Tangatanga wamtishia Mutyambai, wataka Matiang’i ajiuzulu

IBRAHIM ORUKO na NDUNGU GACHANE

WABUNGE wa Chama cha Jubilee wanaoegemea mrengo wa Tangatanga, sasa wametishia kumwadhibu Inspekta Mkuu wa Polisi, Bw Hillary Mutyambai wakidai anatumia mamlaka yake kinyume cha kisheria.

Wabunge hao wapatao 40 pia walirejelea wito wao kumtaka Katibu wa Wizara ya Usalama wa Nchi, Dkt Karanja Kibicho na Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i wang’atuke mamlakani kwa madai kwamba wanawabagua kwa misingi ya kisiasa.

Wakizungumza katika majengo ya bungejana, walidai Bw Mutyambai alishawishiwa na wakuu katika Afisi ya Rais kumhangaisha Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro na hivyo basi wataanzisha mchakato wa kumwondoa mamlakani.

Bw Nyoro alikamatwa na polisi usiku wa kuamkia jana baada ya kukwepa mtego wao tangu Jumapili alipodaiwa kuzua rabsha katika Kanisa Katoliki la Gitui, Kaunti ya Murang’a.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichungwa na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, wabunge hao walidai Idara ya Polisi imegeuzwa kuwa chombo cha kukandamiza baadhi ya viongozi nchini.

“Ukatili wa polisi na utumiaji wa idara hiyo kisiasa limekuwa jambo la kawaida tangu Bw Mutyambai alipochukua usukani kuwa Inspekta Mkuu. Tunakashifu mienendo hii kwa sababu ni kinyume cha matakwa ya kikatiba,” akadai Bw Cheruiyot.

Kwa upande mwingine, Bw Ichungwa alitishia kwamba maafisa wa umma wanaoruhusu idara wanazosimamia zitumiwe kudhulumu wengine kisiasa, watachukuliwa hatua kibinafsi na wabunge kwani kile wanachofanya ni sawa na uharibifu wa mali za umma.

“Tutafanya idara ya polisi iwe huru kutoka kwa afisi ya Rais ili kuzuia isitumiwe na watu kama Dkt Kibicho,” akasema.

Lakini Bw Kibicho alipuuza madai ya wanasiasa hao akisema amekuwa akilaumiwa na viongozi kila wakijipata matatani na akawataka wasimuingize kwenye mizozo yao.

“Watu wanapojikuta taabani, watatue shida zao bila kumhusisha Kibicho. Wananilaumu kwa sababu wanataka kugeuza suala la kihalifu liwe la kisiasa,” akasema.

Huku hayo yakijiri, imefichuka wakuu serikalini waliamua kutoendeleza mashtaka dhidi ya Bw Nyoro baada ya kubaini kwamba hatua hiyo ingemzidishia umaarufu wa kisiasa.

Usiku wa kuamkia jana, kulikuwa na maandamano Murang’a ambapo wafuasi wa mbunge huyo chipukizi waliziba barabara kwa kuwasha moto njiani, hali iliyolazimu polisi kuwatawanya kwa kutumia vitoa machozi.

Duru zilisema suala hilo la kutaka kumkamata Bw Nyoro liliingizwa siasa tele na kama serikali ingeendeleza kesi dhidi yake, angezidi kugonga vichwa vya habari kila kukicha na kupata umaarufu mkubwa.

“Tunaamini Mbunge huyo atashtakiwa baadaye, lakini kwa sasa kutokana na joto la kisiasa lililotokea, wakubwa wetu waliona ni busara kutumia mbinu nyingine kutatua suala hilo,” akasema afisa aliyeomba asitajwe jina kwani hana idhini kuzungumzia suala hilo kwa wanahabari.

Viongozi wa Tangatanga vilevile, wamefufua wito wao wa kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuitisha mkutano wa wabunge wa chama hicho ili kumaliza mizozo na kuimarisha mazingira ya utawala.

Wakiongozwa na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, Alice Wahome (Kandara) na Seneta wa Murang’a Irungu Kangata, viongozi hao walisema kukamatwa, kuhangaishwa na kutishwa kwa baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya na polisi ni sehemu ya njama za kuvuruga Jubilee zinazoendelezwa na wanasiasa wenzao kupitia polisi.

Bw Kangata alisema mashtaka ambayo polisi walitaka kumfungulia Bw Nyoro hayana msingi akidai hawakuwa na ushahidi wowote. Mbunge huyo aliachiliwa jana bila kushtakiwa.

Seneta huyo alisema vinara wa chama cha Jubilee wanapaswa kukabiliana na masuala yanayozua mgawanyiko chamani akisema anataka chama hicho kuwa na amani na kuhakikisha Kenya inastawi.

Bw Nyoro alimtaka Rais kuitisha mdahalo wa kuunganisha chama akilaumu kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga kwa kuvuruga chama tawala.

Lakini mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu alisema mzozo katika chama hicho hauwezi kutatuliwa na mkutano wa kundi la wabunge akisema ni tatizo la eneo la Mlima Kenya ambalo limesababishwa na Naibu Rais.

Habari zinazohusiana na hii