Tobiko aagiza wanyakuzi wote wa misitu wajiondoe mara moja
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI imeshikilia msimamo mkali kwamba watu wote wanaomiliki ardhi kinyume cha sheria katika maeneo yote ya Msitu wa Mau na misitu mingine nchini lazima waondoke kwa hiari yao la sivyo serikali iwafurushe.
Licha ya baadhi ya viongozi kudai wakazi misituni wanafurushwa kwa misingi ya kisiasa, Waziri wa mazingira Bw Kariako Tobiko jana aliwaambia wabunge kwamba serikali haitarudi nyuma katika juhudi za kutunza misitu.
Alisema maafisa wataelekea katika misitu mingine baada ya zoezi la sasa la kuwaondoa walowezi kutoka msitu wa Maasai Mau kukamilika, huku akisema kufikia sasa kati ya familia 850 na 1,000 kati ya familia 3,372 zimejiondoa kwa hiari.
“Ningependa kutoa ilani kwa watu wote ambao wametwaa ardhi ya misiti kinyume cha sheria, wawe wakubwa au wadogo kwa waondoke mapema kwa sababu tutawafurusha. Baada ya kukamilisha zoezi la sasa katika eneo la Maasai Mau, tutaenda katika sehemu zingine za Msitu wa Mau kisha kuendeleza operesheni hiyo katika misitu ya Abadare, Mlima Kenya na mengineyo,” Bw Tobiko akaambia kamati ya Bunge kuhusu Mazingira katika majengo ya bunge, Nairobi.
Aliitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki kupiga jeki wizara yake katika harakati zake za kuhifadhi misitu na chemchemi ya maji kote.
“Juhudi hizi zitafaulu tu ikiwa kamati na bunge kwa jumla itaniunga mkono kwa kutenga fedha za kutosha kufadhili shughuli hiyo. Tutahitaji pesa zaidi ili kwa mfano tugharimie mpango wa kupanda miti upya katika maeneo yaliyokombolewa,” Bw Tobiko aliongeza.
Waziri huyo alilazimika kutoa hakikisho hilo baada ya Bw Mbiuki na wa wanachama wa kamati hiyo; Hillary Kosgei (Kipkelion Magharibi), Charity Kathumbi (Njoro), Ongondo Were (Kabondo Kasipul) kudai kumuuliza ni kwa nini wananchi wadogo ndio wanalengwa.
Wabunge hao walimtaka Bw Tobiko kuhakikisha kuwa watu mashuhuri walionyakua sehemu zingine katika msitu wa Mau pia watafurushwa “ili Wakenya wajue kwamba serikali inaongozwa na nia njema ya kuhifadhi msitu huo.’’
Waziri Tobiko alisema kati ya zaidi ya watu 16,000 waliopata ardhi katika msitu wa Maasai Mau, ni 716 pekee wana hatimiliki ambazo ni halali “lakini zilizopatikana kinyume cha sheria.”
Alisema faili ya uchunguzi kuhusu wale waliouza ardhi ya Mau kinyume cha sheria imewasilishwa kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na “hivi karibuni ataamua ikiwa wanapasa kushtakiwa au la.”