ‘dimensia’.
“Madhara yanayosababishwa na moshi wa magari yanatarajiwa kuongezeka maradufu miaka michache ijayo kwa sababu watu wananunua magari kila uchao. Wingi wa magari umesababisha misongamano barabarani, miili yetu inaumia na uchumi pia unadorora,” anasema Bi Msuya.
Mnamo 2012, Kenya ilikuwa na magari milioni mbili lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi magari milioni nane kufikia 2050, kulingana na ripoti ya Shirika la Kudhibiti Kawi nchini (ERC).
Magari mapya
Ripoti ya Hali ya Uchumi ya 2019 iliyotolewa na KNBS inaonyesha kwamba magari mapya 297,289 yalisajiliwa mwaka 2018 ikilinganishwa na magari 282,672 mnamo 2017.
Hiyo ni sawa na nyongeza ya asilimia 5.2.
Kenya ingali inajikokota katika kutekeleza Kifungu cha 27 (2) cha sheria kuhusu Ubora wa Hewa iliyopitishwa mnamo 2014.
Sheria hiyo inataka magari ya usafiri wa umma na malori ya kubeba mizigo kukaguliwa kila mwaka ili kubaini usalama wa moshi yanayotoa.
Sheria hiyo pia inataka magari ya kibinafsi yaliyo na miaka mitano na zaidi tangu kuingia sokoni, kukaguliwa kila baada ya miaka miwili.
Katika kikao kilichohudhuriwa na wawakilishi kutoka mataifa ya Afrika Mashariki kilichoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (Unep) mnamo Juni mwaka huu, ilibainika kuwa sheria hafifu na utepetevu katika utekelezaji wa sheria zilizopo, kunachangia katika uagizaji na kuundwa kwa magari yasiyo kuwa na teknolojia ya kuhakikisha kuwa yanatoa moshi salama kwa mazingira na binadamu.
Mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi yaliafikiana kwa kauli moja kubuni sheria itakayohakikisha kuwa magari yanayoingizwa katika ukanda wa Afrika Mashariki yana teknolojia inayosafisha moshi.